Fahari ya Serengeti

Saturday, January 3, 2015

MKAKATI WA KUMTETEA DED WAWAGAWA MADIWANI

.

 
Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara
wamegawanyika huku kundi kubwa likipinga mpango wa kumtetea aliyekuwa Mkurugenzi wa halmashauri aliyevuliwa madaraka kwa kushindwa kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa.

Uteuzi wa Goody Pamba ulitenguliwa Desemba 17  mwaka huu na  Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu(Tamisemi)Hawa Ghasia  baada  ya  Rais Jakaya Kikwete kuridhia watendaji wote waliohusika kuvuruga uchaguzi

wachukuliwe hatua.

Baadhi ya madiwani wakiongea na Serengeti media Centre wamesema  hawakubalini na mpango unaoendeshwa na Mwenyekiti wa halmashauri wa kumtetea Pamba kwa madai kuwa kufanya hivyo ni kupingana na uamzi wa Rais Kikwete kwa kuwa
kutofanyika kwa uchaguzi siku iliyopangwa kumechangia kuleta matokeo mabaya kwa CCM katika maeneo mengi.

“Mpango huo hatutakubaliana nao kwa kuwa hauna maslahi kwa wilaya bali kikundi cha watu wachache ambao wanahofu kuondolewa kwake mambo yao mengi yatajulikana….maana alikuwa na kikundi cha madiwani wachache na
watumishi aliowaona bora ,kukaa vikao kwa ajili ya jambo hili ni matumizi mabaya ya fedha za wananchi”anasema diwani mmoja jina tunalo.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo John Ng’oina anasema  kuwa watakaa wajadili kisha nao watoe kauli kuhusiana na uamzi huo ambao anadai haukumtendea haki Pamba kwa kuwa hakuhojiwa na mamlaka zake za
uteuzi ili ajitetee.

“Huyu mama ameonewa maana hajahojiwa sehemu yoyote…hakuna
aliyemlalamikia,baada ya kutokea dosari aliahirisha kwa mjibu wa
sheria na kupanga tarehe nyingine,sasa kutengua uteuzi wake katika
mazingira haya lazima nasi kama halmashauri tulijadili kisha nasi
tutoe sauti yetu”alisema.
Hata hivyo katika kikao cha kamati ya madiwani ya Mipango ,uchumi na
fedha kilichokutana desemba 23 mwaka huu hakikufikia uamzi baada ya
hoja hiyo kuleta mgongano,huku wengine wakitaka waliokuwa wasimamizi
wasaidizi wa uchaguzi nao wachukuliwe hatua.
Katika kikao cha desemba 30 bado hawakupata muafaka na kukubaliana uchunguzi ufanyike utakaofanywa na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ili kubaini watumishi wengine waliohusika kuvuruga uchaguzi huo,waweze kuchukuliwa hatua.

“Kuna watu waliokuwa wananufaika kwa tenda na kupitishiwa fedha kwa
ajili ya mambo yao kwa kivuli cha safari za halmashauri ndiyo wako
mstari wa mbele kutaka wote tuungane nao….hili jambo limesababisha
madhara makubwa kidemokrasia,na kwasasa wananchi wanafuatilia kwa
karibu mambo yanayoendelea na fedha zao zinavyotumiwa,”anasema diwanina kuongeza.

“Kuna mkakati wa kuchota fedha baadhi ya watu waende Dar es salaam ama Dodoma kumtetea ,hizo ni fedha za wananchi ambazo zingesaidia kwenye ujenzi wa vyumba vya maabara ama kulipia karo watoto

watakaokosa karo…. Matendo kama haya yataendelea kututesa kwa
jamii,”anasema.

Habari kutoka kwa chanzo kingine kilisema kuwa baada ya kusikia Rais
Kikwete alipokuwa  kwenye mapumziko ya sikukuu  katika hotel ya Four Session  ndani ya hifadhi ya Taifa yaSerengeti ,wanasiasa walitumwa  ili arudishiwe madaraka,hata hivyo hawakufanikiwa.
Mmoja wa watu ambaye anadaiwa kuwa na uhusiano wa karibu na mkurugenzi aliyevuliwa madaraka na pia mnufaika wa zabuni kwa kofia ya nafasi yake ndani ya Chama hakuwa tayari kulizungumzia suala hilo baada ya mkakati wake kukataliwa.

Hata hivyo baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa vinavyounda Ukawa
wilayani hapa walisema kuwa uamzi wa kumvua madaraka ulikuwa sahihi
kutokana na uzembe wa kufanya maandalizi ya uchaguzi,huku wakidai kuwa katika vikao vyao vyote aliwahakikishia kuwa maandalizi yamekamilika,wakati hali ilikuwa kinyume.
Wanasema kuwa hapakuwa na maandalizi ya kutosha kwa kuwa hata baada ya kuahirisha uchaguzi  bado vifaa vilipungua na kulazimisha watendaji kuwa wanatoa nakala  karatasi za kupigia kura kwenye maduka,huku matukio ya watu kukamatwa na  karatasi za kupigia kura yakijitokeza.
Mwisho.

0 comments:

Post a Comment