Fahari ya Serengeti

Monday, December 19, 2016

WAFUNGWA MIAKA MITATU KWA KUMKEKETA MTOTO

 Wegesa John(60)Mkazi wa kijiji cha Nyamburi kata ya Sedeko wilaya ya Serengeti kulia akiwa na Mbusiro Ketari(530mkazi wa kijiji cha Mosongo kata ya Mosongo wilayani Serengeti wakisubiri kupelekwa magereza baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kila mmoja,kulipa faini ya sh 300,000 na baada ya kifungo kila mmoja kumlipa fidia ya sh 2 milioni mtoto wa miaka 14 waliyemkeketa.


JELA MIAKA 3 KWA KUMKEKETA MTOTO
Anthony Mayunga,Serengeti.
Wazazi wawili wa vijiji  vya  Nyamburi na Mosongo wilayani Serengeti Mkoa wa Mara wamehukumiwa vifungo vya miaka mitatu kila mmoja ,kulipa faini y ash 300,000  na baada ya kifungo  kila atatakiwa kumlipa  fidia ya sh 2 mil.mtoto wa miaka 14 waliyemkeketa.
Waliokumbwa na adhabu hiyo iliyotolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya wilaya Amaria Mushi ni Wegesa John(60)mkazi wa kijiji cha Nyamburi na Mbusiro Ketari(53)mkazi wa kijiji cha Mosongo ambao kwa pamoja wamekiri kumkeketa mtoto wa miaka 14 katika kijiji cha Nyamburi.
 Mwendesha mashitaka wa polisi  Paskael Nkenyenge akisoma hati ya mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Amaria Mushi amesema  ,desemba 15 mwaka huu katika kijiji cha Nyamburi kata ya Sedeko kwa pamoja walimkeketa mtoto wa miaka 14 kinyume na  kifungu 169(A)cha sheria kanuni ya adhabu sura 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Amesema desemba 16 mwaka huu  katika kijiji cha Nyamburi washitakiwa walikamatwa na jeshi la polisi baada ya kupata taarifa za kumfanyia ukatili mtoto huyo na kufikishwa kituo cha Polisi  Mugumu ambapo walikiri kumkeketa mtoto huyo.
Washitakiwa wameulizwa na kukiri ndipo mwendesha mashitaka akaomba mahakama iwape adhabu kali ili iwe fundisho kwa wazazi na ngariba wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Akitoa hukumu  hiyo Hakimu Mushi amesema  kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ukeketaji ambavyo vinasababisha madhara makubwa ya kiafya na kisaikolojia kwa watoto Mahakama yake imeona itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine wanaojihusisha na vitendo kama hivyo.
Amesema kwa kuwa hawakuisumbua mahakama na kutokana na shitaka waliloshitakiwa nalo kila mmoja atakwenda jela miaka mitatu,kulipa faini sh 300,000  na baada ya kutumikia adhabu hiyo watalazimika kila mmoja kumlipa mtoto waliyemsababishia madhara kwa kumkeketa sh 2 milioni,na kuwa wana haki ya kukata rufaa kama hawakuridhika na adhabu hiyo.
Mwisho.

1 comment:

  1. Ngoja wajifunze huko maana sikio la kufa halisikii dawa.

    ReplyDelete