Fahari ya Serengeti

Thursday, March 9, 2017

MIGUU MIWILI YA PUNDAMILIA YAWAPELEKA JELA MIAKA 20



Serengeti Media Centre.
Wakazi wawili wa kijiji cha Nyamakendo  kata ya Machochchwe wilayani Serengeti Mkoani Mara  wamehukumiwa kifungo cha miaka kumi  jela kila mmoja  ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kukutwa na miguu miwili ya Punda milia yenye thamani ya sh.2,520,000 kinyume cha Sheria.


Waliohukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya ya Serengeti ni Amosi Malalasha (32)na Felician Sahana(35) wote wakazi wa kijiji cha Nyamakendo ambao kwa pamoja wametiwa hatiani kwa makosa makosa matatu ya uhujumu uchumi.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya Ismael Ngaile akitoa hukumu  katika kesi ya uhujumu uchumi namba 15/2016 ,amesema washitakiwa wametiwa hatiani kwa makosa  matatu waliyoshitakiwa nayo.

Ameyataja makosa hayo kuwa ni pamoja na kuingia ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti  bila kibali, kukutwa na silaha visu viwili na nyaya tatu za kutegea wanyama ndani ya hifadhi kinyume cha Sheria,na kosa la tatu ni kukutwa na nyara za taifa ,miguu miwili ya Pundamilia yenye thamani y ash 2,520,000 kinyume cha Sheria.

Hakimu Ngaile amesema Mahakama inalazimika kutoa adhabu kali kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya uhujumu uchumi, kwa kuwa vimezoeleka na vinaligharimu taifa ,hivyo kila mmoja atatumikia kifungo cha miaka kumi jela.

Mapema mwendesha mashitaka wa Jamhuri Emmanuel Zumba ameiambia Mahakama kuwa aprili 24,2016 washitakiwa walikamatwa katika eneo la Borogonja ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti ikiwa ni kinyume cha kifungu cha 21(1)(a)(2) na kifungu cha 29(1)cha Sheria ya uhifadhi wanyamapori ya mwaka 2002.

Zumba amesema washitakiwa walikutwa na visu viwili na nyaya tatu za kutegea wanyama ikiwa ni  kinyume cha kifungu cha 24(1)(b)(2) cha Sheria ya Uhifadhi ya mwaka 2002,na kosa la tatu walikutwa na nyara za serikali ,miguu miwili ya Punda milia yenye thamani ya sh 2,520,000 kinyume na kifungu 86(1)(b)(2)(ii) cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya mwaka 2002.

Ameomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa washitakiwa kutokana na kukithiri kwa vitendo vya hujumu uchumi ndani ya Hifadhi za Taifa na Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania.

Wakati huo huo Watu wawili kutoka vijiji vya Tamukeri na Motukeri wilayani hapa  wamefikishwa katika Mahakama hiyo kwa kesi mbili tofauti za kukutwa na meno ya tembo yenye jumla ya kilo 8.7 yakiwa na thamani ya sh 65.4 milioni.

Katika kesi ya uhujumu uchumi namba 41/2017 Mwendesha Mashitaka wa Jamhuri Emmanuel Zumba mbele ya Hakimu Mfawidhi wa wilaya Ismael Ngaile amemtaja  Makuru Mbumba (38)mkazi wa kijiji cha Tamukeri alikamatwa na jino moja la tembo lenye uzito wa kilo 2.8 likiwa na thamani y ash 32,700.000 Machi 3 mwaka huu majira ya  saa 6 usiku nyumbani kwake.

Katika kesi ya uhujumu uchumi namba 42/2017   Matera Simango(42)mkazi wa kijiji cha Motukeri alikamatwa  machi 3 mwaka huu nyumbani kwake akiwa na vipande vitatu vya meno ya tembo  vyenye uzito wa kilo 5.9 vikiwa na thamani  ya sh 32,700,000 kinyume cha sheria.

Amesema makosa hayo ni kinyume na kifungu namba 86 (1)na(2)(b)cha sheria ya wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009,hata hivyo washitakiwa wamekana shitaka na wamepelekwa mahabusu baada ya kukosa dhamana hadi machi 21 mwaka huu itakapotajwa tena.

Mwisho.


0 comments:

Post a Comment