Fahari ya Serengeti

Saturday, August 22, 2015

TUJIKUMBUSHE AHADI ZILIZOTOLEWA MWAKA 2010 KABLA YA KUPOKEA ZA 2015




Na Serengeti Media Centre(SMC)
Agosti 22,2015.
 
Katika uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010 vyama vya CCM,CHADEMA na CUF vilitoa ahadi mbalimbali ambazo  walipanga kuzitekeleza katika kipindi cha miaka mitano.
Ahadi ambazo zililenga kutoa majawabu ya matatizo  ya Ujinga,Umaskini,maradhi na kuimarisha utawala bora kwa jamii.
Kabla ya kuja na ahadi mpya katika kampeini ambazo zimeanza ,hawajarudi kwa wananchi kama sehemu ya tathimini nini tuliahidi,tumetekeleza nini,bado nini,je kuna changamoto mpya,badala yake ndimi zao uhubiri mafanikio tu, kana kwamba waliyoyafanya yako mbinguni ambako hatujafika.
Kazi nyingi zilizofanyika ,utekelezaji wake umewahusisha wanancha kwa nguvu na michango yao,sioni mantiki  ya kuja na maneno mengi kwa kuwa walishiriki katika utekelezaji wake, tunategemea waje waseme kwa yake ambayo hayakufanyika ni kero kwa jamii,kwanini hayakufanyika,na kuna mkakati gani.
Serengeti Media Centre(SMC)inawarudisha kwenye ahadi za vyama vya CCM,CUF na CHADEMA walizotoa mwaka 2010  ili wananchi waone kilichoahidiwa ,kilichotekelezwa na nini wanaleta kipya,je kimezingatia matatizo yao ama yameachwa.
CCM.
Chama cha Mapinduzi (CCM)kupitia aliyekuwa mgombea wake Jakaya Kikwete alitoa ahadi 75 kubwa ,ambazo kama zingetekelezwa taifa lingesonga mbele na kuinua uchumi wa jamii.
Ujenzi reli mpya kutoka Dar es salaam mpaka mikoa ya kanda ya Ziwa(Nzega),Mikoa ya Tanga kuwa jiji la viwanda(Tangamjini)Tabora kutumia maji ya ziwa Victoria(Igunga)kulipa madeni ya chama cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga(SHIRECU)Shinyanga.
Kumaliza migogoro ya ardhi nchini(Dodoma)Wakulima kuacha kutumia jembe la mkono(Dodoma mjini)Kuwapatia trekta wakulima –kata ya Mrijo(Dodoma)Wananchi kutoondolewa Ranchi ya Misenyi(Kagera)Kujenga uwanja wa ndege Misenyi(Kagera).
Kupanua uwanja wa Ndege Bukoba(Bukoba mjini)Kujenga uwanja wa Ndege mkubwa Kigoma(Kigoma mjini)Mtukula kupatiwa umeme kutoka Uganda(Kagera)Mikoa ya Kagera,Kigoma,Lindi,Rukwa na Ruvuma kuunganishwa katika gridi ya Taifa ya Umeme(Kagera)Kuimarisha Takukuru kwa miaka mitatu(Kagera).
Hukumu kwa waliopatikana na hatia ya kuua  albino(Mbeya)Kununua Meli kubwa kuliko Mv Bukoba(Kagera)Kuanzisha benki ndogondogo kwa ajili ya wajasiliamali,Serikali kusaidia vyama vya Ushirika (Mwanza)Kuimarisha usalama Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika kwa kupeleka kikosi maalum chenye vifaa kupambana na waharifu(Mwanza),Wilaya ya Geita kuwa hadhi ya Mkoa (Geita)Kulinda Muungano kwa gharama zote(Pemba).
Kuwajengea nyumba waathirika wa mafuriko ya Kilosa(Morogoro)Kununua Meli mpya kubwa  Ziwa Nyasa(Mbeya mjini)Kujenga bandari Kasanga(Rukwa)Kumaliza tatizo la walimu miaka mitano (Songea)Kufufua Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira(Mbeya)Kuzuia hatari ya Kisiwa cha Pangani kuzama(Tanga)Kununua bajaji 400 kwa ajili ya kubeba wajawazito hasa vijijini(Iringa)Kujenga barabara yenye kiwango cha Lami kutoka Same mpaka Kisiwani,Kihunio na kuunganisha na barabara kuu ya Moshi-Dar es Salaam(Same).
Kuboresha barabara za Igunga (Tabora)Kusambaza walimu 16,000 katika shule za sekondari zenye upungufu mkubwa wa walimu(Kisesa Magu),Kusambaza vyandarua viwili kwa kila Kaya(Mbeya Mjini),Kuzipandisha hadhi hospitali maalum saba nchini kuwa za rufaa ili kupunguzia mzigo hospitali ya taifa ya Muhimbili(MNH)(Hydom Wanyama).
Kulinda amani nchini kwa kuzuia chokochoko za kidini,kikabila na kisiasa(Musoma)Kulinda haki za walemavu (Makete),Kujenga barabara ya Makete Njombe kwa kiwango cha Lami urefu wa kilometa 109(Iringa mjini),Kuenga barabara ya Lami Musoma –Mto wa Mbu(Arusha mjini),Kuanzisha jimbo la Ulyankulu(Shinyangamjini).
Kujenga barabara ya lami Manyoni Kigoma(Kaliua Tabora)Kukarabati barabara ya Arusha Moshi(Moshi mjini)Kuboresha barabara ya Handeni ,Kondoa mpaka  Singida (Dodoma)Kuwafidia wanakijiji ng’ombe waliokufa wakati wa kiangazi mwaka 2009(Longido),Vijiji vyote vilivyoko kilometa 15 kutoka kwenye bomba kuu la mradi mkuu wa maji wa Ziwa Victoria  Shinyanga-Kahama kuunganishiwa Maji,(Shinyanga).
Tatizo la umeme kufika kikomo novemba 2010 mkoa wa Arusha(Arusha mjini)Kukopesha wavuvi zana za kilimo (Busekela wilaya ya Musoma)Kuwapatia maji wakazi wa Longido(Longido)Kujenga barabara ya lami kupitia pembezoni mwa hifadhi ya Taifa ya Serengeti(Ngorongoro),Utekelezaji wa mpango wa maendeleo ya kilimo kuwasaidia wafugaji kuweza kupata na kutunza mifugo yao vizuri,(Mbulu Arusha).
Kusambaza umeme,utoaji wa huduma za afya,na uboreshaji wa kilimo cha umwagiliaji na utoaji wa ruzuku kwa wakulima 2010-2015(Babati mjini)Kuongeza mara tatu wananchi wanaonufaika na ruzuku ya pembejeo na kilimo kwa mfumo wa Vocha -(Iringa),Kuhakikisha Isimani inapata maji ya uhakika(Iringa mjini),Kulinda usalama wa wananchi kwa ujumla ili kudumisha amani na sifa ya nchi-(Ifunda).
Kutokomeza Malaria 2015(Bunda Mara)Kuwapa wanawake nafasi zaidi(Iringa)Kuisaidia Zanzibar kuendeleza miradi mbalimbali ya kijamii(Kibandamaiti mjini Zanzibar),Kusaidia Zanzibar kila panapohitajika msaada(Kibandamaiti Zanzibar)Serikali kujenga upya bandari ya Mbambabay(Ruvuma)Ununuzi wa Meli Mpya yenye  uwezo wa kubeba tani 400(Mbambabay Ruvuma).
Kufufua chama kikuu cha Ushirika cha wakulima wa Mbinga(Ruvuma),Hakutakuwa na umwagaji wa damu baada ya uchaguzi wa 2010(Dar es Salaam),Mtwara kuwa mji wa viwanda(Mtwara)Ujenzi wa kiwanda cha dawa ya viluwiluwi vya mbu,hospitali ya Tumbi kuwa ya Mkoa(Kibaha),Halmashauri ya manispaa ya Kibaha kutenga eneo maalum la viwanda(Kibaha)Ujenzi wa reli kutoka Ubungo hadi Tegeta(Dar es Salaam).
Kujenga kiwanda cha kusindika matunda mkoani Pwani(Kibaha)Kuhifadhi zao la mpunga katika ghala la Taifa (Malinyi),kujenga daraja la Kilombero lenye ukubwa wa mita 400(Morogoro)na kuboresha barabara za vijijini kwa kiwango cha  changarawe(Kilombero)
CHADEMA.
Dk Wilbroad Slaa akinadi sera za chama cha Demokrasia na Maendeleo mwaka 2010 alitoa ahadi 18 kubwa ,iwapo wangeshinda ambazo zingesaidia kukuza uchumi wa taifa na wananchi.
Kurudisha fedha za mradi wa Rada(Moshi),Kushughulikia suala la taasisi ya  kuweka na kuvuna pesa (DECI-Uwanja wa Mashujaa Moshi),Kujenga nchi isiyo na ufisadi(Mwanza)Kufufua Tanganyika ili irejee mezani kujadili Muungano na Zanzibar(Ifakara)Kufufua uchumi wa nchi kwa kutumia rasilimali zilizopo(Arusha) Kukata asilimia 20 ya mshahara wa Rais(Mwanza),Kupunguza mishahara ya wabunge kwa asilimia 15(Arusha).
Kuweka Mwenge wa uhuru jumba la Makumbusho(Kilimanjaro),Kutoa huduma bora za afya bure(Mwanza )Kufuta kodi ya vifaa vya ujenzi(Tarime)Kufuta walimu wote wa cheti cha stashahada shule za sekondari na kuleta walimu walio na shahada (Arusha)Kutoa elimu bure kuanzia shule ya awali hadi kidato cha sita(Morogoro).
Kutoa huduma za afya bure kuanzia kituo cha afya hadi hospitali ya rufaa(Mwanza)Kutoa ruzuku taasisi za kidini(Ifakara)Kusambaza magari aina ya shangingi kwa jeshi la polisi ili wakamatie wahalifu badala ya mawaziri kuyatumia(Ifakara)Mfuko wa saruji na bati kuuzwa sh 5,000(Bukoba)Kufuta pocho ya chai serikalini.
CHAMA CHA WANANCHI(CUF)
Tofauti na wagombea wengine Profesa Ibrahimu Lipumba alitoa  10 kubwa ambazo angepata ridhaa zingesaidia kutatua matatizo yanayoikabili nchi na jamii.
Kubadili Katiba na kumteua Dk Mohamed Shein kuwa Makamu wa Rais(Unguja)Elimu ya bure kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu(Tanga)Kubana matumizi kwa kupunguza ukubwa wa baraza la Mawaziri(Tanga)Kuunda serikali shirikishi(Mtwara)Kusimamia raslimali(Tanga),Kuimarisha miundo mbinu(Kidongo chekundu).
Kusimamia na kuboresha afya(Kidongo Chekundu)Kuboresha kilimo,viwanda na uwekezaji(Mtwara)Kudhibiti uuzaji wa zao la Korosho(Mtwara)na Mfuko maalum wa kusomesha walemavu.
Tusubiri ahadi za Mwaka huu zitakazodumu kwa kipindi cha miaka mitano,Tutaendelea kuwaletea taarifa mbalimbali kadri kampeini zinavyoendelea ili wananchi waweze kuchukua uamzi sahihi wakati wa kupiga kura.

Friday, August 21, 2015

UKAWA WASAMBARATIKA-SERENGETI.

 Mgombea Ubunge kwa tiketi ya ACT WAZALENDO jimbo la Serengeti Thomas Burito kulia akitinga ofisi ya afisa uchaguzi jimbo hilo kurudisha fomu.
Mgombea Ubunge kwa tiketi ya CCM Dk Stephen Kebwe akiwasilisha fomu za kugombea ubunge jimbo hilo kwa Msimamizi wa Uchaguzi wilaya Naomi Nnko.

  Mgombea Ubunge kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM)Jimbo la Serengeti Dk Stephen Kebwe akiwasilisha fomu zake kwa msimamizi wa Uchaguzi jimbo hilo Naomi Nnko.
 Msimamizi wa uchaguzi jimbo hilo akiweka sahihi kukiri kupokea fomu za mgombea huyo.
 Dk Kebwe akiagana na Msimamizi wa Uchaguzi.


 Mosena Nyambabe mgombea ubunge kwa tiketi ya Nccr Mageuzi jimbo la Serengeti akiwasilisha fomu kwa msimamizi wa Uchaguzi jimbo hilo Naomi Nnko.
 Anaweka sahihi kukiri kurudisha fomu

 Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Serengeti Naomi Nnko akiongea na Mosena Nyambabe,aliyesimama ni afisa uchaguzi jimbo hilo Prosper Ndiva akipitia fomu za mgombea huyo baada ya kurudisha.
 Mosena Nyambabe akiwa na viongozi wa chama hicho katika ofisi ya Afisa Uchaguzi wilaya.
 Msimamizi wa Uchauguzi jimbo la Serengeti Naomi Nnko akiwa na afisa uchaguzi Prosper Ndiva wakijadiliana na mgombea Ubunge jimbo hilo kwa tiketi ya Nccr Mageuzi Mosena Nyambabe,hayupo pichani.
 Mosena Nyambabe Mgombea Ubunge jimbo la Serengeti akisalimiana na Msimamizi wa Uchaguzi wilaya Naomi Nnko .
 Mgombea Ubunge jimboa la Serengeti kwa tiketi ya Nccr Mageuzi ambaye pia ni Katibu Mkuu Taifa wa Chama hicho,kushoto Mosena Nyambabe akiwa na viongozi na wanachama wa chama hicho mara baada ya kurudisha fomu ya kugombea Ubunge.
Mgombea Ubunge kupitia Act Wazalendo Thomas Burito kulia akiwa amekaa na viongozi wa chama hicho katika ofisi ya Afisa uchaguzi wilaya ya Serengeti ,muda mfupi baada ya kurusdisha fomu.


UKAWA WASAMBARATIKA-SERENGETI
Na Serengeti Media Centre
Agosti 21,2015
Umoja wa Katiba ya Wananchi(Ukawa)wilayani Serengeti Mkoa wa Mara umesambaratika,na kila chama kinachounda umoja huo kimesimamisha mgombea ubunge ,na udiwani kila kata.
Katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika wilaya hiyo vyama vya Nccr Mageuzi na Chama cha Wananchi(CUF)viliunda Umoja wao baada ya kushindwa kuelewa na uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema)waliotaka kuachiwa vijiji na vitongoji vingi,ikiwemo maeneo ambayo vyama hivyo vilikuwa vinaongoza.
Mwenyekiti wa Chadema wilaya Manawa Sang’uda akiongea na Serengeti Media Centre kwa njia ya simu amesema pamoja na kuwa hawana waraka kutoka Makao Makuu ya chama chao kuhusiana na kumteua Mgombea Ubunge jimbo hilo,wameamua kuchukua fomu na kurudisha.
“Makao makuu wameniambia kuwa jimbo hili tumepewa sisi,ingawa hawajatuma waraka wowote kuhusiana na uamzi huo….imetupa wakati mgumu sana maana katika orodha ya majina ya wagombea mkoa wa Mara,yapo majina ya wagombea tisa na jimbo hili halipo”amesema.
Serengeti Media Centre ilipomuuliza taarifa zilizozagaa jimboni humo kuwa Chama cha Nccr Mageuzi kati ya majimbo waliyoongezewa na hilo limo,alikiri kusikia taarifa hizo,”ni kweli nimesikia lakini sasa makao makuu nao wanasema mgombea wetu ndiye anayegombea”amebainisha.
Kuhusu madiwani ,Mwenyekiti amesema kuwa haitawezekana kwa kuwa muda umekwisha na wanaanza kampeini,”ni vigumu kwa sasa,Toolate”amedai Mwenyekiti.
Akiongea na SMC mgombea ubunge kupitia chama cha Nccr Mageuzi ambaye pia ni Katibu Mkuu Taifa wa Chama hicho Mosena Nyambabe,amesema yeye ndiye amepewa jimbo hilo kupitia Ukawa ,ikiwa ni kutekeleza azimio la kikao cha Umoja huo kilichofanyika Zanzibar.
“Miongoni mwa makubalino yalikuwa ni palipo na kiongozi Mkuu wa Kitaifa wa Chama anapewa nafasi ya kugombea,na ndicho killichofanyika hapa….katika majimbo kumi ya mkoa wa Mara ,sisi tumepewa moja hili la Serengeti,nadhani wenzetu wanapaswa kuheshimu makubaliano hayo na wasitake kila kitu wenyewe”anasema.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi(CUF)wilaya hiyo Joseph Rhobi amesema kuwa amejitahidi kuhakikisha vikao vinakaa ili waweze kugawana kata na namna ya kuendesha kampeini kwa umoja wao ili waweze kushinda.
“Vikao viwili tulivyokaa Chadema hawakufika kabisa,tulikutana ofisi ya Nccr mageuzi,wenzetu wakadai hawana nafasi,wana vikao vya uteuzi,wakapanga tukutane jioni ofisi ya Cuf wilaya…..hawakufika wala hawakutoa taarifa,sisi na Nccr Mageuzi tumeunda umoja wetu kama ilivyokuwa uchaguzi wa serikali za mitaa,maana hawataki”amesema kwa masikitiko.
Smc ilipotaka ufafanuzi kutoka kwa Mwenyekiti wa Chadema,amekiri kutohudhuria kwa madai kuwa alikuwa na majukumu,hata hivyo amekiri kupokea waraka kutoka makao makuu ya chama chake kuwataka wakae wagawane kata kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa.
Wakati huo huo wagombea wa vyama vya Wananchi (CUF)Emakulata Mniko,Thomas Burito(Act wazalendo)Dk Stephen Kebwe(CCM)Marwa Ryoba(Chadema)na Mosena Nyambabe(Nccr Mageuzi(Nccr Mageuzi,wamerudisha fomu za kuwania Ubunge jimbo hilo.
Mwisho.

Thursday, August 20, 2015

MAHABUSU ALIYEJINYONGA YADAIWA ALIKUWA NA MATATIZO YA AKILI,



Na Serengeti Media Centre
Agosti 20,2015
Serengeti:
Mahabusu anayedaiwa kujinyonga katika kituo cha Polisi Mugumu wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara,imebainika alijinyonga kwa shati na kusababisha mfumo wa hewa kushindwa kufanya kazi.
Katika mahojiano na Serengeti Media Centre(SMC)Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali Teule ya Nyerere wilaya hiyo Emiliana Donalda amesema  kuwa uchunguzi ulioshirikisha polisi na ndugu wa Mosi Mrigo ulibaini kuwa chanzo cha kifo chake ni kujinyonga kwa shati.
Amesema uchunguzi wa kitabibu umebaini mchubuko shingoni uliosababishwa na kujinyonga kwa shati,na shingo ilikuwa imekakamaa,mbegu za kiume zikiwa zimevuja  kutokana na kukosa hewa.
“Historia yake inaonyesha kuwa alikuwa na matatizo ya akili,kitendo cha kumkamata na kumweka katika mazingira hayo kilimfanya achanganikiwe zaidi na kuamua kujinyonga…tumekuta michubuko shingoni na mbegu za kiume zimevuja,hiyo inatokana na mfumo wa hewa kushindwa kufanya kazi”amesema.
SMC ilipomuuliza kepteni mstaafu Thomas Kemincha ambaye ni mjomba wa marehemu amesema wameamua kuchukua mwili wa marehemu kwa ajili ya mazishi baada ya kujiridhisha na uchunguzi uliofanywa na madaktari.
“Sisi wenyewe tumemchunguza sana kila sehemu na kubaini alama ya shingoni tu ambayo inatokana na kujinyonga,maeneo mengine ya mwili hapakuwa na alama inayoashiria kuwa amepigwa…sasa hivi tunaendelea na mazishi’amebainisha.
Amekiri kuwa  familia wamekubaliana na taarifa hiyo ndiyo maana wamekubali kuzika kwa kuwa chanzo kimebainishwa na wataalam,pia amekubali kuwa mpwa wake alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa akili ,tatizo ambalo lilikuwa likijirudia rudia mara kwa mara.
 Chanzo cha kukamatwa.
Kwa mjibu wa mjomba wake na mashuhuda wengine kijijini Kitembele kata ya Issenye wamesema kuwa agosti 17 mwaka huu ,marehemu alimshambulia jilani yake akimtuhumu kujisaidia haja kubwa ndani ya shamba lake la pamba ,katika shambulio hilo alimsababishia majeraha na kukimbilia kituo kidogo cha polisi Issenye.
Agosti 18 mwaka huu alikamatwa na askari polisi nyumbani kwake na kupelekwa kituo cha Polisi Mugumu ili agosti 19 apelekwe mahakamani kujibu tuhuma zilizokuwa zinamkabili,siku hiyo majira ya saa 1 jioni alijinyonga na kufariki muda mfupi baada ya kufikishwa hospitali Teule ya wilaya.
Habari kutoka kwa baadhi ya mahabusu aliowakuta ndani  zinadai alikuwa akionyesha vituko ikiwemo,kuimba,kupiga kelele na kusali ,hata alipovua shati na kujitundika walidhani utani ,hata hivyo walilazimika kupiga kelele baada ya kuona hali inabadilika na kuokolewa na askari polisi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara Philip Karangi alithibitisha kutokea kwa kifo hicho na kudai wanaendelea na uchunguzi.
Mwisho. 

Wednesday, August 19, 2015

MAHABUSU AFA KWA KUJINYONGA POLISI,



Agosti 18,2015
Mahabusu mmoja katika kituo cha polisi Mugumu wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara amekufa akidaiwa kujinyonga kwa kutumia  shati lake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara Philip Karangi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo agosti 18 majira ya saa moja jioni katika kituo cha polisi Mugumu na kumtaja aliyekufa kuwa ni Mosi Mrigo(32)mkazi wa kijiji cha Kitembele Issenye wilayani humo,ambaye alifia hospitali Teule ya Wilaya ya Nyererealikokimbizwa kwa ajili ya matibabu.
Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo Emiliana Donald amekiri mwili wa marehemu kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti,huku wakisubiri kufanyika kwa uchunguzi kujua chanzo cha kifo chake na kukiri kufariki kabla hajapata matibabu.
Kamanda Karangi akiongea na Serengeti media Centre   kwa njia ya simu ,alisema kuwa Mosi alijitundika kwa shati lake na mahabusu wenzake wakalazimika kupiga kelele na kuokolewa na polisi,ambao walimkimbiza hospitali na kufariki muda mfupi baada ya kufikishwa.
Alipoulizwa idadi ya mahabusu waliokuwemo alisema,”subiri, bado tunachunguza tutatoa taarifa kamili baadae”alisema na kukata simu.
Ndugu wadai uchunguzi
Hata hivyo Thomas Kemincha kepteni msaafu wa jeshi la Wananchi ambaye ni mjomba wa marehemu alisema kuwa hawatachukua mwili wa marehemu mpaka uchunguzi ufanyike ili kubaini chanzo cha kifo ,kwa kuwa alichukuliwa kijijini akiwa mzima.
“Agosti 18 majira ya saa 2 asubuhi alikamatwa nyumbani kwake na askari polisi wa kituo cha Issenye akidaiwa kumjeruhi jilani yake aitwaye Ngeme waliyepigana baada ya kujisaidia kwenye shamba lake la pamba ….polisi walimchukua akiwa mzima na kumleta Mugumu ili afikishwe mahakamani,usiku tunapata taarifa amekufa kifo cha mashaka,lazima uchunguzi ufanyike”alisema kepteni mstaafu.
Alisema taarifa zinazotolewa zinawapa mashaka kwa kuwa kufikia kujinyonga mapema hivyo na ndani ya mahabusu alikuwa na wenzake,na kuwa uchunguzi ndiyo utatoa majibu nini kilimsibu.
Baba yake mdogo na marehemu Juma Mosi aliimbia Serengeti Media Centre kuwa alipigiwa simu saa 12 jioni na mdogo wake kumtaarifu afuatilie kituo cha Polisi Mugumu ili amsaidie Mosi kama dhamana itahitajika.
“Kwa kuwa ilikuwa jioni nilisema nitaenda asubuhi…saa 2 usiku nikapigiwa simu na binti yangu aliyeko Kahama kuwa Mosi amepelekwa hospitali na amekufa….nilipofika hospitali mapokezi walithibitisha kuwa walimpokea na kabla ya kumhudumia alikufa,nikarudi na kutoa taarifa kwa ndugu zangu”alisema.
Kwa upande wake ndugu wa marehemu Mokonya Kikondesi alisema alifuatilia polisi kujua chanzo cha kifo ,aliambiwa kuwa alijinyonga ,na kuambiwa kama ndugu wa marehemu aandike maelezo,”niliandika maelezo ,nilipotaka kujua kosa alilokuwa anatuhumiwa nalo wakasema kujeruhi,alipigana na jilani yake,”alisema.
Serengeti Media Centre inafuatilia tukio.