ANASWA KWA BIASHARA YA KUSAFIRISHA
WATU,
Serengeti Media Centre
Mkazi mmoja
wa kijiji cha Masinki kata ya Ring’wani wilayani Serengeti Mkoa wa Mara
anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kusafirisha watoto kutoka wilaya
ya Ngara Mkoa wa Kagera na kuwauza katika mikoa ya Mwanza na Mara.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Mara Ramadhani Ng’azi amelithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa
huyo (Julitha Lucas 40)ambaye
alikamatwa septemba 3 mwaka huu baada ya polisi kupata taarifa kutoka kwa
wasamaria wema,huku akidai hilo ni tukio la kwanza kutokea mkoani hapo.
Hata hivyo
inadaiwa wengine watatu hawajapatikana na haijulikani walikopelekwa ,huku
kukiwa na taarifa kuwa wamekimbia baada ya kuambiwa kuwa wanakamatwa kuwa si
raia na wanatakiwa kupelekwa kwenye makambi ya wakimbizi kwa madai kuwa si raia
wa Tanzania.
Alisema
mtuhumiwa alikutwa na wasichana sita ambao alikuwa amewaoza kwa watu mbalimbali
na vijana wawili ambao walikuwa wameuzwa kwa watu wawachungie mifugo na
miongoni mwao walibainika hawajui Kiswahili na wanadaiwa kuwa huenda ni raia wa
Burundi.
“Wasichana
hao wana umri kati ya miaka 15 hadi 18 na inadaiwa anawachukua kwao kwa madai
kuwa wanakuja kufanya kazi za ndani,lakini wakifika huwaoza kwa gharama kuanzia
sh 150,000 hadi 300,000 kwa kutegemea alivyo,na inasemekana wengine wako Mwanza
,Bunda na Serengeti,hapa tumemkamata na watoto 5 wa kike na wa kiume
wawili,tunaendelea na uchunguzi ushahidi ukikamilika tutamfikisha mahakamani
kwa makosa ya kusafirisha watoto,”alisema.
Wakiongea na
waandishi wa habari watoto hao walisema mama huyo ambaye naye ni mzaliwa wa
kijijini kwao humtumia wifi yake aliyeko kijijini hapo kumtafutia watoto kwa
madai ya kufanya kazi ,lakini walipofika wakaishia kuozwa na wawili wamebainika
kuwa na ujauzito tayari.
“Baada ya
kufika siku ya kwanza tukaenda shambani ,kutokana nikakuta wamenunua vitenge na
kuambiwa ninaolewa na kukabidhiwa mme ambaye hata sikuwahi kuzungumza
naye,nikaenda nimekaa kwake kwa wiki moja akawa ananipiga sana na kunitishia
kunikamata…niliporudi kwa mama huyo akasema mimi ni mkimbizi ninatakiwa kutulia
na hata tukimpeleka polisi hatutamshinda si wazawa,”alisema mmoja wao huku
akitokwa machozi.
Naye
mtuhumiwa huyo alipoulizwa alikiri kuwa watoto hao aliwaleta yeye kwa ajili ya
kuwatafutia kazi na baada ya kufika wakapata wanaume na kuwa fedha za mahari
alipanga kuwatumia wazazi wake,na kuwa zaidi ya watoto 17 ameishawatoa kijijini
na kuwauza maeneo mbalimbali.
(Lucas Nyanswi)ambaye aliozwa msichana aliyekuwa na
mtoto mdogo kwa sh 100,000 alisema alitoa malipo ya awali kwa mama huyo
akamfatia mwanamke,”kitanda hakizai haramu nilipewa na mtoto kwa mahari hiyo
baada ya kuuza pamba,sikujua kama ni Mrundi lakini yeye alisema anawatoa
Ngara,”alisema.
Mwenyekiti
wa kitongoji cha Gwinyanki Gitiri Ikwabe alisema agosti 2 mwaka huu alifuatilia
nyumbani kwa mama huyo na kukuta watoto 6 ambao alidai wamefika kumsalimia kwa
kuwa alikuwa anaumwa,hata hivyo baada ya mwezi mmoja alifuatilia na kuambiwa
wangeondoka septemba 2 mwaka huu.
Mratibu wa
Kituo cha Nyumba Salama kinachohudumia watoto wanaofanyiwa ukatili Rhobi
Samweli alisema walipewa taarifa na wasamaria wema kutoka kijijini hapo
kuhusiana na mateso waliyokuwa wanafanyiwa watoto hao na kulazimika kutoa
taarifa dawati la polisi la jinsia na baada ya kufuatilia ndipo wakabaini
mtandao huo.
Idara ya
uhamiaji wilayani hapa wanaendelea na uchunguzi ili kubaini uraia wa wasichana
hao baada ya kuwepo wasiofahamu lugha ya Kiswahili na wanaongea lugha ambayo
wenzao walidai kuwa ni watanzania.
Akutwa na wanyama wa ajabu.
Katika hali
isiyokuwa ya kawaida mtuhumiwa huyo alikutwa amefunga wanyama wengi wa ajabu ambao wanakijiji walishindwa
kuwatambua,ambapo mwenyekiti wa kitongoji hicho Gitiri Ikwabe alisema pamoja na
kufika nyumbani hapo mara kwa mara lakini hakujua kama anafuga wanyama hao.
Mwisho.
Picha inasomwaje? Mtuhumiwa huyo yupo upande gani mwa picha hiyo kushoto au kulia.
ReplyDelete