Fahari ya Serengeti

Sunday, June 19, 2016

TEMBO WAVAMIA KATA TATU WILAYANI SERENGETI,WAUA NA KUHARIBU MASHAMBA YA MAZAO.




Serengeti Media Centre.
Kundi kubwa la Tembo limevamia kata tatu wilayani hapa na kusababisha kifo cha mkazi wa Kijiji cha Nyamatoke na kuharibu mashamba ya mazao mbalimbali.
Mkuu wa Wilaya hiyo Maftah Ally amethibitisha kutokea kwa matukio hayo na kumtaja aliyeuawa kuwa ni Tano Ndago(60)Mkazi wa kitongoji cha Tang’usa kijiji cha Kemugesi juni 17 majira ya kati ya saa 1.30 usiku wakati akilinda nyani wasile  shamba lake la mahindi.
Alisema makundi makubwa matatu ya tembo yanaonekana kuzagaa katika maeneo ya Nyamatoke,Kenokwe kata ya Mosongo,Kenyana kata ya Ring’wani na Kemugesi kata ya Nyamatare ,na askari wa wanyamapori wanaendelea kuwadhibiti ili wasilete madhara zaidi kwa wananchi.
Diwani wa Kata ya Mosongo Samson Mrimi akiongea na Serengeti Media Centre  kwa njia ya simu kuwa Ndago alivamiwa na kundi kubwa la Tembo akiwa shambani na jitihada za kukimbia hazikuzaa matunda ndipo wakamkanyaga na kusababisha kifo chake.
“Toka juni 16 kundi la tembo zaidi ya 150 walikuwa kijiji cha Kenokwe,askari wa wanyamapori alijitahidi kuwafukuza bila mafanikio na kuondoka,baadae walisema gari limeharibika…kilichofuata ni mauaji ya Ndago na kuharibu mazao mbalimbali,tathimini haijafanyika lakini hali ni mbaya sana,”alisema.
Alisema usiku kucha wananchi wanahaha kufukuza tembo kwa kupiga madebe na mabati,hata hivyo mbinu hiyo inaonekana kuzoeleka kwa tembo na hawatishiki,”shughuli za maendeleo zimesimama,mifugo haitolewi kwa hofu ya kukutana na kundi la tembo porini,kwa ujumla hali ni mbaya na hapa ni zaidi ya kilometa 30 kutoka maeneo ya hifadhi,je walioko jilani,?”alihoji.
Diwani wa kata ya Nyamatare Chembo Manyanya alisema tembo zaidi ya 100 wamekaa katika kijiji cha Kemugesi kwa siku mbili na kusababisha wananchi washindwe kupeleka mifugo yao kwenye malisho,kwenda mashambani na shughuli nyingine za kiuchumi,licha ya kutoa taarifa lakini askari wanyamapori hawajafika.
Afisawanyamapori wilaya John Lendoyan alikiri kuwa hali ni mbaya kutokana na makundi makubwa ya tembo kuvamia vijiji ambavyo viko mbali na maeneo yaliyohifadhiwa,”changamoto ni magari ,tunashindwa kwenda maeneo yote,tunaendelea kuomba misaada kwa wadau wengine ili kuwanusuru wananchi na maafa,”alisema.
Alisema kupitia kikao cha wadau wa  uhifadhi kwa ajili ya kudhibiti tembo ambacho kilishirikisha Halmashauri ya wilaya hiyo,Hifadhi ya Taifa ya Serengeti,Wma’s,Pori la Akiba Ikorongo na Grumeti Game Reseaves kuweka mkakati wa pamoja wa ulinzi ,hata hivyo hakuna utekelezaji wa pamoja  uliokwishafanyika
Kwa mjibu wa taarifa ya halmashauri kwa  kipindi cha kutoka mwaka 2009 hadi sasa zaidi ya watu 20 wameuawa na wanyamapori hasa tembo na ekari zaidi ya 6700 za mazao mbalimbali zinadaiwa kuliwa ,na uharibifu huo umekuwa ukijirudia kila msimu .
Katika baadhi ya vijiji wananchi wanatumia waya na mizinga ya nyuki pembezoni mwa mashamba yao kwa ajili ya kudhibiti tembo.
Mwisho.

0 comments:

Post a Comment