Fahari ya Serengeti

Thursday, July 6, 2017

WAKAZI WA MACHOCHWE SERENGETI WATAKA SHERIA YA WANYAMAPORI IFANYIWE MAREKEBISHO

 Diwani wa Kata ya Machochwe wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara Chacha Michael akipitia hoja zilizowasilishwa na wananchi wa kata yake wakati wa Mkutano wa hadhara,moja ya mambo yaliyojadiliwa kwa nguvu na watu wengi ni kukithiri kwa tatizo la tembo kutoka ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Wameomba .Kanuni za ulipaji wa fidia na kifuta machozi kwa wananchi wanaopata madhara yanayotokana na wanyama kama tembo ziangaliwe upya kwa kuwa zinachangia ongezeko la umaskini kwa jamii.

Kupitia sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya Mwaka 2009 na kanuni za ulipaji fidia za mwaka 2011 ,ekari moja ya mazao yaliyoharibiwa na tembo hulipwa kati ya sh 25,000 hadi 100,000 kutegemea na umbali.

Daniel Makuri Mkazi wa Kijiji cha Machochwe wilayani Serengeti katika mkutano huo ameshauri serikali na wabunge ,badala ya kurekebisha sheria za Madini ,waangalie pia udhaifu wa sheria hiyo ya  wanyamapori kwa kuwa inachangia ongezeko la maskini hasa waishio pembezoni mwa maeneo yaliyohifadhiwa.

“Ng’ombe akikanyaga hifadhini mfugaji hulazimika kulipa sh 50,000 kwa ng’ombe mmoja,lakini tembo akila ekari moja moja ya mazao mtu analipwa sh 25,000,tena inachukua zaidi ya miaka mitatu,wakati  mifugo unalipa papo hapo,sheria hii inatakiwa kufanyiwa mabadiliko kama tunataka kupunguza umaskini,”alisema.

Suzana Chacha mkazi wa kijiji cha Manyata kwa hasira alisema,”tembo akiuawa mtu anatakiwa kutoa kulipa sh 25 mil,lakini akiua mtu serikali inamlipa mtu sh 1 milioni,harafu viongozi wanasisitiza tupende uhifadhi,katika mazingira ya kutathimini wanyama kuliko watu,kuna uhifadhi hapo,?”alisema
 Baadhi ya wazee wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa kata ya Machochwe ulioongozwa na Diwani wa kata hiyo.
 Wanafuatilia mjadala



Kila kona katika kata hiyo na kata za jilani zilizoko kando ya maeneo yaliyohifadhiwa wanalia na tatizo la tembo.

1 comment:

  1. Pamoja na hayo yote kuna lililofanyiwa kazi au bado wanakijiji hao bado wananyanyasika

    ReplyDelete