Fahari ya Serengeti

Tuesday, March 31, 2015

PICHA MBALIMBALI ZA MATUKIO

 Ng'ombe waliokamatwa kwa kuingia ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti wakitolewa kituo cha Lamai kilichoko wilayani Tarime ,baada ya wahusika kulipa faini ,hata hivyo kumekuwa na malalamiko ya kutozwa faini bila kupewa risti.
 Ng'ombe wakitolewa kambi la Lamai
 Vibarua wa kampuni ya Isaack and Son's wakilima zao la alzeti huku wakiongozwa kwa ngoma kazi hiyo inadaiwa kufanywa na kabila la wasukuma,shamba hilo lilo katika maeneo ya Gibaso wilayani Tarime,hata hivyo linadaiwa kuwa na mgogoro kati ya kampuni hiyo na wakazi wa kijiji cha Gibaso.
 Kazi na dawa ,ngoma hiyo inadaiwa huwatia hamasa ya kulima zaidi.
 Muhono Mwikwabe mkazi wa kijiji cha Rwamchanga wilaya ya Serengeti ambaye inadaiwa alipigwa risasi na askari wa pori la akiba la Ikorongo kwa madai ya kuchungia mifugo ndani ya eneo la hifadhi hiyo na kusababisha kukatwa mguu,hapo akieleza mkasa uliomkuta na kumfanya kuwa tegemezi.
Anaendelea kueleza jinsi ambavyo alitendewa unyama huo na wahusika hawajawahi kukamatwa licha ya kufahamika

 Waandishi wa habari wakiwa wanamsikiliza Mwikwabe ambaye anategemewa na familia ya watu 20.
 Kutokana na ulemavu huo hawezi kwenda shamba wala kuchunga mifugo.
 Emmanuel Salinge Mwanasheria kutoka Pingo's akiwa amekaa na Mwikwabe baada ya kusikiliza mkasa uliomkuta ha kuwa polisi hawajawahi kushughulikia masuala yake ikiwemo ng'ombe wake 40 anaodai walichukuliwa na askari wa wanyama pori wa Ikorongo.
 Kutokana na vyanzo vya maji kuchukuliwa na kuwa ndani ya Pori la Ikorongo wakazi wa vijiji vya Rwamchanga,Bonchugu na maeneo yaliyoko pembezoni mwa pori hilo wanalazimika kusomba maji na kuwanywesha ng'ombe kwa kuogopa kukamatwa.
 Adha ya maji
 Vijana kutoka kijiji cha Bonchugu wilayani Serengeti
 Mnadani Mugeta wilayani Bunda biashara ya Ng'ombe ni kubwa kwa kuwa watu hutoka maeneo mbalimbali kwa ajili ya kununua ng'ombe .
 Wanatolewa mnadani
 Biashara inaendelea hapo wanalipana baada ya kuuziana ng'ombe
 Baada ya manunuzi safari huanza kama inavyoonekana.
 wafugaji wanajadiliana
wafugaji wa  jamii ya Kitaturu wa kijiji cha Sarakwa kata ya Hunyari  wilayani Bunda wakiwa kwenye kikao cha kujadili changamoto  za ufugaji zinazowakabili ikiwa ni pamoja na kukosa malisho na maji

ANAHITAJI MSAADA



| Na Serengeti Media Centre
Godfrey Msagati(23)mkazi wa Mugumu wilaya ya Serengeti anahitaji msaada wa pesa ili aende Oceon Road kwa matibabu ya Kansa ,hapo yuko na mama yake mzazi,picha na Serengeti Media Centre

Posted  Ijumaa,Marchi27  2015 
Kwa ufupi
Nashon mzaliwa wa Mugumu Wilaya ya Serengeti kwa kipindi cha miaka saba, alikuwa akifanya kazi na kampuni moja ya Kichina iliyopo nchini.
Geofrey Msagati (23), ni Fundi Seremala ambaye ndoto za siku moja kufungua kampuni yake zimezimika na wala hajui hatima ya maisha yake kutokana na maradhi yanayomsibu.
Nashon mzaliwa wa Mugumu Wilaya ya Serengeti kwa kipindi cha miaka saba, alikuwa akifanya kazi na kampuni moja ya Kichina iliyopo nchini.
Kampuni hiyo ilishiriki kujenga majengo mbalimbali nchini ikiwamo Hoteli ya Kiwanda cha Saruji cha Kigamboni pamoja na hoteli kadhaa za kitalii Zanzibar na Mtwara, pia nyumba za wafanyakazi wa mradi wa gesi Mtwara.
Kwa sasa ‘yupo gizani’ kutokana sehemu kubwa ya maisha yake kuitumia akiwa kitandani.
Hali hiyo kwa Msagati ambaye ni mkazi wa Mtaa wa NHC mjini Mugumu, mkoani Mara inatokana na maradhi yanayoelezwa kuwa ni saratani iliyosababisha mguu wake kuvimba tangu unyayo hadi pajani, hata kushindwa kutembea wala kuvaa nguo.
Anaeleza kwamba alikutwa na mkasa huo alipokuwa kazini, wakati akiweka ‘jipsum’ katika moja ya nyumba za wafanyakazi wa mradi wa gesi Mtwara.
“Machi mwaka jana nikiwa na wenzangu mkoani Mtwara katika ujenzi wa nyumba za wafanyakazi wa mradi wa gesi, mguu wangu uliteleza kutoka mbao nilizokuwa nimekanyaga na moja ikanigonga mguuni eneo la ugoko… nilihisi maumivu makali, lakini baadaye nikaendelea na kazi,” anasimulia Msagati huku akiugulia maumivu.
Anasema siku hiyo aliendelea na kazi bila kujua kama madhara yake yatakuwa kama yalivyo sasa, lakini bahati mbaya mwajiri wangu hakutaka nikachunguze afya yangu.
“Kumbe walinihitaji mimi kwa utaalamu wangu, wala hawakujali afya yangu…. sasa nakufa huku nakijiona na hakuna msaada wowote kutoka kwao,” anasema huku akitokwa na machozi.
Msagati anaeleza kuwa matibabu aliyokuwa akipata ni dawa za maumivu, huku akiendelea na kazi na kwamba hata alipoomba fedha kwa ajili ya matibabu hakupewa na kulazimika kujitibu na baadaye akapewa nauli ya kumrudisha Dar es Salaam.
Anaeleza kuwa akiwa huko alipata huduma na dawa za maumivu hali ikawa nzuri na kurejea Zanzibar kwenye ujenzi wa hoteli moja ya kitalii.
“Nikiwa Zanzibar maumivu yalianza tena nikaenda Hospitali ya Mnazi Mmoja, nikapigwa X-ray wakasema nyonga na mifupa iko sawa na kwamba huenda ni mishipa haijakaa vizuri. Nikapewa dawa za maumivu, lakini hali ikazidi kuwa mbaya ndipo nikarudishwa Dar es Salaam bila msaada,” anasema.
Anaeleza kuwa alirudishwa Dar es Salaam huku akitembea kwa kuchechemea kutokana na maumivu, ndipo Oktoba mwaka 2014 alipoona hali inazidi kuwa mbaya aliomba atumiwe nauli na mama yake ili aweze kurudi nyumbani.
Msagati anasema Desemba mwaka jana mguu wake ukaanza kuvimba huku uwezo wa kutembea ukipungua. Alikwenda Hospitali Teule ya Nyerere, Wilaya ya Serengeti ambako madaktari walimpa rufaa kwenda KCMC Moshi mkoani Kilimanjaro kwa mabingwa wa mifupa.
“Hatukwenda kwa wakati kwa kuwa mama alikuwa ameishiwa fedha. Ikabidi mama aanze kazi ya kuomba kwa msaada kwa watu mbalimbali na makanisani. Tulipopata fedha Februari mwaka huu, nikapelekwa KCMC na madaktari walisema nina saratani kwenye mifupa, hivyo nipelekwe Taasisi ya Saratani Ocean Road Dar es Salaam,” anasema Msagati na kuongeza:
“Tatizo ni fedha maana naishi na mama ambaye anafanya biashara ndogondogo. Kuna wadogo zangu wanasoma, naye kwa kipindi chote hafanyi kazi maana ndiye anayenibeba kila hatua, kampuni niliyofanya kazi haijanisadia wala haikutaka kutupatia mikataba ya kazi, hivyo nashindwa nianzie wapi.”
Kilio cha mama
Mama wa Msagati, Lucy Magere anasema anachokiomba kwa sasa kutoka kwa Watanzania ni kunusuru maisha ya kijana wake kwa kuwa hana uwezo wala namna ya kufanya kutokana na umaskini huku akiishi kwa misaada ya watu wanaofika kumjulia hali mgonjwa.
“Kwa kipindi chote niko ndani namhudumia Msagati, sina muda wa kutoka hata kufanya ujasiriamali, mtaji wenyewe umeisha… maana hivi nililazimika kukaa hospitali kwa muda mrefu kutokana na hali yake kuwa mbaya,” anasema.
Anaomba wanaoguswa wamsaidie huku akiishauri Serikali kufuatilia kampuni za kigeni kwa kuwa hazitoi mikataba kwa wafanyakazi wake na wanapopata matatizo haziwasaidii.... “Kijana wangu kakaa na kampuni kwa miaka saba, lakini ameugua wamemtekeleza na mimi ndiyo nahangaika.”
Msagati anasema licha ya kuugua, mabosi wake hao huwa wamampigia simu mara kwa mara wakimtaka arudi kazini.
Kwa watakaoguswa wawasiliane kwa simu namba 0787 337562 au 0768522546.





Tuesday, March 24, 2015

Polisi msitumie nguvu kubwa - JK.



 Na Salome Kitomary
24th March 2015


 


Rais Jakaya Kikwete.
Rais Jakaya Kikwete, amelitaka Jeshi la Polisi kuacha kutumia nguvu kubwa katika kukamatwa wahalifu,  badala yake kuweka mbele suala la haki za binadamu.

Rais alitoa angalizo hilo jana jijini Dar es Salaam katika Chuo Kikuu cha Polisi, wakati wa hafla ya kuwapandisha vyeo askari 290 wa Zanzibar na Bara waliomaliza mafunzo ya miezi sita.

“Ipo haja ya kutumia mbinu mbalimbali katika kuwakamatwa watuhumiwa kuliko matumizi ya nguvu kubwa, jitahidini sana kutumia nguvu kiasi ili kuhakikisha hamvunji haki za binadamu,” alisema.

Rais Kikwete aliwataka polisi kujenga mazingira rafiki na wananchi ili kurahisisha utendaji kazi ikiwamo kukabiliana na uhalifu nchini kwa kupata taarifa mbalimbali kwa urahisi.

Rais Kikwete pia alisema wizi wa mtandaoni ni tatizo kubwa na zinahitajika nguvu za ziada kupambana nalo na polisi wanapaswa kujipanga kikamilifu na kwamba kwa sasa kuna matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ambayo inatumika kutukana, kukashfu watu jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

“Naliagiza Jeshi la Polisi kuchukua hatua dhidi ya wahusika wote wa matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii,” alisema.

Aidha, alisema mauaji yanayotokana na wananchi kujichukulia sheria mkononi yameongezeka kutoka 2,075 mwaka 2005 hadi 3,775 mwaka 2015, hasa  mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi ambayo yameliabisha Taifa na kwamba zinahitajika jitihada kuyamaliza.

Awali, Mkuu wa Polisi nchini, IGP Ernest Mangu, alimuomba Rais kuangalia uwezekano wa kuongeza vifaa vya kisasa kwa jeshi hilo ili liweze kutekeleza majukumu yake vizuri hasa kwa kipindi hiki ambako Taifa litashiriki kura ya maoni kwa Katiba inayopendekezwa na uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.

CHANZO: NIPASHE