Wanyama
aina ya swala wakiwa katika mawindo porini. Picha ya Maktaba.
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Posted Decemba27 2014 saa 10:34 AM
Posted Decemba27 2014 saa 10:34 AM
KWA UFUPI
·
Utafiti huo unaonyesha
kuwa kwa Shule ya Tamkeri ambayo inapakana na hifadhi ya Serengeti mahudhurio
ya wanafunzi mwaka 2013, yalikuwa ni asilimia 27 na mwaka huu ni asilimia
29, wakati Mugumu B ambayo ipo karibu na Mugumu mjini, mahudhurio yalikuwa mwaka
2013 asilimia 99 na mwaka huu ni asimilia 100.
Serengeti. Inawezekana likawa jambo ambalo siyo la kawaida, lakini
ndiyo hali ilivyo ya ujangili nchini hivi sasa, baada ya kubainika kuwa baadhi
ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari zilizopo kando kando ya hifadhi na
mapori ya akiba Wilaya ya Serengeti mkoani Mara wameacha masomo na kushiriki
ujangili wa wanyamapori kwa ajili ya kujipatia kipato.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa muda
mrefu unaonyesha kuwa wanafunzi wa shule za msingi wanaoshiriki ujangili huo ni
wa kuanzia darasa la nne hadi la saba na kwamba kazi hiyo wanaifanya kwa baraka
za wazazi wao.
Baadhi ya wazazi wa wanafunzi hao wameamua
kuwapa baraka watoto wao kuingia kwenye hifadhi kuwinda wanyamapori ili
wakikamatwa na maofisa wanyamapori wahurumiwe na kuachiwa kutokana na umri wao
mdogo.
Shule za msingi na sekondari zinazokabiliwa na
tatizo la utoro wa wanafunzi za Kata ya Sedeko, Mbalibali na Machochwe ambazo
ziko kando kando ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Mapori ya Akiba ya
Ikorongo na Gurumeti.
Uchunguzi wa gazeti hili uliofanywa katika
maeneo hayo na kuthibitishwa na walimu, waratibu elimu, madiwani, waendesha
mashtaka na wadau mbalimbali umebaini vitendo hivyo hufanywa kwa sababu
mbalimbali.
Jinsi ujangili
unavyofanyika
Chacha Joseph mkazi wa Kijiji cha Machochwe
anasema kuna aina nyingi ya uwindaji unaofanywa na wanafunzi hao mojawapo ni
wanafunzi kuwinda wanyamapori usiku wakiwa na ng’ombe wao ili kukwepa kuonekana
na askari wa hifadhi. Anasema hufanya kazi mbili kwa wakati mmoja, moja
kuwapatia malisho ng’ombe wao ambao hawana sehemu ya kuwalishia wakati wa
mchana na kufanya kazi ya uwindaji.
Uwindaji hufanywa kwa kutumia kurunzi
kubwa yenye mwanga mkali na njia ya pili ya kuwakimbiza wanyamapori wakiwa
katika makundi kuwaelekeza katika makorongo makubwa yaliyopo katika hifadhi hiyo
ambako hutumbikia na kufa.
Anasema wakiingia eneo la hifadhi huwaacha
ng’ombe wakiendelea kula majani, wao huelekea ndani zaidi ya hifadhi kutafuta
wanyamapori ambako hupatikana kwa wingi.
Chacha anasema kwa kutumia kurunzi maarufu
kama ‘kombora’ wanafunzi hao wakiwa katika kundi la watu 10 hadi 15, wakiwaona
wanyama kama vile swala, pofu, nyumbu huwafuata taratibu kisha kuwamulika
ghafla na kurunzi hiyo, hivyo kutokana na mwanga wake kuwa mkali
huwachaganya na hivyo, kwa kutumia mbwa na mikuki huwashambulia na
kuwaua.
Anasema njia hii ya uwindaji huwafanya waue
zaidi ya wanyama watano kwa siku.
Hata hivyo, anasema kwa njia ya kuwinda kwa
kuwafukuza wanyama kwa kuwaelekeza katika makorongo makubwa huua wanyama wengi
zaidi.
Anasema
njia hii huua zaidi ya wanyama 50 kwa mpigo kwa sababu wanyama wengi huwa
katika makundi makubwa hiyo wengi hutumbukia na kufa.
Chacha
anasema kazi hii hufanyika kuanzia saa 4.00 usiku hadi saa 10.00 alfajiri na
kwamba wakati wakiua wanyama huwa pia wanawasiliana na wazazi wao kwa ajili ya
kuratibu mtandao wa kuuza nyama hizo.
Nyama
hizo huuzwa katika maeneo ya kijiji walichotoka vijana hao na kama wamepata
nyingi huwa inasafirishwa kwa kutumia pikipiki usiku huo huo na vijana wakubwa
kupelekwa maeneo mengine ya Tarime na Rorya na wakati mwingine huvushwa hadi
nchini Kenya.
Ofisa wanyamapori
Ofisa
Wanyamapori mstaafu, Julius Nyigesa naye anasema ujangili unaofanywa na watoto
hao kama hautadhibitiwa utakuwa na madhara makubwa kwa kuwa wengi wao wanaacha
ujangili wa nyama na kujikita kwenye ujangili wa tembo na faru.
Anasema
kuna aina nne ya ujangili anaoufahamu unaofanywa na wanafunzi hao; ujangili wa
kutumia kurunzi kubwa, mbwa, mitego na kukaa muda mrefu porini wakiwasaidia
wazazi kuwinda tembo na wanyama wengine.
“Kuna
ujangili wa aina nne ninaoufahamu unaofanywa na hao watoto, wapo wanaotumia
kurunzi kubwa, mbwa na mitego na kulala huko kwa muda mrefu ambao unawafanya
wawe wazoefu porini kwa kuwa hubeba majukumu ya kupika, kusomba maji na
kukausha nyama,” anasema.
Anasema
baada ya muda watoto hao hutumiwa na majangili wakubwa kwa kuwa wanao uzoefu
mkubwa na mapori hayo kwa kujua wanyama wa aina fulani wanapatikana wapi na kwa
wakati gani na ulinzi ulivyo.
Sababu za kufanya ujangili
Nyigesa
anasema watoto hao kila mmoja ana sababu za kujiingiza katika ujangili.
Wapo
ambao wazazi wamezeeka hawawezi kuwahudumia hulazimika kwenda kuwinda ili
wapate fedha, wapo ambao wanaingia baada ya kuona wenzao wanafanya ujangili
wanapata fedha nyingi na wengine wanaingia ili waweze kupata fedha za michango
mbalimbali ya shule.
Nyisega
ambaye alikuwa askari wanyamapori Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti anasema
taarifa za wanafunzi hao kufanya ujangili zinafahamika na wazazi wao ama walezi
kwa kuwa hurejea nyumbani wakiwa na nyama na nyingine huuza na kununua mifugo
kama mbuzi na ng’ombe.
Hata
hivyo, watoto hao wakikamatwa hujitokeza na kudai kuwa hawakuwa wanajua.
Mstaafu
huyo anasema wakati mwingine wazazi huwaficha maeneo mbalimbali ikiwamo Wilaya
ya Tarime waliko na ndugu zao kisha hutoa taarifa kuwa watoto wao waliuawa
ndani ya hifadhi.
Kutokana
na mapato wanayopata wanafunzi wengi huamua kuacha kwenda shule.
Ofisa
wanyamapori huyo mstaafu anasema wanafunzi wengi waliokuwa wakiwakamata kwa
kujihusisha na ujangili wengi walikuwa wakikamatwa na kuchapwa viboko, kisha
kuachiwa na wale ambao umri wao ni mkubwa walikuwa wanapelekwa mahakamani.
Wakuu
wa shule wadai hali ni mbaya
Mkuu
wa Shule ya Sekondari ya Machochwe, Edna Nyambina na Mkuu wa Sekondari ya
Kitunguruma, Andrew Phares wanakiri kuwa ujangili na kilimo cha tumbaku umeathiri
sana masomo kwa kuwa wanafunzi ndiyo hutumiwa.
Wanasema
kuwa tatizo hilo linajulikana kwenye kamati za maendeleo za kata na wilaya kwa
kuwa wakati wanyama wanapoingia kwa wingi hasa nyumbu utoro nao huongezeka.
Mwalimu
mwingine ni Nyihita Chacha Nyihita ambaye mwaka jana alikuwa mwalimu mkuu wa
Shule ya Msingi Michochwe, anasema sababu kubwa ya utoro katika shule hiyo ni
wanafunzi kufanya kazi ya uwindaji wa wanyamapori na kilimo cha tumbaku.
Anasema
wanafunzi ambao wanashiriki kazi ya uwindaji ni kuanzia darasa la tano hadi la
saba.
“Utoro
ni mkubwa mno, wanafunzi wengi wanashiriki kazi ya uwindaji na kilimo cha
tumbaku na kuacha shule,” anasema.
Nyihita
ambaye alihamishiwa Shule ya Msingi Kibeyo iliyopo Mugumu mjini Februari mwaka
huu, anasema kazi ya uwindaji kwa wanafunzi wa shule za msingi inachochewa na
wazazi ili wajipatie kipato.
Anasema
baada ya kuona utoro unazidi kuongezeka aliwahi kushirikisha kamati ya shule
kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo, lakini alikwama kwa sababu wazazi hawakumpa
ushirikiano.
Nyihita
anasema ujangili kwa wanafunzi katika eneo hilo umekithiri kiasi kwamba
inafikia mahali hata wanafunzi wenyewe wanaoshiriki kuwinda wanyamapori
wanawapigia simu walimu kuwauzia nyama.
“Inashangaza
wanafunzi ambaye haji shule miezi miwili anakupigia simu akikuambia ‘Mwalimu
nina nyama hapa ya pofu au swala nikuletee kilo ngapi?” anasimulia mwalimu
huyo.
Anashauri
ili kumaliza utoro katika shule hizo wazazi wanapaswa kuacha kuwatumia
wanafunzi katika kazi za ujangili kwa sababu mbali ya kuwachosha wasifike
shuleni, pia wanapata fedha ambazo wanaona hakuna haja ya kwenda shule.
Madiwani
Diwani
wa Kata ya Machochwe, Samwel Gibewa anadai kuwa watoto hao walifanya kazi hiyo
zamani na kwa sasa hawafanyi ujangili, badala yake utoro mwingi unachangiwa na
kilimo cha tumbaku, kwa kuwa wanatumiwa na wazazi ama watu wengine kwa gharama
nafuu.
Naye
Chacha Nyikera Diwani wa Kata ya Sedeco alikiri kuwepo kwa utoro mkubwa kwa
wanafunzi wa shule za msingi na huchangiwa na mambo mengi, ikiwamo la ujangili
wa wanyamapori, wazazi wenyewe kutokuwa na mwamko na elimu.
Mahudhurio shuleni
Utafiti
uliofanywa na Shirika lisilokuwa la kiserikali la Hakielimu katika Shule za
Msingi Tamkeri, Mbalibali, Mugumu B na Kambarage zilizopo kando ya Hifadhi ya
Serengeti unaonyesha kuwa mahudhurio ya wanafunzi shule hizo yanatofautiana
kulingana na shule ilivyo karibu na hifadhi.
Kwa
shule ambazo zipo karibu na hifadhi mahudhurio ya wanafunzi ni mabaya kutokana
na baadhi yao kushiriki katika ujangili usiku na hivyo kushindwa kufika shuleni.inaendelea.
0 comments:
Post a Comment