Fahari ya Serengeti

Friday, January 20, 2017

WALIOPORA NG’OMBE WATATU WA AJUZA WAKUBALI YAISHE WAREJESHA,



Goshiyi Maduhu(72)kulia na Anna Masoya(51) wakazi wa Wagete kataya Rigicha wilayani Serengeti wakati wakiongea na Serengeti Media Centre jinsi walivyorudishiwa mifugo yao .Picha na Serengeti Media Centre.

Serengeti Media Centre.
Watuhumiwa  watatu waliokuwa wamekamatwa kwa kumpora  ng’ombe watatu  ajuza Goshiyi Maduhu(72)mkazi wa kijiji cha Wagete kata ya Rigicha wilayani Serengeti Mkoa wa Marabaada ya kuokoka na  kuachana ungariba wamekubali yaishe na kumrudishia mali zake.
Maduhu ambaye pia alikuwa mganga wa kienyeji(Sangoma)aliyekuwa tegemeo kwa jamii ya kabila la Wataturu ,aliokoka na kuteketeza mikoba yote ,matendo yaliyoudhi ukoo wake na kuamua kuchukua ng’ombe watatu bila ridhaa yake kwa ajili ya kufanyia matambiko.
Wakiongea na Serengeti Media Centre Maduhu na mwanaye Anna Masoya (51)walisema watuhumiwa baada ya kukamatwa ,ukoo ulikubaliana kurudisha ng’ombe wote watatu akiwemo mmoja waliyokuwa wamechinja.
“Wamerudisha ng’ombe wawili waliochukua januari 13,wa tatu wametulipa mdogo kwa kuwa wa kwetu walikuwa wameishachinja,nimekubali  ili yaishe,tunajifunza kusamehe,lakini wanatakiwa kujifunza kuheshimu haki za watu wengine,maana walifanya hivyo wakijua sisi ni wanawake hatutawafanya kitu,”alisema Maduhu.
Alisema katika tukio la kuwapora mifugo kwa nguvu walimchukua mke wa mjukuu wake ambaye anatokana na ukoo huo,kama njia ya kuwakomoa,”mjukuu wangu yuko masomoni kwa sasa alioa kwa hao watuhumiwa,akalipa mahari,lakini kuokoka kwangu kumeleta mgogoro mkubwa hadi wakamtoa kwangu,kama vile mimi sifai tena “alisema.
Hata hivyo alisema baada ya watuhumiwa kubanwa na serikali walikiri kuwa walishapokea mahari na kuamriwa kumrudisha yeye na mtoto wake mchanga, ”tumeiomba serikali kuwapa masharti ili wasije tufanyia vurugu tena,”alisema Anna Masoya.
Afisa Mtendaji wa Kata hiyo  Msami Chimaja alikiri watuhumiwa Giseni Maduhu(62)Magarinja Gitambeka(30)na Gina Gitambeka(32)wakazi wa kijiji cha Wagete kurudisha mifugo ,”tumewabana na wamerudisha ng’ombe wote watatu na binti waliyekuwa wamemtoa kwa mme wake,na wameachiwa ,”alisema.
Alisema wameyamaliza kiukoo lakini serikali imehusishwa ili kuhakikisha haki inatendekea ,huku akikemea vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyofanywa kwa kivuli cha mila.
Januari 12,na 13 mwaka huu Maduhu aliporwa ng’ombe watatu na ukoo wake kama faini  baada ya kuokoka na kuacha kazi ya ungariba na uganga wa jadi,na kushutumiwa na jamii kwa kuwa alikuwa tegemeo kwa masuala ya jadi yao.
Mwisho.



.

0 comments:

Post a Comment