Fahari ya Serengeti

Tuesday, March 24, 2015

Polisi msitumie nguvu kubwa - JK.



 Na Salome Kitomary
24th March 2015


 


Rais Jakaya Kikwete.
Rais Jakaya Kikwete, amelitaka Jeshi la Polisi kuacha kutumia nguvu kubwa katika kukamatwa wahalifu,  badala yake kuweka mbele suala la haki za binadamu.

Rais alitoa angalizo hilo jana jijini Dar es Salaam katika Chuo Kikuu cha Polisi, wakati wa hafla ya kuwapandisha vyeo askari 290 wa Zanzibar na Bara waliomaliza mafunzo ya miezi sita.

“Ipo haja ya kutumia mbinu mbalimbali katika kuwakamatwa watuhumiwa kuliko matumizi ya nguvu kubwa, jitahidini sana kutumia nguvu kiasi ili kuhakikisha hamvunji haki za binadamu,” alisema.

Rais Kikwete aliwataka polisi kujenga mazingira rafiki na wananchi ili kurahisisha utendaji kazi ikiwamo kukabiliana na uhalifu nchini kwa kupata taarifa mbalimbali kwa urahisi.

Rais Kikwete pia alisema wizi wa mtandaoni ni tatizo kubwa na zinahitajika nguvu za ziada kupambana nalo na polisi wanapaswa kujipanga kikamilifu na kwamba kwa sasa kuna matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ambayo inatumika kutukana, kukashfu watu jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

“Naliagiza Jeshi la Polisi kuchukua hatua dhidi ya wahusika wote wa matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii,” alisema.

Aidha, alisema mauaji yanayotokana na wananchi kujichukulia sheria mkononi yameongezeka kutoka 2,075 mwaka 2005 hadi 3,775 mwaka 2015, hasa  mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi ambayo yameliabisha Taifa na kwamba zinahitajika jitihada kuyamaliza.

Awali, Mkuu wa Polisi nchini, IGP Ernest Mangu, alimuomba Rais kuangalia uwezekano wa kuongeza vifaa vya kisasa kwa jeshi hilo ili liweze kutekeleza majukumu yake vizuri hasa kwa kipindi hiki ambako Taifa litashiriki kura ya maoni kwa Katiba inayopendekezwa na uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.

CHANZO: NIPASHE


0 comments:

Post a Comment