Fahari ya Serengeti

Saturday, August 29, 2015

WALIMU SERENGETI WANAIDAI SERIKALI ZAIDI YA SH 847 MIL




 Mwenyekiti wa CWT wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara Moranya Baruti akitoa tamko la chama hicho kuhusu madai yao,kulia ni kaimu katibu Juma Nyakimori,picha na Serengeti Media Centre.
Na Serengeti Media Centre(Centre)

.
Agosti 28,2015
Serengeti:Walimu wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara wanaidai halmashauri ya wilaya hiyo zaidi y ash 847 mil.za malimbikizo na mapunjo,na wametoa tamko kuunga mkono msimamo wa uongozi wa chama taifa.
Hivi karibuni Rais wa Chama hicho Taifa Gration Mkoba alitoa msimamo wa chama na kuitaka serikali kulipa mapunjo,malimbikizo,posho za madaraka kwa wakuu wa shule,kutokutekelezwa muundo mpya wa utumishi na madai mengine,kabla ya mshahara wa mwezi agosti.
Akisoma tamko la chama hicho ofisini kwake Mwenyekiti wa chama wilaya Moranya Baruti,alisema madeni hayo ni kutoka mwaka 2008,yakihusisha uhamisho,likizo,matibabu,gharama za masomo,malimbikizo ya mishahara.
“Pamoja na matamko ya serikali kuhusu malipo ya madeni ya walimu,hatujalipwa kiasi hicho,mpaka malipo ya kustaafu…serikali inatumia mamia ya mamilioni ya fedha kulipa wabunge kwa utumishi wa miaka mitano,posho  ya siku inayolingana na mshahara wa mtumishi bila kukatwa kodi,”alisema.
Baruti alisema serikali ilipitisha muundo mpya wa utumishi wa walimu mwaka 2013 ,ambao ulitakiwa kuanza kazi julai 1 mwaka 2014 ,ukiwa umefungua madaraja kwa walimu ,hadi mwaka mpya wa fedha 2015/16 walimu 1052 hawajabadilishiwa muundo huo.
“Posho ya madaraka kwa walimu wakuu wa shule za msingi,sekondari ,wakuu wa vyuo na wakuu wa idara iliyokuwa ianze kulipwa kuanzia julai 1,2015 kupitia mishahara yao ,hakuna utekelezaji wowote,”alifafanua.
Alisema ongezeko la mishahara lililotajwa na Rais Jakaya Kikwete wakati wa Mei Mosi ni kidogo kwa kuwa ni kati y ash 49,000 hadi 138,000 wka mwezi kulingana na ngazi,ambalo ni sawa na asilimia 11 “lakini mfumko wa bei ni asilimia 6.4 ,kiuhalisia ongezeko hilo ni sawa na asilimia 4.6 kiasi ambacho hakilingani na kupanda kwa gharama za maisha”alisema.
Aidha ametoa msimamo kuwa walimu wilayani hapo wako tayari kuungana na uongozi wa chama taifa kudai haki za walimu.
Akiongea na Serengeti Media Centre ,ofisa elimu ufundi wilaya Christopher Mosi alikiri kuwepo kwa deni hilo,kwa madai kuwa fedha hazitolewi kwa wakati na mahitaji kila siku yanaongezeka,na kuwa hivi karibuni wameorodhesha madeni na kuwa yanafikia zaidi ya mil.847.
Mwisho.

0 comments:

Post a Comment