Fahari ya Serengeti

Thursday, March 9, 2017

WANAWAKE CHANZO CHA KUSHAMIRI UKEKETAJI


Mkuu wa wilaya ya Serengeti Nurdin Babu
Wanawake ni chachu ya ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa ukeketaji kwa kuwa ndiyo wahusika wakuu,ikiwemo kazi ya ngariba na maandalizi mengine.
Mkuu wa wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara Nurdin Babu katika maadhimisho ya  siku ya Mwanamke kiwilaya iliyofanyika kijiji cha Nyamakendo kata ya Machochwe,alisema kundi hilo linatakiwa kuwa chachu ya mabadiliko kwa kuachana na vitendo vyenye madhara kwa watoto wa kike.


Alisema kupitia Kauli mbiu ya Tanzania ya Viwanda,wanawake ni msingi wa mabadiliko ya kiuchumi yaweke msukumo katika kuwainua kiuchumi na kujiunga na viwanda vidogovidogo,lazima wawe mstari wa mbele kuwaendeleza watoto wa kike kwa kuwa hao ndiyo msingi mkuu wa viwanda vinavyotarajiwa.

“Mnatakiwa kuwa mstari wa mbele kupinga ukeketaji,ndoa za utotoni zinazochangia kukatisha masomo watoto wa kike,ninyi ndiyo mnafanya kazi ya ungariba kwa watoto ,mnawafanya wengine wanakimbia nyumbani na kuhifadhiwa katika Kituo cha Nyumba Salama,tutatekelezaje kauli mbiu hii kama hamtaki kuwekeza kwenye elimu,”alisema.

Aliwataka wazee wa mila kuachana na misimamo yao inayotweza utu wa mwanamke ikiwemo mtoto ambaye hajakeketwa kuwa hataolewa wala kufungua zizi la ng’ombe,mambo ambayo yanadidimiza uchumi wa mwanamke,familia na Taifa.

Naye Leah Mkami kutoka Jumuiya ya Kikristo Tanzania wilayani hapo  alisema maadhimisho kama hayo yaliyoanza kufanyika mwaka 1997 yanatakiwa kuleta mabadiliko kwa Mwanamke ambaye ni chachu ya mabadiliko ya kiuchumi kwa kuondoa vikwazo vinavyochangiwa na mfumo dume.

“Wanawake wanapata shida kubwa kupata mitaji ya kuendeshea biashara na kutoa misamaha ya kodi kwa biashara zilizosajiriwa ili kusaidia upatikanaji wa faida kwenye biashara inayoendeshwa”alisema.

Alisema upatikanaji wa masoko kwa bidhaa wanazozalisha ni changamoto kubwa na wengi wanakata tamaa,na hilo linaweza kuwa kikwazo kwa mkakati wa Tanzania ya viwanda.

Mapema afisa maendeleo ya Jamii wilaya Sunday Wambura alisema kupitia makusanyo ya ndani halmashauri imetoa mkopo wa sh 118 mil kwa vikundi 67 vya wanawake.

Mwisho.

0 comments:

Post a Comment