Serengeti Media
Centre.
Halmashauri ya
wilayani hapa Mkoa wa Mara imejipanga kuhakikisha fursa zinazowazunguka
hasa za utalii na uhifadhi zinachangia kuchochea kukua kwa uchumi wa jamii na
wilaya hiyo.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Juma Porini akizindua awamu
ya pili ya utoaji wa mikopo kwa wanawake na vijana kupitia asilimia tano ya
makusanyo ya ndani jana ,alisema lengo lao ni kuona fursa hizo zinawanufaisha
wajasiriamali wakubwa kwa wadogo wakiwemo wakulima wanaozalisha mazao yao na
kukosa soko badala yake wanaambulia madhara yanayosababishwa na uhifadhi na
utalii.
Alisema jumla ya sh 128 milioni zimetolewa kwa vikundi 55 vya wanawake vikiwa 33 na vijana 22 toka machi mwaka huu ikiwa ni bajeti ya mwaka wa fedha 2015/16,lakini
kumekuwa na tatizo la soko hasa kwenye mahoteli na kambi za kitalii zilizomo
ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti,ili kuhakikisha wanafungua mahusiano
mazuri na jamii inayowazunguka alisema wamepanga kutembelea fursa hizo ili
wajadiliane changamoto zilizopo na namna ya utatuzi.
“Wakati tunahangaika kufungua milango ya fursa
zinazotuzunguka ,ni vema nanyi kujitahidi kuzalisha bidhaa zenye ubora ili
kuendana na soko,na pia mikopo hii ingawa ni kidogo maana tunatoa sh 2 milioni kwa kikundi ziweze
kusaidia kuleta tija kiuchumi kwa kila anayekopa,”alisema.
Alisema awali vikundi vingi vilivyokuwa vikinufaika na
mikopo vilikuwa vya mjini,lakini kwa awamu ya uongozi wao waliazimia maeneo
yote wanufaike na katika awamu ya pili ya mikopo kwa wanawake mjini wamepata
vikundi viwili na vijijini 10 .
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Seif Hamsini alisema
tatizo la wananchi kutonufaika na fursa za utalii zinazowazunguka ni la kitaifa
na kuwa wanajitahidi kuondoa mazingira hayo,huku akiwasihi wanufaika na mikopo
kama wanataka kushika soko la mahoteli ya kitalii waepuke kuzalisha mazao yao
kwa kutumia kemikali za viwandani.
“Lazima kufanyike na mabadiliko ya uzalishaji ,wenzetu wa
Uganda kwa nchi za Afrika Mashariki wamefanikiwa kushika soko hilo kwa kuwa
wanazalisha mazao yao bila kutumia kemikali za viwandani ,nanyi pia tumieni
njia za asili ili kulinda ubora wa matunda na mboga mboga mnazozalisha ili
kupanua soko,”alisema.
Hata hivyo alikiri kuwa kiwango kinachotolewa ni kidogo cha
sh 2 milioni ambazo ziko chini ya dola 1000 na kuwa watajitahidi kuona namna ya
kuboresha mikopo,hata hivyo serikali kuu kutokutoa ruzuku ya maendeleo kwa
bajeti ya mwaka 2015 ilifaya halmashauri itumie fedha za ndani kutekeleza
miradi na kukopesha makundi hayo.
Afisa vijana wilaya Isack Mwankusye alisema watafanya
ufuatiliaji kwa wanufaika wote kwa kuwa baadhi wamekuwa wakipata mikopo
wanaelekeza kwenye shughuli ambazo hawakuombea.
Naye afisa maendeleo ya Jamii Hidaya Mkaruka aliwataka
wanawake kuhakikisha wanarejesha kwa wakati kwa kuwa wasipofanya hivyo
wanaiingiza halmashauri kwenye gharama za kuwafuatilia na pia kukwamisha
wengine kukopa.
Mmoja wa wanufaika Mwita Chacha toka Kebanchabancha
alishauri halmashauri ifikie hatua ya kukopesha mtu mmoja mmoja hasa baada ya
kujiridhisha na kazi zake kwa kuwa kwenye vikundi watu wengi hawana mtizamo wa
aina moja na ndiyo maana vinashindwa kupiga hatua za kimaendeleo.
Mwisho.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Serengeti Juma Porini akitoa nasaha kwa wanachama wa vikundi vya vijana na wanawake ambao wamepata mkopo wa fedha kupitia asilimia tano ya makusanyo ya ndani bajeti ya mwaka 2015/16 jumla ya sh 128 mil zimetolewa toka machi hadi sasa
0 comments:
Post a Comment