Fahari ya Serengeti

Thursday, August 20, 2015

MAHABUSU ALIYEJINYONGA YADAIWA ALIKUWA NA MATATIZO YA AKILI,



Na Serengeti Media Centre
Agosti 20,2015
Serengeti:
Mahabusu anayedaiwa kujinyonga katika kituo cha Polisi Mugumu wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara,imebainika alijinyonga kwa shati na kusababisha mfumo wa hewa kushindwa kufanya kazi.
Katika mahojiano na Serengeti Media Centre(SMC)Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali Teule ya Nyerere wilaya hiyo Emiliana Donalda amesema  kuwa uchunguzi ulioshirikisha polisi na ndugu wa Mosi Mrigo ulibaini kuwa chanzo cha kifo chake ni kujinyonga kwa shati.
Amesema uchunguzi wa kitabibu umebaini mchubuko shingoni uliosababishwa na kujinyonga kwa shati,na shingo ilikuwa imekakamaa,mbegu za kiume zikiwa zimevuja  kutokana na kukosa hewa.
“Historia yake inaonyesha kuwa alikuwa na matatizo ya akili,kitendo cha kumkamata na kumweka katika mazingira hayo kilimfanya achanganikiwe zaidi na kuamua kujinyonga…tumekuta michubuko shingoni na mbegu za kiume zimevuja,hiyo inatokana na mfumo wa hewa kushindwa kufanya kazi”amesema.
SMC ilipomuuliza kepteni mstaafu Thomas Kemincha ambaye ni mjomba wa marehemu amesema wameamua kuchukua mwili wa marehemu kwa ajili ya mazishi baada ya kujiridhisha na uchunguzi uliofanywa na madaktari.
“Sisi wenyewe tumemchunguza sana kila sehemu na kubaini alama ya shingoni tu ambayo inatokana na kujinyonga,maeneo mengine ya mwili hapakuwa na alama inayoashiria kuwa amepigwa…sasa hivi tunaendelea na mazishi’amebainisha.
Amekiri kuwa  familia wamekubaliana na taarifa hiyo ndiyo maana wamekubali kuzika kwa kuwa chanzo kimebainishwa na wataalam,pia amekubali kuwa mpwa wake alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa akili ,tatizo ambalo lilikuwa likijirudia rudia mara kwa mara.
 Chanzo cha kukamatwa.
Kwa mjibu wa mjomba wake na mashuhuda wengine kijijini Kitembele kata ya Issenye wamesema kuwa agosti 17 mwaka huu ,marehemu alimshambulia jilani yake akimtuhumu kujisaidia haja kubwa ndani ya shamba lake la pamba ,katika shambulio hilo alimsababishia majeraha na kukimbilia kituo kidogo cha polisi Issenye.
Agosti 18 mwaka huu alikamatwa na askari polisi nyumbani kwake na kupelekwa kituo cha Polisi Mugumu ili agosti 19 apelekwe mahakamani kujibu tuhuma zilizokuwa zinamkabili,siku hiyo majira ya saa 1 jioni alijinyonga na kufariki muda mfupi baada ya kufikishwa hospitali Teule ya wilaya.
Habari kutoka kwa baadhi ya mahabusu aliowakuta ndani  zinadai alikuwa akionyesha vituko ikiwemo,kuimba,kupiga kelele na kusali ,hata alipovua shati na kujitundika walidhani utani ,hata hivyo walilazimika kupiga kelele baada ya kuona hali inabadilika na kuokolewa na askari polisi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara Philip Karangi alithibitisha kutokea kwa kifo hicho na kudai wanaendelea na uchunguzi.
Mwisho. 

0 comments:

Post a Comment