Na Serengeti Media Centre
Mkazi wa kitongoji cha
Mihuru kijiji cha Kitarungu kata ya Nyansurura wilayani Serengeti Mkoa
wa Mara amekufa baada ya kujinyonga kwa kamba ya katani ,chanzo kikitajwa kukosa ng’ombe wa kulipa mahari.
Polisi wilayani hapa,uongozi wa kitongoji na serikali ya
kijiji umethibitisha kutokea kwa tukio hilo kati ya septemba 7 na 8 majira ya
usiku,ambapo Chacha Bruna(25)mwenyeji wa kijiji cha Nyabisaga wilayani Tarime
,alijinyonga kwa kamba ya katani hadi kufa.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho Yohana Gimano akiongea na Serengeti Media
Centre kwa njia ya simu kutoka eneo la tukio ,alisema Bruna aliyekuwa amefikia
kwa baba yake mdogo Diabe Marwa ,alifikia uamzi huo baada ya kunyang’anywa
mwanamke kwa kushindwa kulipa mahari.
“ Yeye ni Mkazi wa Tarime lakini hapa kijijini kuna ukoo wao,alipofika hapa alimtorosha
binti mmoja(Rhobi Samweli)akakaa naye kwa muda wa siku nne,septemba 7 ndugu
zake walifuata huyo binti ili atoe mahari,kufuatilia akaambiwa atoe ng’ombe
9,yeye akasema anaye mmoja….wakamfukuza mpaka atoe mahari ndipo apewe mke,usiku
akaamua kujiua”alisema.
Alisema kuwa kabla ya kuchukua uamzi huo akiwa na kamba ya katani alimwambia mwanamke mmoja kwenye mji
aliokuwa anaishi,kuwa haoni faida ya kuishi na kuwa siku hiyo ndiyo mwisho
wake,hata hivyo hawakufualia kwa kuwa hawakutegemea kama angechukua uamzi huo.
“Asubuhi wamekuta ananing’inia kwenye mti pembeni ya
barabara akiwa ameishakufa…inaonekana alijinyonga usiku ule ule ,kwa kuwa
wanadai hata chakula cha usiku hawakula naye,walijua yuko katika matembezi ya
kawaida”alibainisha.
Naye Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Kitarungu ambaye ni
jilani yake alisema ,tukio hilo limebainika alfajiri wakati watu wanapita
,wakiwemo wanafunzi ,”suala la yeye kunyang’anywa mwanamke linajulikana ,na
alionekana mwenye mawazo sana baada ya kushindwa kuelewana na ndugu wa mchumba
wake,huenda ilimuathiri kisaikolojia na kukosa msaada wa ushauri”alisema.
Mmoja wa wahudumu wa baa iliyoko jilani na eneo la tukio
ambaye hakutaka jina lake litajwe,alisema kuwa uhusiano wa Bruno na huyo binti
ulikuwa wa muda mrefu ,”toka mwezi februari nilikuwa najua ni wachumba,na
walikuwa wanawasiliana sana kwa simu,na
ilijulikana baadae baada ya kumtorosha na ndugu kufuatilia,”alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara Philip Karangi hakuweza
kupatikana kuzungumzia tukio hilo,hata hivyo Polisi wilayani hapa wamesema uchunguzi wa tukio hilo unaoshirikisha mganga ili kubaini chanzo cha kifo hicho ukikamilika
ndugu wataruhusiwa kuendelea na mazishi,na hakuna mtu anayeshikiliwa kuhusiana
na tukio hilo.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment