Na Salome Kitomary
24th March 2015
Rais Jakaya Kikwete.
Rais Jakaya Kikwete, amelitaka Jeshi
la Polisi kuacha kutumia nguvu kubwa katika kukamatwa wahalifu, badala
yake kuweka mbele suala la haki za binadamu.
Rais alitoa angalizo hilo jana
jijini Dar es Salaam katika Chuo Kikuu cha Polisi, wakati wa hafla ya
kuwapandisha vyeo askari 290 wa Zanzibar na Bara waliomaliza mafunzo ya miezi
sita.
“Ipo haja ya kutumia mbinu
mbalimbali katika kuwakamatwa watuhumiwa kuliko matumizi ya nguvu kubwa,
jitahidini sana kutumia nguvu kiasi ili kuhakikisha hamvunji haki za binadamu,”
alisema.
Rais Kikwete aliwataka polisi
kujenga mazingira rafiki na wananchi ili kurahisisha utendaji kazi ikiwamo
kukabiliana na uhalifu nchini kwa kupata taarifa mbalimbali kwa urahisi.
Rais Kikwete pia alisema wizi wa
mtandaoni ni tatizo kubwa na zinahitajika nguvu za ziada kupambana nalo na
polisi wanapaswa kujipanga kikamilifu na kwamba kwa sasa kuna matumizi mabaya
ya mitandao ya kijamii ambayo inatumika kutukana, kukashfu watu jambo ambalo ni
kinyume cha sheria.
“Naliagiza Jeshi la Polisi kuchukua
hatua dhidi ya wahusika wote wa matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii,”
alisema.
Aidha, alisema mauaji yanayotokana
na wananchi kujichukulia sheria mkononi yameongezeka kutoka 2,075 mwaka 2005
hadi 3,775 mwaka 2015, hasa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi ambayo
yameliabisha Taifa na kwamba zinahitajika jitihada kuyamaliza.
Awali, Mkuu wa Polisi nchini, IGP
Ernest Mangu, alimuomba Rais kuangalia uwezekano wa kuongeza vifaa vya kisasa
kwa jeshi hilo ili liweze kutekeleza majukumu yake vizuri hasa kwa kipindi hiki
ambako Taifa litashiriki kura ya maoni kwa Katiba inayopendekezwa na uchaguzi
mkuu Oktoba mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment