Fahari ya Serengeti

Sunday, November 27, 2016

AFIA NDANI YA SHIMO LA DHAHABU



AFIA NDANI YA SHIMO LA DHAHABU,

Serengeti Media Centre.

Mchimbaji mmoja wa dhahabu katika kijiji cha Nyamokobiti kata ya Majimoto wilayani Serengeti Mkoa wa Mara amekutwa ndani ya shimo la dhahabu akiwa amekufa huku akiwa na jeraha kichwani.
Tukio hilo ambalo limeibua maswali mengi linadaiwa kutokea usiku wa kuamkia novemba 26 mwaka huu katika shimo linalomilikiwa na John Ugolo lililoko katika eneo la Bigeso Mantago mkazi wa kijijini hapo,limethibitishwa na Polisi na uongozi wa kijiji na kata ambao wamemtaja aliyekufa kuwa ni Maro Matiko(45)ambaye ni ndugu na mmiliki wa shimo hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara Ramadhani Ng’anzi akiongea na Serengeti Media Centre amemtaja aliyekufa kuwa ni Maro Matiko(45)na kudai kuwa hakuna mtu wanayemshikilia kwa kuwa hiyo taarifa wanaichukulia kuwa ya kawaida.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho Kebegi Nyamori ameiambia Serengeti Media Centre  kwa njia ya simu kutoka eneo la tukio amesema,maiti iligunduliwa novemba 26 majira ya saa 2 asubuhi baada ya kukuta tochi aliyokuwa anaitumia kwa ulinzi nje ya shimo nay eye akawa haonekani.
“Siku ya tukio walikuwa wamepanga kwenda kijijini kwao Ring’wani na ndugu yake ambaye ni mmiliki wa shimo baada ya kuuza dhahabu ,Ugolo alilala kijijini na Matiko(marehemu)alilala nje ya shimo kama mlinzi ili watu wasiingie kuchimba,akawa amelewa viroba,inaonekana aliteleza akiwa amesinzia na kutumbukia na kupiga kichwa kwenye miamba,”alisema.
Alisema baadhi ya wachimbaji walishuka shimoni wakidhani anaendelea na kazi ya uchimbaji na kumkuta amekufa,”hata hivyohawakusubiri polisi wala uongozi wa kijiji walimtoa nje ndipo wakatoa taarifa kwangu nami nikajulisha polisi kwa ajili ya uchunguzi wa tukio zima maana hakuna mwenye maelezo sahihi jinsi ilivyotokea”alidai.
Kwa upande wake mwenye eneo hilo Bigeso Mantago alisema alipata taarifa za tukio kupitia kwa John Ugolo,hata hivyo alisema nje ya shimo alipokuwa amelala kama mlinzi walikuta  tochi na pakti za viroba hali ambayo inadhihirisha kuwa alikuwa amelewa.
Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho walisema tukiohilo limetokea ikiwa ni siku chache baada ya ndugu hao kupata dhahabu ambayo waliuza na kupanga kwenda kijijini kwao Ring’wani huku wakiwa wamesitisha shughuli mpaka warudi,hata hivyo hakuna aliyekuwa na uhakika wa kiasi walichopata.
“Hili ni tukio la kwanza kutokea kwenye eneo langu limetushangaza sana ,lakini katika maeneo ya uchimbaji hapa ni la pili kufuatia tukio la kwanza kwenye shimo la Mndore Marungu mchimbaji mmoja alikufa baada ya kuzidiwa na moshi wakati wakitoa maji kwa jenereta,”alisema mmoja wa wakazi wa kijiji hicho.
Mwisho.


0 comments:

Post a Comment