Fahari ya Serengeti

Thursday, January 8, 2015

Ahadi ya ujenzi barabara Serengeti yakwama




 Na Mussa Juma, Mwananchi

Posted  Alhamisi,Januari8  2015 
KWA UFUPI
NI ile yenye urefu wa kilomita 421 iliyopaswa kujengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya Sh648 bilioni.
Arusha, Ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Mto wa Mbu, wilayani Monduli, Mkoa wa Arusha hadi Nata, wilayani Serengeti, Mkoa wa Mara umekwama baada ya Serikali kushindwa kutoa fedha kama ilivyoahidi awali.
Serikali iliahidi kujenga barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 421 kwa gharama ya Sh648 bilioni, huku eneo linalokatiza ndani ya hifadhi lenye kilomita 53, likitarajiwa kujengwa kwa changarawe.
Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Arusha, Deusdedit Kakoko alisema pamoja na kwamba Serikali haijatoa fedha hadi sasa, ahadi ya kujenga barabara hiyo iko palepale.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Jowika Kasunga wakati akizungumza kwenye Kikao cha Bodi ya Barabara Arusha kilichofanyika juzi.
“Ni kweli ujenzi wa barabara haujaanza, lakini ahadi ya kuijenga iko palepale, kinachosubiriwa ni fedha kutoka Serikali Kuu,” alisema Kasunga.
Awali, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ngorongoro, Elias Ngolisa alihoji lini barabara hiyo itaanza kujengwa kutokana na umuhimu wake.
Ngolisa aliitaka Serikali kueleza kwa nini haijatoa kiasi cha fedha za awali za ujenzi huo, kiasi cha Sh7 bilioni.
“Pamoja na fedha hizo kutotolewa hadi sasa, bado kiasi hicho ni kidogo, labda kitumike kukarabati na siyo kujenga,” alisema.
Ahadi ya ujenzi huo ilitolewa na Rais Jakaya Kikwete ili kuwapunguzia usumbufu wakazi wa Arusha na Mara kutokana na mikoa hiyo kutounganishwa kwa barabara ya lami.


0 comments:

Post a Comment