Fahari ya Serengeti

Thursday, July 6, 2017

GRUMETI GAME RESERVES WADAI WAKO TAYARI KULIPA IKONA WMA BAADA YA MARIDHIANO

Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Grumeti Game Reserves Ami Seki amekiri kampuni yao inadaiwa na Ikona Wma zaidi ya sh 1.2 bilioni na kuwa wapo tayari kulipa baada ya kukamilisha maridhiano na kusainiana makubaliano hayo.

Ufafanuzi huo ameutoa baada ya siku tano toka askari na viongozi wa Ikona Wma kuziba njia za kwenda kwenye hoteli ya Farufaru na maeneo mengine yaliyoko ndani ya eneo la Ikona Wma ambayo yanatumiwa na Kampuni hiyo kwa mkataba wa Malipo,hata hivyo kwa zaidi ya miaka mitatu kampuni hiyo haijalipa deni hilo hali ambayo inadaiwa kuathiri utendaji wa jumuiya hiyo.

Seki amesema kuwa katika mpango Mkakati wa Ikona imeanishwa taratibu za uwekezaji ,hata hivyo wanadai zimekiukwa ikiwa ni pamoja na kuweka kambi nyingi nje ya mpango na kuathiri wawekezaji wengine ikiwemo kampuni hiyo.

"Tumeishalalamika sana kwao,halmashauri na ofisi ya Dc bila mafanikio,tukaamua kusitisha malipo yao ili tukae maana wanataka haki bila kutimiza wajibu ,tuko tayari kuwalipa mara baada ya kusainiana makubaliano ya utendaji kazi,"anasema.

Akizungumzia masharti hayo Katibu wa Ikona Wma Yusuph Manyanda anasema kuwa Grumeti wanatakiwa kutimiza matakwa ya mkataba uliowafanya wakapewa eneo,si kuleta masharti ambayo hayana msingi ,kwa kuwa deni hilo ni haki ya Ikona kulipwa kwa kuwa anafanya biashara kwenye eneo la jamii.

"Haiwezekani mpangaji ndiye anaweka masharti dhidi ya mwenye nyumba na kumtaka ayasaini,maana Grumeti hawezi kuandaa masharti ya kufanya kazi katika eneo ambalo ameomba na kupewa kwa taratibu za jumuiya na taifa,kama kuna mambo ambayo anaona yamekiukwa afuate mamlaka zinazohusika,si kutalia fedha wakati akiendelea kufanya biashara,"anasema.
Mkuu wa wilaya ya Serengeti Nurdin Babu amesema ameishaita pande zote ofisini mwake ili waweze kumaliza mgogoro huo ambao kimsingi unahitaji maridhiano,"hatua ya kufunga njia wageni wasiiingie inaathiri sekta ya utalii,ni kweli Grumeti anadaiwa anatakiwa kulipa ,kuna mambo tukikutana tutayamaliza,"amesema.

0 comments:

Post a Comment