Ghati Kisiba (75 mkazi wa kitongoji cha Mereshi Kijiji cha Robanda wilayani Serengeti ambaye alikamatwa na kupigwa na wananchi kwa tuhuma za uchawi amefariki.
Serengeti:Mtuhumiwa mmoja kati ya
wanne waliokamatwa kwa matukio
yanayodaiwa ya kishirikina katika kitongoji cha Mereshi kijiji cha Robanda
wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara amefariki.
Kamanda wa polisi wilaya ya
Serengeti Pius Mboko amemtaja aliyekufa kuwa ni Ghati Kisiba (75)mkazi wa
kijiji cha Robanda,ambaye amefia Teule
ya wilaya ya Nyerere alikopelekwa jana
baada ya hali yake kubadilika ,chanzo
cha kifo chake kitajulikana baada ya uchunguzi kufanyika.
Kamanda huyo alisema mtuhumiwa
mwingine Chausiku Kyahama Mahiti(61)naye amepelekwa hospitali kwa ajili ya
kupata matibabu ,”walipigwa na wananchi kabla ya kuwaokoa huko hivyo mmoja
amepelekwa hospitali ili kupata matibabu kutokana na majeraha aliyopata”alisema
kamanda.
Hata hivyo Mganga mkuu wa
hospitali hiyo Kelvin Mwasha akiongea na Serengeti Media Centre kwa njia ya simu
kuhusiana na tukio hilo ,alisema Ghati
alifikishwa hospitali akiwa amekufa hivyo hawakuweza kumtibu.
“Hakutibiwa hivyo hatuwezi kusema
chanzo ni nini mpaka tufanye uchunguzi(post mortem) ndugu wa marehemu hawapendi
kufanyika kwa uchunguzi kujua chanzo cha kifo…..katika hatua ya kwanza tumebaini mwili wake haukuwa na jeraha lolote.”alisema.
Alisema alifikishwa hospitali na
ndugu zake wala si polisi kama ilivyodaiwa na kamanda wa polisi wilaya na baada
ya kufika mapokezi na kubaini kuwa ameisha kufa walilipia gharama za kuhifadhi
maiti.
Februari 7 majira ya saa 3.30
usiku mwaka huu Matiko Mkeya(20)anayefanya kazi ya kuchunga ng’ombe mali ya
Stephen Nyamkinda alipotea ghafla akiwa ndani,na februari 8 msako ulianza kwa
kushirikisha wakazi wa kitongoji cha Mereshi na hatimaye kijiji kizima cha
Robanda.
Katika msako huo walifanikiwa
kumkuta akiwa katika bafu la Chatu Mkali na Chausiku Mahiti huku akiwa amefungwa sanda nyeupe yenye maandishi
mekundu ya namba 7 , akiwa hajitambui,baada ya Chausiku kupigwa alikiri kuhusika
na kumchukua kijana huyo kwa njia za kishirikina na kutaja mtandao wake.
Miongoni mwa mtandao wake ni
marehemu Ghati Kisiba ,Wisaka Makuru(43)na Chatu Mkali,ambao walipigwa na
nyumba 7 za watuhumiwa hao zikateketezwa kwa moto,na polisi wa kituo kidogo cha
Robanda baada ya kuzidiwa waliomba msaada wa askari kutoka wilayani
waliofanikiwa kuwachukua mikononi mwa wananchi waliokuwa wanataka kuwaua.
Hata hivyo baada ya kuchukuliwa
kwa watuhumiwa waumini wa makanisa mbalimbali wakiongozwa na kanisa la EAGT anakosali
Mkeya waliendesha maombi hadi fahamu zikamrudia,na kubainisha kuwa chanzo cha
mkasa huo ni maziwa kwa kuwa mtuhumiwa Chausiku na mmewe Chatu Mkali
walishindwa kulipa deni,ndipo wakaahidi kumshughulikia.
Wakiongea na hazeti hili
watuhumiwa wakiwa polisi walisema kuwa walionewa,huku Chausiku akikiri kumtaja
Ghati baada ya kuzidiwa na makosa na kuwa aliamua kumtaja tu,hata hivyo
ilibainika kuwa walikuwa hawaelewani alimtaja kama njia ya kumkomoa.
Polisi wamesema wanaendelea na
uchunguzi wa mkasa huo,huku wakikiri kuwa watuhumiwa hawawezi kuwaruhusu kurudi
kijijini kwa kuwa wanaweza kuuawa.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment