Fahari ya Serengeti

Tuesday, October 17, 2017

NG'OMBE 1179PARK NYIGOTI WATAIFISHWA NA MAHAKAMA

NG’OMBE 119,MBUZI 20 KUPIGWA MNADA HUKU WAMILIKI WAKIKWEPA KIFUNGO KWA KULIPA FAINI,
Na Serengeti Media Centre
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya ya SerengetI Mkoa Mara imetaifisha ng’ombe 119 na mbuzi 20 huku washitakiwa wawili wakazi wa kijiji cha Park nyigoti wakilazimika kulipa faini ya sh 800,000 kukwepa kifungo cha miaka mitatu jela.
Katika kesi ya Jinai namba 219/2017  Hakimu wa Mahakama hiyo Ismael Ngaile amemhukumu Ntagiri Manyeresa(44)mkazi wa kijiji cha Park nyigoti baada ya kutiwa  hatiani kwa makosa matatu aliyoshitakiwa nayo.
Akitoa adhabu  hiyo hakimu Ngaile amesema kwa kosa la kwanza mshitakiwa anatakiwa kulipa faini ya sh 200,000 au kifungo cha mwaka mmoja jela, kosa la pili anatakiwa kulipa faini sh 300,000 au jela miaka mitatu na kosa la tatu kulipa sh 300,000 au kifungo cha miaka mitatu.
Ambapo kama atashindwa kulipa faini atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela na kama atalipa faini atalazimika kulipa sh 800,000 ,hata hivyo amelipa na kuachiwa huru.
Hakimu Ngaile amesema ng’ombe 100  waliokamatwa ndani ya Pori la Akiba la Ikorongo watataifishwa chini ya kifungu cha 111(1)(a)(3)na (4) cha Sheria ya Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 ikisomwa pamoja na kifungu namba 351 (1)(2)na(4)cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura namba 20 ya mwaka 2012.
Katika Utetezi Mshitakiwa ameomba Mahakama imhurumie kwa kuwa umri wake ni mkubwa ,ana mke, watoto na anategemewa na mama yake,hata hivyo upande wa waendesha mashitaka umeomba adhabu kali itolewe ili liwe fundisho kwa watu wengine.
Wakati huo huo Katika kesi ya Jinai namba 220/2017 katika Mahakama hiyo hiyo mshitakiwa Nelson Museti Mwera(31)mkazi wa kijiji cha Parknyigoti amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au faini ya sh 800,000 .
Amesema  ng’ombe 19 na mbuzi 20  watataifishwa na serikali chini ya kifungu cha 111(1)(a)(3)na (4) cha Sheria ya Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 ikisomwa pamoja na kifungu namba 351 (1)(2)na(4)cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura namba 20 ya mwaka 2012.
Mapema waendesha Mashitaka Shukrani Msuya wa Senapa na koplo wa Polisi Renatus Zakeo mbele ya Hakimu mfawidhi wa Mahakama hiyo Ismael Ngaile  wameikumbusha mahakama kuwa katika kesi ya jinai namba 219/2017,Manyeresa  septemba 31,2017 saa 5 asubuhi alikamatwa eneo la Mto Manchira ndani ya Pori la Akiba la Ikorongo.
Na kuwa oktoba 4,2017 alifikishwa mahakamani kwa makosa matatu ya kuingia ndani ya Pori la Akiba bila Kibali kinyume cha Kifungu cha Sheria 15(1)(2) cha Sheria Namba 5 ya Wanyamapori ya Mwaka 2009.
Kosa la pili ni kuchunga mifugo katika Pori la Akiba kinyume na kifungu cha 18(2)(4)cha Sheria Namba 5 ya wanyamapori ya mwaka 2009,na kosa la tatu ni kuharibu uoto wa asili katika Pori la Akiba la Ikorongo kinyume na kifungu cha 18(1)(3)cha Sheria ya Wanyapori namba 5 ya mwaka 2009,ambapo alikutwa na ng’ombe 100.
Katika kesi ya jinai namba 220/2017  wameiambia Mahakama kuwa  31,2017  mshitakiwa Nelson Museti Mwera alikamatwa katika eneo la Burumbaga ndani ya Pori la Akiba la Ikorongo na kufikishwa mahakamani kwa makosa matatu ya kuingia,kuchungia ndani ya eneo hilo kinyume cha sheria na kuharibu uoto wa asili.
Mwisho.


0 comments:

Post a Comment