Fahari ya Serengeti

Wednesday, January 18, 2017

AKIRI KUUZIWA NYAMA YA NYUMBU NA MPANGAJI WAKE





 MWENYENYUMBA AKIRI  MAHAKAMANI KUUZIWA NYAMA YA MYUMBU NA MPANGAJI WAKE.
Serengeti Media Centre.


Mama mwenye nyumba amekiri mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara kuuziwa vipande viwili vibichi vya nyama ya nyumbu kwa thamani ya sh 2000 na mpangaji wake.
Mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo Ismael Ngaile Neema Thomas(24)mkazi wa Mtaa wa Stendi kuu baada ya kusomewa shitaka, alikiri kuuziwa nyama hiyo na Samwel Kibundali(29)mkazi wa MCU,ambaye ni mpangaji wake.
Katika kesi ya uhujumu uchumi namba 111/2016  washitakiwa Samweli Kibundali na Neema Thomas wanakabiliwa na  kosa moja la kukutwa na nyara za serikali zenye thamani ya sh.1,430,000 kinyume na kifungu namba 86 kidogo(1)na cha(2)(c)(ii)cha sheria ya wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 .
Mwendesha mashitaka wa Jamhuri Emmanuel Zumba mbele ya Hakimu wa Ngaile aliiambia mahakama kuwa Novemba 8 majira ya saa 7:15 mchana mwaka 2016 katika eneo la Stendi Mpya washitakiwa walikamatwa baada ya kukutwa na nyara za taifa.
Alisema Polisi walipata taarifa  kutoka kwa msiri wao kuwa kuna mtu anauza nyama pori eneo hilo ,nakumkuta mshitakiwa Samwel Kibundali akiwa  na ndoo ya plastiki ambayo ilikuwa imehifadhi nyara za serikali kinyume cha sheria.
“Katika upekuzi wa polisi nyumbani kwa mshitakiwa namba moja walikuta  vipande 30 vikavu vya nyama ya nyumbu na vipande viwili vibichi ambavyo aliviuza kwa mshitakiwa namba namba mbili”alisema.
Baada ya kusomwa hati ya mashitaka ,mshitakiwa namba moja Samwel Kibundali alikana kosa ,mshitakiwa namba mbili  Neema Thomas alikiri na kusisitiza”ni kweli aliniuzia vipande viwili vya nyama mbichi  kwa bei ya sh.2,000,maana huyu ni mpangaji wangu,”aliiambia mahakama.
Kesi hiyo imehairishwa hadi januari 23 mwaka huu itakapoanza kusikilizwa kwa jamhuri kuwasilisha ushahidi wake, mshitakiwa namba moja amerudishwa mahabusu na mshitakiwa namba mbili yupo nje kwa dhamana.
Mwisho.
  

0 comments:

Post a Comment