Fahari ya Serengeti

Monday, December 19, 2016

HUKUMU KESI YA NGARIBA NA MWENZAKE DESEMBA 21 MWAKA HUU

Nyakaho Msamba(46)mkazi wa Mesaga  ngariba anayesubiri hukumu desemba 21 mwaka huu baada ya kumkeketa mtoto wa miaka 15 kwa kushirikiana na bibi yake ambaye ni mshitakiwa

HUKUMU YA KESI YA NGARIBA NA MWENZAKE DESEMBA 21 MWAKA HUU,
Serengeti Media Centre.
Hukumu ya kesi inayowakabili Nyabitara Masaka(64)(nyanya wa mtoto) na Nyakaho Msamba(46)(ngariba) wakazi wa kijiji cha Mesaga wilayani Serengeti wanaoshitakiwa kwa kosa la kumkeketa mtoto wa miaka 16 kusomwa desemba 21 mwaka.
Katika kesi hiyo ya jinai Namba 206/2016 Jamhuri ilikuwa na mashahidi watatu ikiwemo  taarifa ya daktari aliyemfanyia uchunguzi mtoto huyo,askari wa dawati la jinsia na ofisa mtendaji wa kijiji aliyebaini kufanyika kwa ukatili huo, kwa upande wa washitakiwa hawakuwa na shahidi.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya Ismael Ngaile Daktari Nelson Lwwowa wa hospitali Teule ya wilaya ya Nyerere aliyemfanyia uchunguzi mtoto aliyekeketwa akiongozwa na Mwendesha mashitaka wa Polisi Jakobo Sanga,aliiambia Mahakama kuwa  uchunguzi wake ulibaini mtoto huyo amekeketwa.
 Alisema mbali na kumkeketa walikwangua baadhi ya sehemu za siri ,kitaalam ni rahisi kupata matatizo ya uzazi wakati wa kujifungua,kuathirika kisaikolojia na kupoteza kumbukumbu kwa kuwa mishipa ya fahamu imekatwa bila kufuata utaratibu wa kitabibu.
Kwa upande wa shahidi namba mbili wa jamhuri Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mesaga Sagenda Bodo aliiambia mahakama kuwa baada ya kupata taarifa za siri kuhusiana na kukeketwa kwa mtoto huyo alifuatilia nyumbani kwa mshitakiwa  Nyabitara Masaka ambaye ni nyanya wa mtoto huyo na kumkuta mshitakiwa wa pili Nyakaho Msamba ambaye ni Ngariba wamemshikilia mtoto huyo akilia  huku damu zikivuja sehemu za siri.
Aliwachukua hadi ofisi ya Kijiji na kumwita mhudumu wa afya ya msingi ambaye alibaini amekeketwa na kupiga simu Kituo Kidogo cha Polisi Majimoto ambao walifika na kuwakamata washitakiwa na kuwapeleka kituoni.
Akitoa ushahidi WP Sijali Nyambuche toka dawati la polisi Mugumu aliiambia mahakama kuwa baada ya kufikishwa na kupata maelezo ya awali alilazimika kumpeleka mtoto hospitali kwa ajili ya uchunguzi na matibabu mengine na kubaini amekeketwa.
Alisema baada ya daktari kuthibitisha kuwa mtoto huyo amekeketwa washitakiwa walipofikishwa kituoni aliwahoji na  bibi yake akikiri kumkeketa mjukuu wake kama yeye alivyokeketwa kwa lengo la kutimiza mila lakini hawakujua kama ni kosa .
Alifafanua kuwa ngariba alikiri kuitwa na bibi yake na mtoto na kumwomba amkekete mjukuu wake ili aweze kutimiza mila za kabila la wangoreme,hata hivyo washitakiwa hawakuwa na maswali kwa mashahidi.
Wakati huo huo kesi inayowakabili ngariba Wansato Buruna,Ryoba Mrimi(mzee wa mila) na Rhobi Marwa Mwita, wamekana makosa baada ya kusomewa maelezo ya awali na kuahirishwa hadi desemba 21 mwaka huu.
Ngariba Wansato Buruna ameendelea kusota mahabusu kutokana na dhamana yake kuzuiliwa na jeshi la polisi na kuridhiwa na Mahakama kwa kuwa akiachiwa anaweza kuendelea kukeketa watoto,kesi itaendelea desemba 21 mwaka huu , Ryoba Magoiga Mrimi Mzee wa Mila alipata dhamana.
Mwisho.









0 comments:

Post a Comment