Wakiwa kizimbani
NGARIBA AKIRI KUKEKETA MTOTO MMOJA
KATI YA WATATU ALIOSOMEWA SHITAKA.
Serengeti Media Centre
Ngariba mmoja kati ya watatu waliopandishwa katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara amekiri kumkeketa
mtoto mmoja badala ya watatu aliosomewa .
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya Ismael Ngaile
Mwendesha mashitaka wa Jamhuri Jacobo Sanga akisoma hati ya mashitaka alisema
Nyahoswe Mwita(34)ngariba na mkazi wa kijiji cha Burunga kata ya Uwanja wa
ndege ,desemba 9 mwaka huu katika kijiji cha Burunga aliwakeketa watoto watatu
wenye umri wa miaka (14) (16) wanafunzi wa Serengeti sekondari na mmoja wa miaka
(12) mwanafunzi wa shule ya msingi
Burunga
Ngariba huyo Nyahoswe aliyefikishwa mahakamani hapo pamoja na
ngariba wengine wawili,mzee wa mila na msaidizi wa ngariba waliokamatwa maeneo tofauti kwa makosa ya
kukeketa watoto usiku ,bila wasiwasi alikiri kumkeketa mtoto mmoja,”nimesema mimi
nilimkeketa …..peke yake si watatu kama mlivyosema,”alimtaja.
Kukiri kwa ngariba huyo kumkeketa mtoto mmoja ilimlazimu
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya hiyo Ismael Ngaile kuahirisha kesi hiyo ya
jinai namba 233/2016 hadi desemba 14 mwaka huu,na kwa watuhumiwa wengine katika kesi za jinai
namba namba 234/2016, 235/2016
zikiahirishwa hadi desemba 16 kwa ajili ya maelezo ya awali.
Mbele ya Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa wilaya Ismael Ngaile mwendesha mashitaka aliwataja washitakiwa
wengine umri na nafasi zao katika jamii kwenye mabano kuwa ni Wasanto Buruna(56)(ngariba)mkazi
wa kijiji cha Rung’abure,Bhoke Mseti(40)mkazi wa kijiji cha kitunguruma(msaidizi
wa ngariba) ,Ryoba Magoiga(62)mkazi wa kijiji cha Koreri (Mzee wa mila)na Rhobi
Marwa(56)(ngariba)mkazi wa kijiji cha Machochwe
Alisema washitakiwa katika maeneo na muda tofauti walikamatwa
kwa makosa ya kuwafanyia ukatili watoto wa kike kinyume na kifungu namba 169A cha sheria ya
kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Akitoa ufafanuzi wa hati ya mashitaka kwa kila mmoja Mwendesha
mashitaka huyo aliiambia Mahakama hiyo iliyokuwa imefurika wasikilizaji kuwa mshitakiwa Wasanto Buruna anakabiliwa na
makosa zaidi ya matano,katika kosa la kwanza desemba 8 mwaka huu kwa
kushirikiana na Bhoke Chacha waliwakeketa watoto wa kike wawili wanafunzi wa shule ya Msingi Kitunguruma wenye
umri wa miaka (13) kinyume cha Sheria.
Katika kosa la pili ,la tatu na la nne linalomkabili Wansato
alisema desemba 8 mwaka huu aliwakeketa wanafunzi wawili wa shule ya msingi
Kitarungu na katika kosa la tano desemba 10 mwaka huu akishirikiana na Ryoba
Magoiga (mzee wa Mila) katika kijiji cha Koreri walimfanyia ukeketaji mtoto wa
miaka (13)mwanafunzi wa shule ya Msingi Kambarage.
Akifafanua mashitaka yanayomkabili Rhobi Marwa ngariba
kutoka Machochwe,alisema desemba 9 mwaka huu alimkeketa mtoto mwenye umri wa
miaka (14)mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi Kambarage na siku hiyo
hiyo alimkeketa mtoto mwenye miaka (13) anayesoma shule ya Msingi Mbirikiri.
Mshitakiwa Ryoba Marwa (mzee wa mila)alipewa dhamana na
Hakimu Anamaria Mushi ,huku washitakiwa wengine wakikosa dhamana kwa madai kuwa
wakiachiwa wanaweza kwenda kuendelea kuwakeketa watoto ,hivyo watakaa mahabusu
hadi desemba 16 mwaka huu wakati kesi yao itakaposomwa maelezo ya awali.
Katika hatua nyingine kesi inayowakabili Chacha Kiheta na mkewe
Mugusuhi Chacha imeingia katika hatua nyingine baada ya kusomewa maelezo ya
awali.
Mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa wilaya Ismael Ngaile
mwendesha mashitaka wa Jamhuri Jacobo Sanga akisoma maelezo ya awali alisema kuwa
mnano desemba 21 ya mwaka 2015 washitakiwa walifanya ukatili dhidi ya watoto
wao watatu wenye umri wa miaka 17,16 na 13.
Hata hivyo mara baada ya kusomewa maelezo hayo wote walikana
na kesi kuahirishwa hadi desemba 16 mwaka huu ambapo jamhuri imekamilisha
upelelezi na itawasilisha mashahidi wake,washitakiwa wamerudishwa mahabusu hadi
tarehe hiyo.
Wazee wa mila na ngariba licha ya kupata mafunzo ya athari za
ukeketaji kupitia Mradi wa Tokomeza Ukeketaji Serengeti unaotekelezwa na amref
health africa tanzania na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC) na kuapa
mbele ya viongozi wa wilaya kuachana na kazi hiyo,wamebuni mbinu ya kuendesha
ukeketaji usiku wa manane.
Mwisho.
Wanashuka kwenye gari ili wapande kizimbani
Wakielekea mahabusu baada ya kukosa dhamana hadi desemba 16 mwaka huu
Ngariba Wansato akitoka mahakamani kuelekea mahabusu
Anapanda gari la polisi tayari kwa kuanza safari ya kwenda mahabusu
Safari ya kwenda mahabusu
Kaka hongera kwa kazi nzuri, naona kuna haja ya kuzidi kuipublish website yako ili watu waijue na waanze kuitembelea.
ReplyDeleteNa kwa kuwa Ukeketaji ni janga kubwana pengine la kitaifa, kuwepo na nguvu za ziada kuifanya blog hii ionwe na watanzania wote. Najua inawezekana.
ReplyDelete