ZAIDI YA SH 308 MIL.ZANUFAISHA
VIKUNDI VYA WATOTO WA MAZINGIRA HATARISHI,
Serengeti Media Centre.
Zaidi ya sh 308 milioni zimekopeshwa kwa vikundi 96 vya
Watoto waishio katika Mazingira Hatarishi kupitia Mradi wa Pamoja Tuwalee wilayani
Serengeti Mkoa wa Mara kwa kipindi cha mwaka 2011hadi 2016.
Mradi wa Pamoja Tuwalee ambao umefikia ukomo ulikuwa
unaendeshwa na Shirika la Pact Tanzania kwa kushirikiana na asasi ya BAK-AIDS
kwa ufadhili wa USAID/PEPFAR katika kata 17 kati ya 30 za wilayani hapa,na
kuwezesha akina mama wengi kujihusisha na shughuli za bustani za mboga mboga
ambazo zimewawezesha kuweka akiba.
Mratibu wa Mradi wa BAK-AID wilaya ya Serengeti Christopher
Genya kwenye kikao cha wadau wa maendeleo wilaya wakati wa kukabidhi shughuli
za mradi huo kwa halmashauri
alisema,vikundi hivyo vina akiba y ash 331,162,260,na wanaendesha biashara
mbalimbali 1473 katika maeneo yao.
“Kupitia mradi huu watoto 4517 kati ya 8,046 wanalelewa na
walezi walio katika vikundi,na kaya 1,839 zimenufaika na mradi huo na wameweza
kuboresha makazi yao,wengine wamenunua mifugo,na waliokuwa wanakula mlo mmoja
sasa wanakula milo mitatu,na mafanikio makubwa ni kwamba wanajisimamia wenyewe,”alisema.
Hata hivyo alisema katika utekelezaji wa mradi huo
walikabiliana na changamoto za baadhi ya kamati za watoto wanaoishi katika
mazingira hatarishi kutokuwasaidia watoto,ikiwemo kutokushirikishwa katika
vikao vya serikali za vijiji na kata.
Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya ambaye
pia ni afisa maendeleo ya jamii Sunday Wambura aliwataka wadau wa maendeleo
kuhakikisha katika shughuli zao wanaweka mipango ya kuwasaidia watoto wa
mazingira hatarishi,kwa kuwa hilo ni jukumu la kila mmoja.
Mapema afisa mradi huo Eza Yusuph alisema lengo kuu lilikuwa
kuimarisha mifumo iliyopo ya jamii na familia zao,kuongeza rasilimali za ndani na
nje katika kufikia mahitaji ya watoto na
mfumo wa ustawi wa familia baada ya kukosekana kwa msaada toka nje.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment