Fahari ya Serengeti

Tuesday, June 23, 2015

Sheria za Kimila ‘zaifunika’ Serikali wilayani Serengeti




tangazo linalowazuia zaidi ya watu 200, wakazi wa wilaya hiyo kuingia katika nyumba ya mtu, kuongea na watu waliotengwa au kupata huduma za kijamii kijijini hapo.
Tangazo  lililosambazwa  katika Ofisi za Serikali za Kata na maeneo mengine wilayani Serengeti, Mkoa wa Mara, linaweza kutafsiriwa au kutoa picha kwamba utawala bora, haki za binadamu na utawala wa sheria hauna nafasi kwenye wilaya hiyo.
Hilo ni tangazo linalowazuia zaidi ya watu 200, wakazi wa wilaya hiyo kuingia katika nyumba ya mtu, kuongea na watu waliotengwa au kupata huduma za kijamii kijijini hapo.
Baadhi ya waathirika wakitoka ofisi ya Mtendaji kata ya Mbalibali kutafuta msaada wa serikali bila mafanikio,
Baadhi ya waathirika wa maamzi hayo wakiwa ofisi ya serikali ya kijiji cha Koreri wakisaka msaada wa serikali bila mafanikio.

Iko hivi, mtu yeyote anayeongea na watu hao au kuwapa huduma yoyote hutozwa faini ya ng’ombe watano au kulipa Sh 500,000 ambazo huangukia mikononi mwa wazee wa mila badala ya kufanya shughuli za maendeleo.
Pamoja na uamuzi huo kukiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 12 hadi 17, mamlaka za Serikali zimeshindwa kuchukua hatua stahiki dhidi ya wahusika na kuwafanya wakazi hao wa Kitongoji cha Kisiwani, Kijiji cha Koreri, Kata ya Mbalibali, kilichopo umbali wa kilometa 20 kutoka mjini Mugumu kuishi maisha ya dhiki kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.
Wazee hao wa mila wa ukoo wa Inchage, wanadaiwa kupoteza hadhi mbele ya jamii kwa kudaiwa kutumiwa na baadhi ya watu kwa maslahi yao, ikiwemo wana siasa ili kuwakomoa wengine wanaowaona tishio kisiasa.
 Chanzo
Mwita Kitagira (38), mmoja wa waathirika wa uamzi huo, anasema kuwa kutengwa kwao na  wazee wa mila kumetokana na mgogoro wa ardhi kati yao na mtu aliyemtaja kuwa ni  jirani yao (jina limehifadhiwa). Anasema kuwa hayo yametokea wakati wao wana kesi na mtu huyo waliyoifungua Baraza la Ardhi Kata ya Mbalibali wakimlalamikia kwa kuvamia eneo lao.
“Nilishangaa kuitwa na wazee wa mila, nilipofika waliniambia kuwa nilikaidi uamuzi wao wa kuamuru eneo hilo nimwachie tunayeshitakiana naye. …Niliwaambia kuwa suala hilo liko kwenye vyombo vya sheria, wakasema nimewadharau, nivue kiatu niwaachie. Nilikataa, ndipo wakaapa kuwa nitaona huku wakidai  kuwa nimewadharau,” Kitagira anasema kwa masikitiko.
Anasema kuwa Mei 10 lilipigwa baragumu na kupata taarifa kuwa wazee wa mila wamepanga kuteketeza mji wake naye akalazimika kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa Serikali ya kijiji na Ofisa Mtendaji kata, ambao walilazimika kutaka kujua lengo la kuitisha mkutano huo. Hata hivyo, walidai wana matangazo muhimu.
“Walichofanya ni kutangaza kuwa tangu siku hiyo, wameutenga ukoo wote wa Masero na hakuna mtu kufika au kuzungumza na sisi, wala kununua kitu katika maduka ya kijiji, wala kupata huduma za kijamii. Pia, atakayetuuzia au kutuhudumia naye atatengwa, au kulipa faini ya Sh 500,000. Hapa tulipo, huduma zote tunalazimika kuzifuata mjini,” anasema na kuongeza:
“Watoto wetu wanaosoma walikuwa wamezuiwa kusoma, lakini mwalimu mkuu akawakatalia wazee wa mila akiwaeleza kuwa kisheria watoto wana haki ya kusoma, kupata huduma za afya. Lakini kwetu bado ni vigumu hatujui kama tutaweza kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Kupiga Kura, maana hatutakiwi kuchangamana na watu wengine.”
Naye Samwel Masero (62), mstaafu wa Jeshi la Wananchi ambaye pia amekumbwa na adhabu hiyo anasema kuwa mgogoro huo ulianzia Baraza la Usuluhishi la Kijiji, akapewa haki lakini mwenzake akaamua kwenda kufungua shauri Baraza la Ardhi la Kata.
ni hapo.
 “Wakati shauri likiendelea, mlalamikaji akaenda kwa wazee wa mila wakafika eneo la mgogoro na kutoa uamuzi kuwa eneo hilo aachiwe mlalamikaji, wakati uamuzi wa kisheria haujatolewa. Hatukukubaliana, ndipo wakadai sisi tumewadharau na kutoa uamuzi wa kututenga,”anasema.
Masero anasema kuwa waliwasiliana na uongozi wa kijiji, kata na Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, ambao hawajatatua mgogoro huo, wameshikwa na kigugumizi huku wao wakiendelea kutaabika na wananchi wengine wanaozungumza nao wanatozwa faini na wengine kutengwa .
“Mkuu wa wilaya nimemwona mara tatu bila ufumbuzi; mara zote amesema anawaagiza ofisa mtendaji kata, ofisa mtendaji tarafa na sasa ni zaidi ya mwezi mmoja, hakuna ufumbuzi, nasi tunazidi kuathirika. Kesi ya msingi haisikilizwi kwa kuwa wazee wa baraza wanaogopa kuongea nasi, hata mashahidi wanaogopa kuongozana nasi. Hii ni hatari, wilaya inaongozwa kwa sheria za mila?”anahoji.
Viongozi wajichanganya
Viongozi wa Serikali ya Kijiji cha Koreri, Kata ya Mbalibali, Tarafa na Mkuu wa Wilaya hiyo kwa nyakati tofauti wamekuwa na kauli za kujichanganya kuhusu adhabu zinazotolewa na wazee wa mila.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Koreri, Kisiri Chacha anasema kuwa kwa uamuzi wa wazee wa mila, wao hawana hatua zaidi ya kuchukua kwa sababu wao wanaongoza kwa mjibu wa sheria na mila, hivyo waliotengwa wanatakiwa kuwatafuta wazee wa mila ili waelewane nao.
“Mimi natokana na jamii hii, sasa wazee wakishaamua, aliyeadhibiwa anatakiwa kuwafuata hao ili kuomba apunguziwe adhabu,”anasema.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Joel Simioni anakiri ofisi yake kuhusika katika hatua ya usuluhishi na kutoa haki kwa Masero, kutokana na kujiridhisha kwa ushahidi wa majirani na kutaka asiyeridhika kwenda kufungua shauri Baraza la Ardhi la Kata.
“Licha ya kufungua lalamiko katika Baraza la Ardhi la Kata, Masero akaenda kwa wazee wa mila ambao hawakutushirikisha katika uamzi wao na kutoa adhabu hata kwa wasiohusika na mgogoro. Kama ofisi, hatujachukua hatua za kuwaita wazee wa mila kuhusu suala hili, ingawa waliotengwa wameshafika kulalamika,”anasema.
Pia, Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Peter Hagare, anakiri uamuzi wa wazee wa mila umechukuliwa wakati kuna mashauri mawili kuhusu suala hilo mbele ya Baraza la Ardhi la Kata, moja likimhusu Yatancha Ntagira anayedai mazao yake yaliharibiwa, nyingine ya Mwita Marwa kuhusu eneo lao kuvamiwa .
“Baraza la Ardhi la Kata wameshindwa kusikiliza mashauri haya kwa kuwa wazee wa mila wameingilia na kutoa uamuzi unaowafanya waogope kutengwa….hata wao wakionekana wanaongea na watuhumiwa waliotengwa, watatengwa na jamii. Hata mashahidi hawawezi kujitokeza,”anasema.
Anakiri kupokea maagizo ya mkuu wa wilaya, kupitia kwa ofisa tarafa, kushughulikia uamuzi wa wazee wa mila, hata hivyo anasema kuwa uamuzi wa wazee hao umekiuka haki za msingi za waliotengwa.
“Naendelea kufuatilia kwa kuwa wazee wa mila waliotoa uamzi hawakai kata hii wanatoka maeneo tofauti,” anasema bila kubainisha lini atakutana nao.
Ofisa Tarafa ya Rogoro, Shaweshi Sipemba naye anakiri kuagizwa na Mkuu wa Wilaya kumaliza tatizo hilo na kueleza kwamba angekutana na waliotengwa, viongozi wa Baraza la Ardhi la Kata, wazee wa mila na aliyefikisha shauri kwao Juni 15 mwaka huu katika ofisi ya kata. Hata hivyo, hadi sasa hakuna kikao kilichofanyika.
Mkuu wa wilaya
Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Ally Maftah anakiri kupata taarifa akieleza kwamba ametuma wasaidizi wake kuchukua hatua za kisheria.
“Natarajia kwenda kukutana nao, maana, hivi karibuni, watu watano wameuawa, chanzo ni wazee wa mila. Lazima mambo haya yadhibitiwe na wapewe mipaka ya kazi zao. Huwezi kuwatenga watu kwa kosa la mtu mmoja, hili halikubaliki,”anasema Maftah.
Hata hivyo ni zaidi ya mwezi mmoja tangu alipopata taarifa hizo, kiongiozi huyo hajaenda Kata ya Mbalibali wala kuchukua hatua yoyote.
Wajumbe wakimbia mahojiano.
Katika hali isiyo ya kawaida, wazee wa Baraza la Ardhi Kata ya Mbalibali walikimbia wasihojiwe, baada ya Mwandishi wa habari hizi kufika ofisi ya kata hiyo na kuwakuta wakiwa na na ofisa mtendaji wa kata ambapo licha ya kuombwa watoe ushirikiano, hawakuwa tayari wakieleza kuwa jambo hilo limeshakuwa gumu kwao.
Katibu wa Baraza la Ardhi Kata ya Mbalibali, Chacha Nyangi ambaye baadaye alipatikana tena, alikiri kwamba uamuzi wa wazee wa mila umeathiri shauri namba 3/2015 lililowasilishwa na Chacha, kuhusu eneo lao kuvamiwa ambapo Yatacha alikimbilia kwa wazee wa mila.
Anasema kuwa inakuwa vigumu kuendelea kusikiliza shauri ambalo upande mmoja umetengwa na hauwezi kuchanganyika na watu wananchi wengine na kwamba ili kufikia uamuzi, majirani wanatakiwa kutoa ushahidi lakini ndiyo hao ambao kwa hukumu ya kimila, kuchangamana nao.
Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi Kata ya Mbalibali anasema kuwa uamuzi uliochukuliwa unakiuka haki kwa kuwa suala hilo lilikuwa kwenye chombo cha kisheria.
Mzee wa mila
Mzee wa mila wa Kijiji cha Koreri, Matinde Magoiga alipotakiwa kueleza sababu zilizowasukuma kutoa adhabu hiyo hadi kwa watoto alisema:
“Kulikuwa na dharau kutoka kwa familia ya Masero, tuliagiza eneo hilo wampe Yatacha, lakini wakakaidi na tukaambiwa kuwa walikuwa wanalima wakiwa na silaha za jadi. Tukaona tuwatenge.”
Kuhusu sababu za kuingilia chombo cha kisheria kilichokuwa kinasikiliza mgogoro huo na anayelima shamba hilo kwa sasa, alisema kuwa wao walipokea malalamiko wakaona wachukue hatua na kwamba hajui nani anayelima hapo. Kuhusu faini ya Sh 500,000 au ng’ombe wanaopokea kwa watu wanaoongea na familia ya Masero alisema wao hujilipa posho .

0 comments:

Post a Comment