Fahari ya Serengeti

Friday, January 13, 2017

NGARIBA AZIDI KUANDAMWA NA KESI ZA UKEKETAJI




 Wansato Buruna ngariba anayekabiliwa na kesi sita za ukeketaji akitoka mahakamani tayari kwenda mahabusu baada ya kesi yake kuahirisha,Picha na Serengeti Media Centre.
  
NGARIBA AZIDI KUANDAMWA NA KESI ZA UKEKETAJI,
“Watoto waliokeketwa wazidi kumtambua”
Serengeti Media Centre.
Makosa ya ukeketaji yanayomkabili ngariba Wansato Buruna(56)mkazi wa Kijiji cha Rung’abure wilayani Serengeti Mkoa wa Mara yanazidi kuongezeka kufuatia wazazi wawili kukamatwa mjini Mugumu na kutambuliwa na watoto aliowakeketa.
Kutambuliwa  na watoto  hao wawili  kunamfanya ngariba Wansato kufikisha jumla ya kesi 6 zinazomkabili katika mahakama za  Hakimu Mkazi Mfawidhi na Hakimu Mkazi wa wilaya.
Katika kesi ya jinai namba 6/2017 Wansato Buruna (ngariba)ameunganishwa na Wankuru Mwera(45)na Rose Mwera(32) wakazi wa Mtaa wa National Housing mjini Mugumu ambao wamefikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya wakikabiliwa na makosa mawili ya Ukatili wa Mtoto.
Mbele ya hakimu Mkazi wa mahakama hiyo  Ismael Ngaile mwendesha mashitaka wa jamhuri Jakobo Sanga aliiambia Mahakama kuwa washitakiwa wote watatu walitenda makosa hayo desemba 8 mwaka 2016 katika kijiji cha Mbalibali.
Alisema kwa pamoja waliwakeketa watoto wawili wenye umri wa miaka 12 kinyume na Kifungu 169 A cha Sheria Kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Aliiambia Mahakama kuwa januari 8,2017  askari polisi Mugumu walipata taarifa kutoka kwa raia wema na kuweka mtego na kufanikiwa kuwakamata washitakiwa Wankuru Mwera(45)na Rose Mwera(32)katika eneo la Mistu mjini Mugumu na kufikishwa kituo cha Polisi Mugumu.
Sanga alisema januari 9 mwaka huu walihojiwa na kufikishwa mahakamani kijibu makosa yanayowakabili,ambapo mshitakiwa Wansato Buruna(ngariba)aliunganishwa baada ya kutajwa na watoto waliokeketwa.
Washitakiwa wamekana mashitaka,ambapo  Wankuru Mwera na Rose Mwera wamepata dhamana baada ya kukidhi masharti,huku Wansato akiendelea kusota mahabusu hadi januari 20  mwaka huu kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa.
Wakati huo huo Paulo Zakaria (35)Mkazi wa Kijiji cha Mbalibali na Wansato Buruna(56)mkazi wa Rungabure ambaye ni ngariba,wamesomewa maelezo ya awali kwenye kesi namba 236/2016 ya kumfanyia ukatili mtoto mwenye umri wa miaka 14 mwanafunzi wa shule ya msingi Mbalibali.
Mwendesha mashitaka wa Jamhuri Jakobo Sanga mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Ismael Ngaile alisema, desemba 9,majira ya saa 4 usiku mwaka 2016 washitakiwa walitenda kosa la kumkeketa mtoto mwenye umri wa miaka 14.
Alisema Polisi kwa kushirikiana na uongozi wa kijiji cha Mbalibali walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa namba moja , tarehe 13 desemba 2016 alifanyiwa mahojiano na kumtaja mshitakiwa namba 2 kumkeketa mtoto huyo.
Alifafanua kuwa  desemba 14  mwaka 2016 mshitakiwa Wansato Buruna aliyeko mahabusu aliunganishwa ili kujibu mashitaka yanayomkabili,washitakiwa wamekana mashitaka na kurudishwa mahabusu hadi januari 20 mwaka huu itakapoanza kusikilizwa.
Mwisho.



0 comments:

Post a Comment