Fahari ya Serengeti

Thursday, June 30, 2016

KATA YA KYAMBAHI WILAYANI SERENGETI YAVUKA LENGO KATIKA KUCHANGIA MADAWATI

 Afisa Mtendaji wa kata ya Kyambahi wilayani Serengeti Mkome Manyanya akitoa ufafanuzi wa hitaji la madawati kwa sule tatu za msingi katani hapo ambapo madawati yaliyokuwa yakihitajika ni 174 yenye thamani ya zaidi sh 2 mil.lakini  katika harambee hiyo iliyoendeshwa na Mwenyekiti wa Manispaa ya Musoma William Gumbo kwa niaba ya Mbunge wa jimbo la Musoma Mathayo Manyinyi na kupata zaidi ya sh 5 milioni.


MIFUGO ICHANGIE MAENDELEO YA WATOTO KIELIMU,
Serengeti Media Centre
Jamii ya wafugaji wilayani hapa Mkoa wa Mara inatakiwa kubadili mitizamo kwa kutumia rasilimali walizonazo kusomesha watoto wao hasa wa kike badala ya kuwaoza.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Serengeti Juma Porini alisema hayo wakati wa harambee ya kuchangia madawati katika kata ya Kyambahi kwa ajili ya shule za msingi tatu zinazokabiliwa na upungufu wa madawati 174.
Alisema sekta ya mifugo inahitaji wasomi na wataalam mbalimbali ambao watasaidia sekta hiyo kutoa matunda mazuri,lakini baadhi ya   wafugaji  wameshindwa kuwekeza kwenye elimu ya watoto wao ambao watasaidia kusukuma maendeleo ya taifa.
“Wazazi hakuna sababu ya kuwatupia lawama walimu juu ya kutofaulu kwa watoto kwenye  masomo yao,chanzo ni ninyi wenyewe kutokuona umuhimu wa kuchangia elimu na kuwaendeleza watoto,kuendelea na tabia hiyo kutalikosesha taifa wasomi …wafugaji utajiri wenu wa mifugo utumike kuleta mabadiliko kwenye familia zenu na jamii ,wekezeni kwenye elimu ndiyo faida isiyokwisha thamani,”alisema.
Akiongoza harambee hiyo iliyolenga kubata madawati 174 yenye thamani ya zaidi ya sh 2 milioni, na kufanikiwa kupata sh 5,124.200 ikiwa fedha taslimu sh3031200, ahadi sh2,093,000,  madawati 105 ahadi ngombe 3,mbuzi 4,Meya wa Manispaa ya Musoma William Gumbo alisisitiza wananchi kuwa mstari wa mbele kuchangia maendeleo yao.
“Ni wajibu wa wazazi kuandaa watoto wao kielimu ili waweze kupata mwanga wa kusaidia jamii,hakuna mtu atakuja kuwasomeshea watoto wenu hilo ni jukumu la kila mzazi,kwa kufanya hivyo mnawaandaa pia kuja kuwa wazazi bora,”alisema.
Gumbo pamoja na kuchangia madawati 10 na kuwasilisha mchango wa madawati 50 ya mbunge wa Musoma mjini Vedastus Mathayo ambaye amewekeza katika kijiji hicho,aliwataka kuachana na dhana potofu kuwa serikali itafanya kila kitu kwa msingi wa elimu bure,bali wazazi wanawajibu pia.
Mapema Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kyambahi Mukome Manyanya na Mratibu elimu kata Nemes Sianga wakitoa taarifa zao walisema mbali na upungufu wa madawati kata hiyo haina shule ya sekondari hali inayochangia utoro kwa kuwa baadhi ya wanafunzi wanatembea zaidi ya saa 4 kufika shuleni.
Walisema moja ya mkakati walionao kwa kushirikisha jamii ni kujenga shule ya sekondari ili kuwapunguzia safari ndefu wanafunzi,hali ambayo pia itachangia mazingira rafiki ya kusoma.
Ili kuhakikisha wilaya hiyo inakamilisha upungufu wa madawati zaidi ya 14,000 kwa shule za msingi na sekondari ,kila kata imepewa jukumu la kutatua matatizo yaliyopo,na wilaya inawaongezea kila kata madawati 20.
Mwisho.

 Baadhi ya viongozi wa kata,tarafa,kijiji na wilaya wakiwa wamekaa wakisubiri utaratibu.



 Mwenyekiti wa Manispaa ya Musoma William Gumbo akiwa anafungua baadhi ya michango ya wadau wa maendeleo wa ndani na nje ya kata hiyo ambapo yeye na mbunge wa Musoma mjini walichangia madawati 60.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Serengeti Naomi Nnko akisisitiza umuhimu wa jamii kuchangia shughuli za maendeleo katika maeneo yao.

WAJITOLEA KUJENGA BWENI ;KUWANUSURU WASICHANA RING'WANI SEKONDARI-SERENGETI

 Ctherine Ruge Katibu wa shirika lisilo la Kiserikali la Girls Education Support Initiatives (gesi)kushoto akiwa ameshikana mkono na baba yake mzazi Ruge na wananchi wa kata ya Magange na Ring'wani wakimpongeza kwa uamzi wake wa kusaidia watoto wa kike katika shule ya sekondari ya Ring'wani  wilayani Serengeti,shirika hilo limeanza ujenzi wa bweni la wasichana 56 ili kuwanusuru na adha wanazopata katika maisha ya upangaji kijijini,kazi hiyo itashirikisha mchango wa jamii.
 Mapokezi ya vifaa yalishirikisha viongozi wa kada mbalimbali.


WADAU WAAMUA KUJENGA BWENI KUNUSURU WASICHANA NA MIMBA,
Serengeti Media Centre.
Ili kuwanusuru wanafunzi wa shule za sekondari na mimba,utoro na ndoa za utotoni zinazoendelea wilayani hapa Mkoa wa Mara shirika lisilo la kiserikali la  Girls Education Support Initiatives(gesi)limeanza  kujenga bweni la wasichana katika sekondari ya Ring’wani.
Inadaiwa wasichana zaidi ya 36 wamekatishwa masomo wa sekondari na shule za msingi wilayani hapa wamekatishwa masomo kutokana na ujauzito,pia ndoa za utotoni na utoro huku ukosefu wa mabweni ukitajwa kama chanzo cha tatizo.
Katibu Mtendaji wa shirika hilo lenye makao makuu yake wilayani hapa Catherine Ruge alisema wameanza ujenzi wa bweni litakalosaidia watoto wa kike 56 ambao wamepanga kijijini hapo katika mazingira yanayochangia kukata tamaa ya kusoma.
“Watoto wamepanga kijijini hali inayowafanya waishi maisha kama ya unyumba,wengine wanatoka mbali kiasi kwamba hawahudhurii masomo kwa wakati,waanza wengi wanamaliza wachache na hawafanyi vizuri,ndiyo maana tukatafuta watu wa kutusaidia ili kuwanusuru watoto wa kike,”alisema.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Elibariki Mwita alisema shule hiyo inahudumia kata mbili za Ring’wani na Magange na wengi wanatoka mbali ,wanalazimika kupanga mtaani na wengine wanatembea umbali mrefu hali ambayo inawafanya waache masomo.
“Kwa kipindi cha miaka 13 wasichana 3 pekee ndiyo waliofaulu kwenda kidato cha tano,mwaka 2013 tulipokea wasichana 37 kuanza kidato cha kwanza,lakini waliopo sasa ni 20 pekee ,wasichana 9 wameacha shule  ,wawili wamerudia kidato cha pili na uhamisho wasichana watano,ukosefu wa bweni ni tatizo kubwa hapa kwa kuwa maisha ya mtaani huwageuza kuwa wake za watu,”alisema.
Na kuwa katika mitihani ya majaribio ikiwemo ya BRN wasichana wote hakuna aliyefaulu chanzo kikiwa ni ukosefu wa mabweni.
Ruge akizungumzia mkakati wao alisema ujenzi huo wanategemea kukamilika mwishoni mwa mwaka huu,”inagharimu zaidi y ash 85 milioni kama hakuna nguvu za wananchi,lakini kwa kushirikisha wananchi ambao wamekubali kuchangia nguvu kazi tunategemea kazi hiyo itagharimu zaidi y ash 50 milioni,”alisema.
Alisema shirika lao linalolenga kumsaidia mtoto wa kike wilayani humo lina malengo ya kusaidia shule mbalimbali kadri wanavyopata msaada,aliomba wadau wengine kuwekeza kwenye elimu kama njia pekee ya kumkomboa mtoto wa kike anayekabiliwa na vikwazo vingi ikiwemo mila na desturi.
Diwani wa kata ya Magange George Mahemba alisema kupitia msaada huo wananchi wamekubali kuchangia ili kuwanusuru watoto wa kike .
Mwisho.

 Catherine akiwa na wazazi na baadhi ya viongozi wa kijiji na kata ya Ring'wani na Magange baada ya mtoto wa kike kujitokeza kuwasaidia wadogo zake ili waweze kupata mazingira mazuri ya kuishi na wasome.








WAKAZI WA KATA YA BUSAWE WILAYANI SERENGETI WAJENGA KITUO CHA AFYA NA KUKABIDHI HALMASHAURI.

 Kituo cha Afya kilichojengwa na wakazi wa kata ya Busawe wilayani Serengeti waishio nje ya wilaya,kwa kushirikiana na walio katani hapo na halmashauri wamejenga kituo cha afya chenye thamani ya zaidi ya sh 150 mil.na kukabidhi halmashauri kwa ajili ya uendeshaji
 Baadhi ya waliohuska na ujenzi huo wakiwa na uongozi wa wilaya kwa ajili ya kukabidhi jengo na vifaa na lengo lao ni kuhakikisha huduma za upasuaji zinafanyikia hapo.
 Wananchi wakiwa katika majengo ya kituo hicho ambacho kitakuwa kimewapunguzia adha ya kwenda umbali mrefu kupata huduma za afya.
 Viongozi wakijadiliana mambo ya kufanya.
 Dk Geogre mmoja wa watu walioweza ujenzi wa kituo hicho  akitoa maelezo kabla ya kukabidhi vifaa vya afya
 Wakikabidhi vifaa
makabidhiano ya vifaa

Friday, June 24, 2016

MBUGE YA KUANGAMIZA GUGU LA KIDUHA YAANZA KUSAMBAZWA KWA WAKULIMA WA MAHINDI SERENGETI

Mratibu wa Kampuni ya African Agricultural Technology Foundation (AATF)yenye makao makuu yake  jijini Nairobi  Nchini Kenya na Ofisi ndogo jijini Mwanza, Jovita Joachim wakati wa sherehe ya Mkulima katika kijiji cha Rung’abure  ,akielezea madhara ya gugu la Kiduha linavyoathiri kilimo cha zao la Mahindi wilayani humo.


MBEGU KINZANI ZASAIDIA KUTOKOMEZA GUGU LA KIDUHA,
Serengeti Media Centre Media.
Wakulima wa kata nane wilayani hapa wameanzisha kampeini ya kutokomeza gugu hatari la Kiduha ambalo limekuwa likiathiri uzalishaji wa zao hilo la chakula na biashara.
Kata hizo ni pamoja na Rung’abure,,Manchira,Morotonga,Nyamoko,Uwanja wa ndege,Geitasamo,Mbalibali na Machochwe.
Gugu hilo ambalo inadaiwa kusambaa kwa kasi na kuathiri ukuaji na uzalishaji wa zao la mahindi ,inadaiwa mbegu zake hukaa chini kwa zaidi ya miaka 15 bila kuota na limeathiri wakulima katika nchi nyingi za Afrika ikiwemo Tanzania.
Akitoa ufafanuzi wa kampeini hiyo Mratibu wa Kampuni ya African Agricultural Technology Foundation (AATF)yenye makao makuu yake  jijini Nairobi  Nchini Kenya na Ofisi ndogo jijini Mwanza, Jovita Joachim wakati wa sherehe ya Mkulima katika kijiji cha Rung’abure jana ,alisema kutokomezwa kwa gugu hilo kutaongeza uzalishaji na kipato kwa wakulima.
“Gugu la Kiduha ni hatari sana maana mche mmoja huzalisha mbegu 40 hadi 50 milioni ,na husambaa kwa njia nyingi ikiwemo mifugo,watu na wakati mwingine upepo…na limechangia wakulima wengi kukata tamaa kutokana na uzalishaji mdogo wanaopata,”alisema.
Alisema baada ya utafiti wa makampuni mbalimbali duniani ulibaini mbegu ya (Meru IR621)ina uwezo wa kutokomeza gugu hilo kutokana na viwatilifu vyake na huongeza uzalishaji  mahindi  kwa ekari moja hadi  magunia 24 kwa kuwa inaua nguvu ya gugu hilo ambalo hufyonza maji chini ya mmea na uharibu rutuba ya ardhi.
Baadhi ya Mikoa ambayo imeathiriwa na gugu hilo ni pamoja na Tanga,Pwani,Lindi,Mtwara,Dodoma,Iringa,Mbeya,Ruvuma,Mwanza na Mara ,na kwa kanda ya ziwa wilaya za Serengeti,Butiama,Musoma,Rorya,Misungwi,Magu,Kwimba,Bunda,Rorya na Butiama.
Kwa Upande wake Mkuu wa wilaya hiyo Maftah Ally aliwataka wakulima kuacha kilimo cha  mazoea na kwa kutumia teknolojia hiyo watafanikiwa kutekeleza kampeini iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa huo Magesa Mulongo ya kujilisha mwenyewe.
“Hakuna haja ya kuhitaji msaada wa chakula kwa wakazi wa wilaya hii kwa kuwa mvua toka agosti mwaka jana hadi sasa inanyesha,tumieni teknolojia ya kisasa ili muongeze mavuno na soko lipo kwa kuwa kuna viwanda vya kusaga unga vinafunguliwa wilayani humo,”alisema.
Akizungumzia mafanikio ya teknolojia hiyo Tatu Nyamuronga mkulima kutoka kijiji cha Miseke alisema yeye ameweza kupata magunia 27 kwa ekari moja ,wakati awali alikuwa akivuna magunia 5hadi 7.
Naye Magoiga Nyamuhanga mkulima kutoka Rung’abure alishauri elimu itolewe zaidi kwa kuwa wakulima  walikuwa wakitilia shaka mbegu kutoota.
Mwisho.


Baadhi ya maafisa wa kilimo wakielezea athari ya gugu la kiduha kwa zao la mahindi.

Baadhi ya wakulima wakiangalia mahindi katika moja ya shamba la mkulima wa kijiji cha Rung'abure.
Burudani mbalimbali zilikuwepo ikiwemo chakula na vinywaji.