Fahari ya Serengeti

Monday, January 23, 2017

NGARIBA NA WENZAKE WAPATA WAKILI WA KUWATETEA


 Ngariba Wansato Buruna na mwenzake wakiwa mahakamani,wamepata wakili wa kuwatetea,Picha na Serengeti Media Centre

Ngariba Wansato Buruna(56) mkazi wa kijiji cha Rung’abure wilayani Serengeti Mkoa wa Mara na wenzake wanaokabiliwa na kesi tano za ukeketaji kutetewa na wakili.
Ngariba huyo ambaye alikamatwa disemba 11,saa 7 usiku mwaka 2016 katika kijiji cha Nyamirama akiwa amebebwa na pikipiki aina ya Sunlog yenye namba za usajiri T378 CAY,akiwa na vifaa vya ukeketaji,ameunganishwa na kesi nyingi kutokana na kutajwa na kutambuliwa na watoto aliowakeketa katika maeneo tofauti.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya Ismael Ngaile  Wansato na wenzake wanakabiliwa na kesi nne za jinai zenye namba 234/2016,235/2016,236/2016 na 6/2017,na katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa wilaya Amaria Mushi anakabiliwa na kesi moja.
Akiahirisha kesi hizo Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya Ismael Ngaile alisema kwa kuwa washitakiwa wanatetewa na wakili mmoja Makowe Advocates Chamber wa Musoma ,kesi zote zitasikilizwa februari 1 mwaka huu.
Katika kesi hizo washitakiwa  Wansato Buruna(56),Bhoke Mseti(40),Nyahoswe Mwita(34)Paul Zacharia(37)Wankuru Mwera(56) Rose Mwera(32) na Ryoba Magoiga(62) wote kwa pamoja wanashitakiwa kwa makosa ya Ukatili wa Mtoto kinyume na kifungu namba 169 A cha sheria kanuni ya adhabu sura ya 16 kamailivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Mwendesha mashitaka wa Jamhuri katika Mahakama Katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi wa wilaya,Jakobo Sanga alisema baadhi ya kesi wameishafunga ushahidi na zimebaki utetezi,nyingine wamebaki mashahidi wa serikali na ukoo na nyingine ndiyo zinaanza kusikilizwa.
Naye Mwendesha mashitaka wa Jamhuri Paskael Nkenyenge katika mahakama ya Hakimu Mkazi wa wilaya alisema ,kesi moja iliyoko mahakamani wamebakiza mashahidi wawili wa Jamhuri ambao ni daktari na askari mpelelezaji.
Jumla ya watu wanne akiwemo ngariba mmoja wameishahukumiwa vifungo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi na Hakimu Mkazi wa wilaya kwa makosa ya ukeketaji.
MWISHO.




0 comments:

Post a Comment