Fahari ya Serengeti

Monday, August 31, 2015

WENYE USHAHIDI WA UFISADI WA LOWASSA WAWEKE HADHARANI-



Paroko wa kanisa Katoliki Mugumu wilaya ya Serengeti Alois Magabe akiendesha ibada ya misa takatifu,picha na Serengeti Media Centre.

Na Serengeti Media Centre
Ili kuachana na siasa zisizokuwa na tija ,watu wenye ushahidi wa  mgombea urais kwa tiketi ya Chadema Edward Lowassa  kuwa ni fisadi,waweke wazi  ili vyombo vinavyohusika vichukue hatua kwa maslahi ya taifa.  
Paroko wa Kanisa Katoliki Mugumu wilaya ya Serengeti Alois Magabe katika mahubiri ya ibada takatifu ya kwanza nay a pili ,amesema kwa serikali yenye kuheshimu utawala wa sheria,haiwezekani tuhuma za mtu zikatolewa kwenye majukwaa badala ya kukabidhi vyombo vinavyohusika aweze kushughulikiwa.
“Karibu miaka kumi tunasikia fisadi fisadi,mla rushwa,hakuna anayetoka na kuweka wazi tuhuma zake wananchi tuzijue ,tunashuhudia wezi,wenye makosa na tuhuma mbalimbali wanakamatwa na kufikishwa mahakamani,wengine wananchi wanawaua ….kwanini huyu anatajwa majukwaani hafikishwi kwenye vyombo vya sheria,au ni chuki binafsi?,”amehoji.
Padri Magabe amesema siasa kama hizo haziwasaidii wananchi kufikia maamzi sahihi kwa kuwa hazina tija,”mimi si mshabiki wa Chadema wala CCM,lakini nakerwa na siasa za namna hii,nchi hii ina maadili ya viongozi,utawala bora,inakuwaje Takukuru,Usalama wa Taifa,Polisi,wapelelezi na Mahakama wapo,kwanini hafikishwi kwenye vyombo hivyo,maana majukwaa hayashughulikii waharifu,”amebainisha na kuongeza.
“Kwa wakristo katika Zaburi ya 15 inasema,Bwana ni nani atakayekaa katika hema yako,atakayefanya maskani yake katika kilima chako kitakatifu…ni mtu aendaye kwa ukamilifu na kutenda haki,asemaye kweli kwa moyo wake,asiyesingizia kwa ulimi wake,wala hakumtendea mwenziwe mabaya”amesema.
Amesema imefikia hatua hata kama kuna ukweli ama la ,wananchi hawaamini kwa kuwa suala moja linazungumzwa kwa miaka mingi,lakini anayetuhumiwa hafikishwi kwenye vyombo vya dola,maana kama amesababisha  athari kubwa kwa jamii inawezekanaje apate sifa za kugombea,na asikamatwe.
Amevitaka na vyombo vya habari visiishie kuandika na kutangaza kama wanavyosema wanasiasa,bali wafanye uchambuzi na kuanisha tuhuma zake  zake kama zipo  ili wananchi wazijue,kwa kuwa kinachosema ni fisadi,mla rushwa na hakuna anayetoka kukabidhi ushahidi vyombo husika,badala yake ni  kuichafua familia hiyo bila kosa.
Amehoji Lowassa  ana uwezo gani wa kuvishinda vyombo vya dola ,badala yake anasemwa majukwaani na ameshiriki shughuli nyingi za kijamii ,kwa kipindi chote na kushika nafasi mbalimbali ndani ya kamati zao za bunge ,na hao hao ndiyo walimchagua,sasa wananchi watawaminije kwa wanayosema leo.
Kuhusu tuhuma za utajiri anaotajwa nao,amesema Azimio la Arusha lilikuwa na misingi mizuri juu ya viongozi,kwa matajiri walibanwa na kodi,”kazi ya serikali ni kutoza kodi kwenye shughuli zake zinazompa utajiri,kama halipi waseme ili wananchi wamjue mapema ,”alisisitiza.
Akizungumzia sera ya mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi(CCM)John Magufuli  ya kuanzisha  chombo cha kushughulikia wala rushwa na mafisadi, kuwa ni ya Chadema ,hata hivyo amesema kutokana na rekodi yake iwapo atashinda anaweza kusimamia sera hiyo na kuwabana watuhumiwa wote.
Amekemea siasa za matusi na chuki zinazotolewa na viongozi na kuwataka waeleze mikakati yao  ili  wananchi wapime nani amejipanga kuliondoa taifa katika matatizo yaliyopo.
Mwisho.

Saturday, August 29, 2015

WALIMU SERENGETI WANAIDAI SERIKALI ZAIDI YA SH 847 MIL




 Mwenyekiti wa CWT wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara Moranya Baruti akitoa tamko la chama hicho kuhusu madai yao,kulia ni kaimu katibu Juma Nyakimori,picha na Serengeti Media Centre.
Na Serengeti Media Centre(Centre)

.
Agosti 28,2015
Serengeti:Walimu wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara wanaidai halmashauri ya wilaya hiyo zaidi y ash 847 mil.za malimbikizo na mapunjo,na wametoa tamko kuunga mkono msimamo wa uongozi wa chama taifa.
Hivi karibuni Rais wa Chama hicho Taifa Gration Mkoba alitoa msimamo wa chama na kuitaka serikali kulipa mapunjo,malimbikizo,posho za madaraka kwa wakuu wa shule,kutokutekelezwa muundo mpya wa utumishi na madai mengine,kabla ya mshahara wa mwezi agosti.
Akisoma tamko la chama hicho ofisini kwake Mwenyekiti wa chama wilaya Moranya Baruti,alisema madeni hayo ni kutoka mwaka 2008,yakihusisha uhamisho,likizo,matibabu,gharama za masomo,malimbikizo ya mishahara.
“Pamoja na matamko ya serikali kuhusu malipo ya madeni ya walimu,hatujalipwa kiasi hicho,mpaka malipo ya kustaafu…serikali inatumia mamia ya mamilioni ya fedha kulipa wabunge kwa utumishi wa miaka mitano,posho  ya siku inayolingana na mshahara wa mtumishi bila kukatwa kodi,”alisema.
Baruti alisema serikali ilipitisha muundo mpya wa utumishi wa walimu mwaka 2013 ,ambao ulitakiwa kuanza kazi julai 1 mwaka 2014 ,ukiwa umefungua madaraja kwa walimu ,hadi mwaka mpya wa fedha 2015/16 walimu 1052 hawajabadilishiwa muundo huo.
“Posho ya madaraka kwa walimu wakuu wa shule za msingi,sekondari ,wakuu wa vyuo na wakuu wa idara iliyokuwa ianze kulipwa kuanzia julai 1,2015 kupitia mishahara yao ,hakuna utekelezaji wowote,”alifafanua.
Alisema ongezeko la mishahara lililotajwa na Rais Jakaya Kikwete wakati wa Mei Mosi ni kidogo kwa kuwa ni kati y ash 49,000 hadi 138,000 wka mwezi kulingana na ngazi,ambalo ni sawa na asilimia 11 “lakini mfumko wa bei ni asilimia 6.4 ,kiuhalisia ongezeko hilo ni sawa na asilimia 4.6 kiasi ambacho hakilingani na kupanda kwa gharama za maisha”alisema.
Aidha ametoa msimamo kuwa walimu wilayani hapo wako tayari kuungana na uongozi wa chama taifa kudai haki za walimu.
Akiongea na Serengeti Media Centre ,ofisa elimu ufundi wilaya Christopher Mosi alikiri kuwepo kwa deni hilo,kwa madai kuwa fedha hazitolewi kwa wakati na mahitaji kila siku yanaongezeka,na kuwa hivi karibuni wameorodhesha madeni na kuwa yanafikia zaidi ya mil.847.
Mwisho.

Friday, August 28, 2015

WATEKA GARI,PIKIPIKI,KUPORA NA KUJERUH



eddted.jpg
Na SERENGETI MEDIA CENTRE(SMC)
Agosti 28,2015


 Mkazi wa kijiji cha Nyichoka wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara,Mahiri Nchagwa(30)akiwa amelazwa katika hospitali Teule ya Nyerere kufuatia kushambuliwa na watu wanaodhaniwa majambazi,picha na Serengeti Media Centre.

Watu wawili wamejeruhiwa mmoja akiwa na hali mbaya baada ya kutekwa kupigwa,kuporwa fedha na watu wanaodhaniwa  kuwa majambazi walioteka gari na pikipiki katika kijiji cha Burunga wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Mara Philip Karangi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo,agosti 27 majira ya kati ya saa 2na 3 usiku mwaka huu,watu wasiojulikana walitega magogo na kuteka pikipiki ,Hiace ,kupora na kujeruhi.
Mmoja wa majeruhi Mahiri Nchagwa(30) ambaye amelazwa katika hospitali Teule ya Nyerere wilayani hapa kutokana na kujeruhiwa vibaya,alisema alitekwa na watu watano waliokuwa na mapanga,na marungu na kumkata kata ,kumpora sh 300,000 ,simu na ufunguo wa pikipiki.
“Nilikuwa natokea mjini kuuza maziwa ,nilipofika eneo hilo niliona matawi ya miti,nikadhani kuna gari limeharibika,nikasogea taratibu nikakuta magogo makubwa yamewekwa barabarani….kusimama ghafla nikavamiwa na watu watano”alisema na kuongeza.
“Mbele yangu kulikuwa na watu wawili waliovalia kofia za kufunika uso,makoti marefu wana mapanga na rungu,nyuma walikuwepo watatu,wakaanza kunishambulia kwa kunikata kata kwa panga,na kunipiga kwa rungu,wakachukua fedha za mauzo,funguo na simu “alisema kwa kugugumia.
Majeruhi huyo alisema wakati wanamshambulia lilitokea gari aina ya Hiace lililokuwa linatokea Bunda ,wakamuacha na kwenda kuwashambulia waliokuwa ndani ya gari,akafanikiwa kukimbia huku akipiga yowe na kusaidiwa na mtu mmoja ,aliyemfikisha hospitali kwa matibabu.
Hata hivyo hakuweza kuwatambua watu hao kwa kuwa kulikuwa ni giza na walikuwa wameficha nyuso zao,Kamanda wa polisi Mkoa wa Mara hakuweza kutaja namba za gari na pikipiki,na alikiri kuwa hakuna mtu anashikiliwa kutokana na tukio hilo,na uchunguzi unaendelea.
Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo Emiliana Donald alisema majeruhi huyo anaendelea na matibabu,ingawa amejeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili,na kuwa majeruhi mwingine Samsoni Jeremia(24)mkazi wa Bunda ameruhusiwa kutoka baada ya kupata matibabu.
Matukio ya watu kutega magogo na kuteka magari ya abiria yanayotoka Bunda jioni yameanza kujitokeza tena,ambapo mwaka 2011/12,uharifu huo ulishamiri .
Mwisho.

WANANCHI WANAOTUHUMIWA KUSABABISHA MAUAJI WASUSA MAZISHI,



Wauguzi ,waganga na madaktari wa hospitali Teule ya Nyerere wilaya ya Serengeti walijitahidi sana kuokoa maisha ya Nyantito Robert mkazi wa kijiji cha Bwitengi,ambaye alichomwa mshale kifuani,juhudi zao hazikuzaa matunda,aliaga dunia.
Serengeti Media Centre(SMC)
Agosti 28,2015
Serengeti:Wakazi wa Kijiji cha Bwitengi wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara wanaodaiwa kuvamia mji wa Robert Ntantato na kusababisha kifo,kujeruhi,kubomoa mji na kupora vitu,wamesusa shughuli za  mazishi ya mwanakijiji mwenzao.
Uamzi huo unadaiwa ni mwendelezo wa msimamo  wa vijiji vitano vya Bwitengi,Morotonga,Rwamchanga,Miseke na Parknyigoti waliouweka agosti 26 mwaka huu kupitia mkutano wa Jamii(Ritongo),kuhamisha familia ya Robert Nyantato,aliyewashitaki baada ya kumnyang’anya ng’ombe tano kufuatia kijana wake kukamatwa kwa tuhuma za wizi wa ng’ombe mmoja.
Paulo Boche mkazi wa kijiji cha Burunga alisema ,mazingira hayo yaliwalazimu majilani  kusaidia shughuli za mazishi baada ya wakazi wa kijiji hicho kususia kwa madai kuwa ametengwa na jamii hiyo.
“Sisi kijiji jilani cha Burunga na ndugu zake ndiyo tumeshiriki shughuli za mazishi ya Nyantato Robert ambaye anadaiwa kuchomwa mshale agosti 26 nyumbani  kwao mwaka huu na kufia hospitali,kitendo hiki kwa kweli kimetusikitisha sana”alisema.
Alisema hakuna matanga yatakayofanyika,”kwa mila na desturi mtu akiuawa katika mazingira kama haya hakuna matanga….na huzikwa nje ya mji kwa kuwa huchukuliwa ni mkosi katika familia”alisema.
Rpc,
Kamanda wa polisi Mkoa wa Mara Philip Karangi akiongea na  Serengeti Media Centre(SMC) kwa njia ya simu ,alisema watu tisa wameishakamatwa kuhusiana na tukio hilo ambao ni wakazi wa kijiji hicho.
“Tunaendelea na msako na wote wanaotuhumiwa watakamatwa ,wananchi watambue kuwa kujichukulia sheria mkononi ni kosa kubwa….tunahimiza utawala wa sheria,hatutamuacha hata mmoja anayevunja sheria,”alisema.

habari kutoka vijiji hivyo zinadaiwa kuwa watu wengi wamekimbilia porini wakikimbia kukamatwa kutokana na tuhuma za kuua,kujeruhi,kubomoa nyumba na kupora mali za Robert Nyantato.
 
Wanaharakati,
Mwenyekiti Mtendaji wa shirika la Wasaidizi wa Kisheria na Haki za Binadamu Samwel Mewama alisema,serikali kuruhusu vikao visivyokuwa vya kisheria kutoa uamzi unaokinzana na sheria za nchi ndiyo matokeo yake.
“Jadi iko juu ya serikali hapa,wanaweza kukaa na kuamua kumhamisha mtu,kupora mali zake,kuua,kuchoma mji ,lakini serikali imekuwa kimya sana na matokeo yake yanasababisha taswira mbaya ya wilaya na jamii ya Waikoma,”alisema.
Ilivyotokea.
Agosti 11 mwaka huu eneo la mnada wa Mugumu  Sanja Robet(27)ambaye ni kijana wa Robert Nyantato alikamatwa na ng’ombe mmoja anayedaiwa kuwa wa wizi,na kufikishwa polisi.
Pamoja na kufikishwa polisi kwa hatua za kisheria ,wananchi walivamia makazi ya Nyantato ambaye ni baba yake na kuchukua ng’ombe tano kwa kosa alilotenda kijana wake ambaye ana mji wake.
Hata hivyo alifikisha malalamiko polisi na ofisi ya Mkuu wa wilaya ,wananchi wakaamriwa warudishe ng’ombe hizo ,na agosti 26 mwaka huu waliahidi kurudisha.
Katika kikao cha wananchi hao kwa mwanvuli wa jadi(ritongo)agenda ya kurudisha ng’ombe ilikataliwa na kuamua kumtenga,kumhamisha hapo kijijini,katika utekelezaji huo walimchoma mshale kifuani Nyantato Robert na kusababisha kifo.
Pia walimjeruhi Robert Nyantato ,kubomoa nyumba na kupora vitu mbalimbali ikiwemo mifugo.
Matukio Mengine kwa jamii hiyo,
Mwanzoni mwa mwaka huu kupitia vikao vya ritongo watu watano katika kata ya Ikoma waliuawa ,wengine makazi yao kuteketezwa,kuhamishwa kwa kutuhumiwa kujihusisha na matendo ya uchawi.
Mwisho.

Wednesday, August 26, 2015

WANANCHI SERENGETI WADAIWA KUUA,KUJERUHI,KUBOMOA NYUMBA NA KUPORA VITU

Familia ya Roberi Nyantato mkazi wa kitongoji cha Mtakuja kijiji cha Bwitengi wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara wakisomba vitu kutoka maeneo tofauti,baada ya wakazi wa vijiji vya Morotonga,Bwitengi,Rwamchanga,Miseke na Park nyigoti kuvamia mji wake,na kumchoma mshale kijana wake Nyantato Robert na kusababisha kifo,kujeruhi mzee,kubomoa mji na kupora vitu,baada ya kuagizwa wamlipe ng'ombe wake watano waliochukua wakituhumu kijana wake kuiba ng'ombe mmoja,hata hivyo mtuhumiwa ameishafikishwa mahakamani kwa kosa la kudaiwa kuiba ng'ombe.
Utafutaji wa vifaa unaendelea kufuatia maamzi yasiyozingatia haki za binadamu yaliyofanywa na kundi la wananchi kwa kivuli cha Ritongo.
Nyumba hiyo ilibomolewa madirisha na milango na kuanza kutoa vitu kwa madai ya kumtenga na kumhamisha kwa kuwa aliwashitaki kwa kupora ng'ombe tano na kuuza kwa tuhuma za kijana wake ambaye anajitegemea .
Baamda lililokuwa na nguruwe na mifugo mingine limebomolewa na wananchi hao.

Hapo wanaendelea kukusanya vitu na mifugo ,hata hivyo wanadai baadhi ya vitu na mifugo vimepotea.

Baadhi ya ndugu wakisaidia kusomba vitu
Polisi walifika kushuhudia unyama huo unaofanywa kwa mwanvuli wa Ritongo
Hali ilikuwa hiv.o
Robert akisaidia na mjukuu baada ya kupigwa na kuumizwa wakati anasaidia kijana wake ,hata hivyo aliaga dunia kutokana na shambulio la mshale ulioharibu mishipa ya moyo.

Watoto na wajukuu wakiwa hawajui nini la kufanya
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Bwitengi,Bwigeki alishuhudia unyama huo.
Baadhi ya vifaa vilivyopatikana.
Majeruhi anapelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu
Ndugu wakiwa hospitali Teule ya Nyerere wakisubiri majibu ya madaktari kuhusiana na ndugu yao aliyechomwa mshale,hata hivyo aliaga dunia
Robert akiwa hospitali akisburi mkupata huduma
Picha ya Xray ikionyesha mshale ulivyokita sehemu ya moyo.