Fahari ya Serengeti

Wednesday, January 18, 2017

TUMBAKU YAANZA KUUZWA KWA MAGENDO



ULANGUZI WA TUMBAKU WADAIWA KUHUSISHA MAKUNDI MBALIMBALI,
Serengeti Media Centre.



Siku chache baada ya kubainika baadhi ya wakulima wa tumbaku wilayani Serengeti Mkoa wa Mara kuanza kuuza tumbaku kwa walanguzi kutoka nchi jilani ya Kenya,imebainika baadhi ya wanasiasa,wafanyabiashara na watumishi wa Kampuni ya Alliance One wanahusika.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Serengeti Mhandisi Juma Hamsini alisema kuwa Licha ya kuweka matangazo na kusambaza barua kwa watendaji wa vijiji na kata  kudhibiti wanunuzi ,uchunguzi wa wahusika unafanyika kwa makini ili kubaini mtandao huo.
Alisema  wamelazimika kuongeza nguvu kwenye maeneo ya vivuko ili kubaini na kudhibiti wahusika ikiwemo eneo la  Mto Mara na maeneo mengine ,”biashara hii inaweza kuwa inahusisha  watu wa kada mbalimbali ,sisi tunapambana na  watendaji  wetu  ikibainika maeneo yao  biashara hiyo inafanyika na hawachukui hatua wala kutoa taarifa lazima washughulikiwe kwa mjibu wa taratibu za utumishi,”alisema.
Hata hivyo imebainika walanguzi wa ndani ya wilaya ambao ni wanasiasa,wafanya biashara na watumishi wa kampuni ya Alliance One Tobacco hasa maafisa ugani  ndiyo wanahusika kununua tumbaku kwa sh 2,500 kwa kilo bila kuangalia daraja la zao hilo, na wakati wa msimu unaotarajiwa kuanza februari 6 mwaka huu,baadhi watauzia kampuni na  walanguzi kutoka  nchi jilani ya Kenya.
“Suala hili kila mwaka linafanyika kwa kuwa linahusisha baadhi ya viongozi na watendaji wa kampuni ,ndiyo maana walanguzi wanakuja kwa jeuri,kama hakutafanyika mikakati ya madhubuti halmashauri itakosa mapato na kampuni itapata hasara kwa kuwa wanadai Kenya bei ni nzuri,”kilisema chanzo chetu cha uhakika jina tunalo.
Baadhi ya maeneo yanayotajwa kuanza ununuzi wa  tumbaku kwa njia za magendo ni pamoja na Machochwe,Kebanchabancha,Musati na Nyansurura ,maeneo ambayo yanalima tumbaku kwa wingi wilayani hapa.
Mkuu wa wilaya hiyo Nurdin Babu alisema yeyote atakayekamatwa atafikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Zao hilo ni miongoni mwa vyanzo vya mapato ya halmashauri kutokana na ushuru wa mazao,ambapo hukusanya kati y ash 500 mil hadi 600 mil kwa msimu.
Mwisho.

0 comments:

Post a Comment