Fahari ya Serengeti

Wednesday, December 21, 2016

UKEKETAJI WAMPELEKA NGARIBA NA BIBI JELA MIAKA KUMI

 Nyakaho Nyaisa (64) bibi wa mtoto aliyekeketwa kwa nguvu ili kutimiza mila za jamii ya Wangoreme mkazi wa kijiji cha Mesaga wilayani Serengeti akiwa mahakamani baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 10 jela na kumlipa mjukuu wake fidia ya sh 5 milioni.

 Nyabitara Magori(45)ngariba mkazi wa kijiji cha Mesaga wilayani Serengeti akilia baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 10 jela kwa kumkeketa mtoto wa miaka 16 kwa ujira wa sh 5,000 na kumsababishia madhara,akitoka gerezani anatakiwa kumlipa fidia ya sh 5 mil,kutokana na madhara aliyomsababishia


UKEKETAJI WAMPELEKA NGARIBA NA BIBI WA MTOTO JELA MIAKA 10,
Alilipwa sh 5,000.
Serengeti Media Centre
.Ngariba aliyemkeketa mtoto wa miaka 16 kwa kushirikiana na bibi yake wakazi wa kijiji cha Mesaga wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara wamehukumiwa kifungo cha miaka 10 kila mmoja na kumlipa fidia ya sh 5 milioni kwa kila mmoja.
Waliohukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya ni Nyabitara Magori(45)ngariba na Nyakaho Nyaisa (64) bibi wa mtoto aliyekeketwa kwa nguvu ili kutimiza mila za jamii ya Wangoreme.
Akitoa hukumu katika kesi ya jinai 206/2016 baada ya kusikiliza maelezo ya mwendesha mashitaka na utetezi wa washitakiwa Hakimu Ismael Ngaile alisema kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo ambavyo vinasababisha madhara kwa watoto wa kike lazima atoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.
“Kila mmoja atakwenda jela miaka kumi na mnatakiwa kumlipa fidia mtoto ya sh 5 milioni kwa kila mmoja kutokana na madhara mliyomsababishia kama ilivyoelezwa na daktari,”alisema hakimu.
Hukumuhiyo ni  ya pili kutolewa kwa ngariba na wazazi katika mahakama hiyo iliibua kilio kutoka kwa washitakiwa hao na  hofu  kwa washitakiwa wengine wenye makosa kama hayo waliokuwa mahakamani hapo.
Katika utetezi wa washitakiwa Nyakaho Nyaisa(bibi wa mtoto) aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwa kuwa ni mgonjwa wa kifua kikuu na ana familia inayomtegemea kwa upande wake Nyabitara Magori aliiambia mahakama  kupunguziwa adhabu kwa kuwa ni mjane na ana familia inayomtegemea.
Mapema mwendesha mashitaka wa Polisi Jakobo Sanga mbele ya hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo alisema  watuhumiwa walitenda kosa mnamo oktoba 18 ya mwaka huu katika kijiji cha Mesaga wilayani hapa  kwa kumkeketa mtoto wa miaka 16 kinyume cha sheria .
Alisema vitendo hivyo ni kinyume cha kifungu cha 169(A)cha sheria kanuni ya adhabu sura 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
 Sanga ameileza mahakama kuwa  kutokana na maelezo ya shitaka na ushahidi uliotolewa ikiwemo taarifa ya daktari na mtoto aliyekeketwa aliomba Mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wengine.

Mwisho.




0 comments:

Post a Comment