UKOO WAMPORA MIFUGO
ALIYEAMUA KUOKOKA NA KUACHANA NA UNGARIBA,
“Wanadai ni adhabu ya
kuachana na mila na desturi”
Serengeti Media
Centre.
Mkazi wa kijiji cha Wagete kata ya Rigicha wilayani
Serengeti Mkoa wa Mara Goshiyi Maduhu(72)aliyeporwa mifugo baada ya kuokoka.
Picha na Serengeti Media Centre.
Mkazi wa kijiji cha Wagete kata ya Rigicha wilayani
Serengeti Mkoa wa Mara Goshiyi Maduhu(72)ameporwa ng’ombe 3 na mmoja kuchinjwa
na ndugu kama adhabu baada ya kuokoka na
kuachana na mila na desturi.
Uamzi wa mama huyo kuachana na kazi za uganga wa jadi na
ungariba na kumrudia Mungu unadaiwa kuudhi jamii yake ya kabila la Wataturu kwa
madai kuwa walikuwa wakimtegemea kwenye kazi za mila na desturi na kukeketa watoto.
Afisa Mtendaji wa kata hiyo Musami Chimaja ,Mchungaji wa
kanisa la AIC Wagete Abel Paulo na Polisi wilayani hapa wamethibitisha kutokea
kwa matukio hayo januari 12 na 13 mwaka huu,na watuhumiwa watatu ambao ni ndugu
zake Giseni Maduhu(62)Magarinja Gitambeka(30)na Gina Gitambeka (32)wote wakazi
wa kijiji hicho wamekamatwa.
Afisa Mtendaji wa kata Chimaja alisema mara baada ya kupata
taarifa za tukio la kupora ng’ombe mmoja januari 12 mwaka huu,alifuatilia na
kukuta wameishamchinja na kuagiza warejeshe,hata hivyo badala ya kumlipa
januari 13 walienda kuchukua ng’ombe wengine wawili kama adhabu ya kuwashitaki
serikalini.
Akiongea na Serengeti Goshiyi Maduhu alisema ,”nimefanya kazi ya
uganga wa kienyeji na ungariba kwa muda mrefu,nikawa napata shida nyingi
ikiwemo kuchanganyikiwa,nikaamua kumrudia Mungu,niliteketeza mikoba yote
niliyokuwa ili nizaliwe upya,”alisema.
Alisema uamzi huo wa kuokoa roho yake na kuepuka mkono wa
serikali kwa mangariba uliudhi ukoo wake na kuanza kumfanyia vurugu,”kwenye
kikao cha mambo ya mila na desturi wakaamuru nitoe ng’ombe kwa ajili ya
matambiko,nikawaambia sihusiki na mila tena,wakaamua kuchukua kwa nguvu na
kwenda kuchinja,”alisema.
Anna Masoya (51)mwanaye alisema baada ya kutoa taarifa ya
kuporwa ng’ombe mmoja wakaamua kufuata wawili kwa nguvu huku wakidai
wataendelea kuchukua mpaka ziishe ,”tuliamua kusimama kidete mimi na mama na
kusaidiwa na mtendaji ili haki iweze kutendeka,maana mila za ukandamizaji
hazipaswi kupewa nafasi,”alisema.
Mchungaji Abel Paulo alisema ,pamoja na kujitahidi kuwaeleza
ndugu zake sababu za kuteketeza mikoba ya uganga,hawakumwelewa na kuahidi
kuchukua mali zake kama adhabu ya kuachana na mila na desturi.
Polisi wilayani hapa wamethibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa
hao na kuwa uchunguzi ukikamilika watafikishwa kwenye vyombo vya sheria kujibu
tuhuma zinazowakabili.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment