Fahari ya Serengeti

Wednesday, August 19, 2015

MAHABUSU AFA KWA KUJINYONGA POLISI,



Agosti 18,2015
Mahabusu mmoja katika kituo cha polisi Mugumu wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara amekufa akidaiwa kujinyonga kwa kutumia  shati lake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara Philip Karangi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo agosti 18 majira ya saa moja jioni katika kituo cha polisi Mugumu na kumtaja aliyekufa kuwa ni Mosi Mrigo(32)mkazi wa kijiji cha Kitembele Issenye wilayani humo,ambaye alifia hospitali Teule ya Wilaya ya Nyererealikokimbizwa kwa ajili ya matibabu.
Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo Emiliana Donald amekiri mwili wa marehemu kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti,huku wakisubiri kufanyika kwa uchunguzi kujua chanzo cha kifo chake na kukiri kufariki kabla hajapata matibabu.
Kamanda Karangi akiongea na Serengeti media Centre   kwa njia ya simu ,alisema kuwa Mosi alijitundika kwa shati lake na mahabusu wenzake wakalazimika kupiga kelele na kuokolewa na polisi,ambao walimkimbiza hospitali na kufariki muda mfupi baada ya kufikishwa.
Alipoulizwa idadi ya mahabusu waliokuwemo alisema,”subiri, bado tunachunguza tutatoa taarifa kamili baadae”alisema na kukata simu.
Ndugu wadai uchunguzi
Hata hivyo Thomas Kemincha kepteni msaafu wa jeshi la Wananchi ambaye ni mjomba wa marehemu alisema kuwa hawatachukua mwili wa marehemu mpaka uchunguzi ufanyike ili kubaini chanzo cha kifo ,kwa kuwa alichukuliwa kijijini akiwa mzima.
“Agosti 18 majira ya saa 2 asubuhi alikamatwa nyumbani kwake na askari polisi wa kituo cha Issenye akidaiwa kumjeruhi jilani yake aitwaye Ngeme waliyepigana baada ya kujisaidia kwenye shamba lake la pamba ….polisi walimchukua akiwa mzima na kumleta Mugumu ili afikishwe mahakamani,usiku tunapata taarifa amekufa kifo cha mashaka,lazima uchunguzi ufanyike”alisema kepteni mstaafu.
Alisema taarifa zinazotolewa zinawapa mashaka kwa kuwa kufikia kujinyonga mapema hivyo na ndani ya mahabusu alikuwa na wenzake,na kuwa uchunguzi ndiyo utatoa majibu nini kilimsibu.
Baba yake mdogo na marehemu Juma Mosi aliimbia Serengeti Media Centre kuwa alipigiwa simu saa 12 jioni na mdogo wake kumtaarifu afuatilie kituo cha Polisi Mugumu ili amsaidie Mosi kama dhamana itahitajika.
“Kwa kuwa ilikuwa jioni nilisema nitaenda asubuhi…saa 2 usiku nikapigiwa simu na binti yangu aliyeko Kahama kuwa Mosi amepelekwa hospitali na amekufa….nilipofika hospitali mapokezi walithibitisha kuwa walimpokea na kabla ya kumhudumia alikufa,nikarudi na kutoa taarifa kwa ndugu zangu”alisema.
Kwa upande wake ndugu wa marehemu Mokonya Kikondesi alisema alifuatilia polisi kujua chanzo cha kifo ,aliambiwa kuwa alijinyonga ,na kuambiwa kama ndugu wa marehemu aandike maelezo,”niliandika maelezo ,nilipotaka kujua kosa alilokuwa anatuhumiwa nalo wakasema kujeruhi,alipigana na jilani yake,”alisema.
Serengeti Media Centre inafuatilia tukio.

0 comments:

Post a Comment