Mchuano mkali kati ya timu ya Kilima Fc na Kibeyo Fc fainali ya ligi daraja la nne ngazi ya wilaya ya Serengeti.
Kipa wa Kilima Fc akijiandaa kunyaka mpira kwa mbwembwe ,katika mchezo ambao Kilima iliibuka na ushindi mnono wa magoli 5-2 na kutawazwa mabingwa wa wilaya.
Apigwa chenga na kubaki chini huku mchezaji wa Kibeyo Fc akikota gozi kutafuta goli kama inavyoonekana hapo.
KILIMA FC MABINGWA WA WILAYA.
Serengeti:Halmashauri ya wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara imepanga
kutenga bajeti kwa ajili ya michezo,itakayosaidia kuibua na kuendeleza vipaji
kwa michezo mbalimbali.
Mbunge wa Jimbo hilo Mwalimu Marwa Ryoba alisema hayo jana wakati
wa kuhitimisha mashindano ya ligi daraja la nne ngazi ya wilaya kwenye uwanja
wa Sokoine,ambapo alisema wanadhamiria kufufua michezo ili waweze kutoa timu
zenye ushindani katika maeneo mbalimbali.
“Mwakani naanzisha ligi yangu ambayo timu nitaziwezesha vifaa
mbalimbali,hiyo itatusaidia kupata vijana wenye vipaji vizuri ili tuweze
kutengeneza timu moja yenye ushindani,hata Mbeya City walianza taratibu chini
ya halmashauri,”alisema.
Kwa upande Mkuu wa wilaya hiyo Mafutah Ally akikabidhi zawadi iliyotolewa na Mbunge wa jimbo hilo kwa
washindi watatu wa ligi hiyo iliyoshirikisha jumla ya timu nane kwenye vituo
mbalimbali,alisema watazisaidia timu za Kilima Fc ya Natta mabingwa wa wilaya
walipata sh 45,000, Seronga Fc walioshika nafasi ya pili (35,000)na Polisi
Fc(20,000) yeye akitoa sh 50,000 kwa ajili ya waamzi wa mchezo huo.
“Mimi nategemea kuanzisha ligi kuanzia ngazi za kata kwa michezo
mbalimbali,kama alivyosema mbunge tuweze kuibua vipaji kwa michezo mbalimbali
ikiwemo ya wanawake,hayo yote ni kwa ajili ya kuwaweka vijana pamoja,kukuza
vipaji na kuwafungulia fursa zingine kupitia michezo,”alisema.
Katika mchezo wa mwisho ulichezwa uwanja wa sokoine timu ya Kilima
Fc ya Natta ilichukua ubingwa wa wilaya baada ya kuinyuka timu ya Kibeyo Fc kwa
mabao 5-2,na kufanikiwa kupata sh 45,000 na kuwakilisha wilaya ligi daraja la
tatu ngazi ya mkoa.
Kama walivyosema wahenga kutangulia si kufika ,Kibeyo kupitia kwa
washambuliaji wake Marwa Julius na Kibisa walipachika mabao katika dakika ya 17
na 25 kipindi cha kwanza na kuwafanya Kilima kupoteana.
Hata hivyo katika dakika ya 28 mshambuliaji wa Kilima Fc aliyeng’ara katika mchezo huo
kutokana na kucheza mpira safi Sixtus Sabilo alifunga bao la kufutia machozi,na
kufanya matokeo kuwa 2-1 kipindi cha kwanza.
Kipindi cha pili kila timu ilifanya mabadiliko ili kuimarisha kasi
ya ushambuliaji na ulinzi,hata hivyo mshambuliaji Sabilo dakika 18 kipindi cha
pili aliwanyanyua mashabiki baada ya kufunga goli zuri na kubadili sura ya
mchezo,na kuwafanya Kibeyo kupoteana.
Dakika ya 20 mshambuliaji Samson Lucas alifunga goli la tatu baada
ya kumzidi ujanja kipa wa Kibeyo,dakika ya 35 mshambuliaji Chisayama aliifungia
Kilima goli la nne kwa kumvika kanzu kipa wa Kibeyo Mgabo,na dakika ya 44
Sixtus Sabilo alifunga kitabu cha magoli na kuibuka mfunga bora katika mchezo
huo.
Katika mchezo wa awali timu ya Seronga iliyoibuka mshindi wa pili
iliifunga timu ya Polisi kwa magoli 2-1,magoli ya Seronga yakifungwa na Paineto
Yusuph na la Polisi likifungwa na Masaita Fulyas.
Makocha wa Kilima Fc Samwel Matete na Seronga Fc Erasto Joshua
walisema wanajiandaa kwa ajili ya kufanya vizuri kwenye ligi daraja la tatu
ngazi ya Mkoa na kuomba wadau mbalimbali kuzisaidia timu hizo kwa kuwa
zinawakilisha wilaya.
Mwenyekiti wa chama cha Mpira wilaya Vedastus Makaranga alisema
timu zilizoshiriki katika mashindano hayo ni pamoja na Itununu Fc,Mageta
Fc,Kilima Fc,Kibeyo Fc,Motukeri Fc,Polisi Fc,Seronga Fc na Imara Fc.
Mwisho.
Mbunge wa jimbo la Serengeti Mwalimu Marwa Ryoba akiwapongeza wachezaji wote kwa kushiriki ligi hiyo,na kuahidi kuanzisha ligi maalum ya kusaka vipaji atakayoifadhili mwenyewe,kulia ni mkuu wa wilaya Mafutah Ally
Dc Mafutah Ally akielezea umuhimu wa michezo kwa vijana na kuahidi kuanzisha michezo mbalimbali kwa makundi ya vijana wilayani humo na kabla ya sikukuu ya mpya mpya atashirikiana na wadau kuanzisha ligi maalum
Wachezaji wa timbu mbalimbali wakisikiliza hotuba za viongozi
Mkuu wa wilaya akikabidhi zawadi ya sh 20,000 nahodha wa timu ya polisi Fc baada ya kushika nafasi ya tatu,
Nahodha wa timu ya Seronga ambayo imeshika nafasi ya pili itashiriki ligi daraja la tatu ngazi ya mkoa
0 comments:
Post a Comment