HUDUMA HOSPITALI ZASITISHWA KWA
KUKOSA MAJI.
Serengeti:Baadhi ya huduma katika hospitali Teule ya wilaya ya Nyerere
wilayani hapa Mkoa wa Mara zimesitishwa kutokana na ukosefu wa maji hali ambayo
kama haitatatuliwa mapema huenda akasababisha madhara makubwa kwa jamii.
Takribani
miezi mitatu hospitali hiyo inayotegemewa na wakazi zaidi ya 200,000 wa wilaya
hiyo na nje ya wilaya haina maji kutokana na kuharibika kwa pampu,hata hivyo
baada ya matengenezo hawajapata huduma
ya maji kwa kile kinachodaiwa kuwa wanatakiwa kurekebisha miundo mbinu yao ya bomba na tenki.
Wakiongea
kwa kukata tamaa baadhi ya wanaoguza wagonjwa walisema wanalazimika kununua
maji,kwenda na shuka zao kwa kuwa za hospitali ni chafu na hazifuliwi, na vyoo
vya wagonjwa vimetapakaa kinyesi kutokana
na kutokuwa na maji.
“Nimefika
hapa saa 3 asubuhi na mgonjwa wangu akiwa na hali mbaya,hadi saa 8 arasili
hakuna huduma ,wauguzi na waganga wanasema hawawezi kutoa huduma wakati hakuna
maji ,maabara na chumba cha upasuaji bila maji hawawezi kutoa huduma,”alisema
kwa masikitiko Marwa Nyakibari.
Grace Joseph
ambaye ana ndugu yake aliyelazwa chumba cha wazazi alisema,wanalazimika kununua
maji mjini ,hata hivyo kwa wale wasiokuwa na uwezo wa kununua wanakabiliwa na
hali mbaya zaidi.
Mganga Mkuu
wa hospitali hiyo Emiliana Donald alidai kuwa huduma zinatolewa kama kawaida ,hata
hivyo alikiri kutokuwa na maji kwa muda mrefu,huku akigoma kutoa ufafanuzi wa
tatizo hilo ambalo linaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko.
Meneja wa
Mamlaka ya Maji Mugumu(Muguwasa)Mhandisi Dickson Gideon alisema kwa mjibu wa
sheria ya Maji namba 12 ya mwaka 2009 wao wanawajibika kufikisha maji kwa mteja
kupandisha kwenye tenki ni wajibu wake,hivyo kuitaka mamlaka iwapandishie maji
hadi juu kwa gharama zile zile ni hasara na watashindwa uendeshaji.
“Pamoja na
kuwa na hitilafu kwa sasa kwenye Control Panel baada ya marekebisho na
kusababisha huduma kusimama ili isiungue tumeagiza vifaa na wakati wowote
tutafunga,lakini hospitali lazima wabadilishe miundo mbinu yao ili maji yaende
juu na hizo ni gharama zao si mamlaka,”alisisitiza.
Wakati
mganga mkuu wa hospitali akidai huduma zinaendelea kama kawaida ,baadhi ya
wauguzi na waganga waliokutwa wamekaa nje ya maeneo yao ya kazi walisema
,taarifa za uongozi wao hazina ukweli kwa kuwa hawatoi huduma katika mazingira
hayo ambayo yanaweza kuwasababishia magonjwa ya mlipuko.
“Shuka
hazifuliwi,hakuna maji maabara ,chumba cha wazazi ,upasuaji ,mawodini na vyoo
vimetapakaa vinyesi harafu kiongozi anasema huduma zinaendelea,kama zinaendelea
kwa nini wagonjwa wanalalamika kutopata huduma,?”walihoji baadhi ya wauguzi.
Boniphace
Magori mkazi wa kijiji cha Remung’orori alisema alimfikisha mgonjwa wake akiwa
na upungufu wa damu na kukuta hakuna huduma,na baada ya kuomba uongozi ndipo
akasaidiwa .
“Kuna hatari
ya kupata magonjwa ya mlipuko hapa maana hali ni chafu sana,tunatoka vijijini
kuja kupata huduma kumbe tunakuja kubeba matatizo mengine,wagonjwa hawaogi
,hakuna maji kwenye vyoo ,”alisema.
Magreth John
alisema wananunua dawa,kitanda wanalipia na maji pia ,ndani ya mawodi harufu ni
mbaya hapakaliki kwa kuwa hata maji ya kufanyia usafi wauguzi wanawanyang’anya
wagonjwa walionunua.
Hata hivyo
kwa muda wa siku tatu sasa mji huo hauna huduma ya maji ya bomba hali ambayo
inawalazimu wananchi kutafuta maji kwenye visima mbalimbali vya asili ambavyo
si safi na salama.
Mwisho.
Moja ya choo cha wagonjwa kikiwa kimetapakaa vinyesi kutokana na ukosefu wa maji hali ambayo ianweza kusababisha magonjwa ya mlipuko kama hatua za makusudi hazitachukuliwa kwa haraka.
Poleni sana wana serengeti. maana hii ni hatari kwa afya za wagonjwa na hata wauguzi wenyewe, serikali ilione hili na kuchukua hatua za haraka.
ReplyDelete