Fahari ya Serengeti

Thursday, March 30, 2017

JELA KWA KUISHI NCHINI BILA KIBALI


Serengeti Media Centre

Gari la Polisi likitoka mahakama ya wilaya kupeleka mahabusu ya Mugumu waliohukumiwa vifungo na mahabusu,Picha na Serengeti Media Centre.
.Mahakama ya Hakimu Mkazi wa  wilaya ya Serengeti mkoani Mara imemhukumu Julius Chacha(50)kifungo cha mwaka mmoja au kulipa faini sh 500,000 kwa kosa la kuishi nchini bila kibali.

Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Amaria Mushi alitoa hukumu hiyo baada ya kujiridhisha pasipo kuacha mashaka juu ya ushahidi  uliotolewa mahakamani hapo na upande wa Jamhuri ,huku mshitakiwa akishindwa kuwasilisha ushahidi na vielelezo vya uhalali wake wa kukaa hapa nchini.

Hakimu Mushi alisema mshitakiwa atatakiwa kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela iwapo atashindwa kulipa faini y ash 500,000,baada ya kutiwa hatiani kwa kosa moja aliloshitakiwa nalo la kuishi  nchini bila kibali kinyume na kifungu namba 31(1) na (2) sheria ya uhamiaji sura ya 54 mapitio ya mwaka 2002 Kama ilivyofanyiwa marekebisho  sheria namba 8 ya mwaka 2015,hata hivyo amepelekwa gerezani baada ya kushindwa kulipa faini.

Mapema mwendesha mashitaka wa Polisi Paskael Nkenyenge akisoma maelezo ya shitaka katika kesi ya jinai namba 164/2016 mbele ya Mahakama hiyo alisema,mshitakiwa alikamatwa agosti 31 mwaka 2016 eneo la mugumu mjini siku moja Kabla ya maandamano yaliyoandaliwa na chama Cha Demokrasia na maendeleo(CHADEMA)maarufu kama UKUTA. 

Alisema kabla ya kukamatwa Agosti 31 mwaka 2016 aliwahi kukamatwa oktoba 21,2015 kwa kosa kama hilo na kufikishwa  katika kituo  kidogo cha polisi  Natta ,hata hivyo alitoroka baada ya kupata dhamana na  hadi alipokamatwa  wakati wa maandalizi ya maandamano ya UKUTA.

Katika mahojiano ilibainika siyo mtanzania bali ni mzaliwa wa Nchi jilani ya Kenya yeye na mama yake mzazi Angelina Okinyi ,ingawa alidai baba yake ni Mtanzania lakini hakuweza kuwasilisha vielelezo vyovyote vinavyothibitisha madai yake.

Pia ilibainika mshitakiwa Julius alisoma katika Shule ya Msingi Kombe iliyopo kata ya Kihancha na elimu ya sekondari katika Shule Tarang'anya iliyopo nchini Kenya na alihitimu  mwaka 1991.

Wakati huo huo David Mwita(41)mkazi wa Mjini Mugumu wilayani Serengeti amefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya ya Serengeti  Ismael Ngaile kwa makosa ya kupatikana na bangi kilo 13.7.

Mwendesha mashitaka wa Polisi Jakobo Sanga aliiambia mahakama hiyo kuwa mshitakiwa alikamatwa na askari Polisi machi 26 majira ya saa 4 asubuhi mwaka huu ndani ya basi akisafirisha bangi mbichi yenye uzito wa kilo 13.7 kwenda Nyamongo wilayani Tarime.

Alisema kosa la kwanza ni kupatikana na bangi kinyume na kifungu namba 15(1)(a)cha sheria namba 5 ya mwaka 2015 ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya,na kosa la pili ni kusafirisha bangi kinyume na kifungu namba 15(2) cha sheria namba 5 ya mwaka 2015 ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya.

Mshitakiwa alikana mashitaka na upelelezi umekamilika ,kesi hiyo itasikilizwa aprili 12 mwaka huu na mshitakiwa yuko mahabusu baada ya kukosa wadhamini.

Mwisho.

0 comments:

Post a Comment