Siri ya ufaulu Shule ya Msingi ya Twibhoki
Mkuu wa shule ya Twibhoki, Alphonce
Magori., Picha na Antony mayunga
Na Antony Mayunga, Mwananchi
Posted Jumanne,Novemba11 2014 saa 12:39 PM
Posted Jumanne,Novemba11 2014 saa 12:39 PM
Kwa ufupi
Ndiyo kinara wa ufaulu katika
mtihani wa kumaliza darasa la saba mwaka 2014 kati ya shule 15,867
Ni mafanikio makubwa ya kitaaluma
kwa shule iliyoshika nafasi ya 28 mwaka jana, kukwea hadi hadi nafasi ya kwanza
mwaka huu.
Hii ni Shule ya Msingi ya Twibhoki
iliyopo Mugumu wilayani Serengeti. Imekuwa kinara katika matokeo ya mtihani wa
darasa la saba yaliyotangazwa wiki iliyopita na Baraza la Mitihani la Tanzania
(Necta).
Sio matokeo ya kubahatisha na wala
haikuwa ajabu kwa shule hiyo kuwa ingefanya vizuri mwaka huu. Mikakati ya
kitaaluma pamoja na moyo wa kujituma na uwajibikaji, vimechangia mafanikio ya
shule hiyo inayomilikiwa na mtu binafsi.
Siri ya ufaulu
Elimu ni mikakati, vifaa, ubunifu na
uwajibikaji na wala sio majengo yenye mvuto. Ufikapo Twibhoki mazingira ya
shule hayana mvuto wa kutisha, lakini hapo ndipo wanapojifunza wanafunzi wengi
walioibuka vinara katika mtihani wa mwaka huu.
“Hatukubahatisha kushika nafasi ya
kwanza kitaifa, bali rekodi yetu inajieleza kitaaluma kuwa tumekuwa tukifanya
vizuri,” anasema mwalimu wa taaluma, Mseti Charles.
“Mafanikio yoyote hutokana na
malengo mnayojiwekea na namna ya kuyafikia. IIi kukuza taaluma tumekuwa na
malengo ya wiki, mwezi na kuendelea, haya yanajumusiha kuwapa mazoezi
mbalimbali wanafunzi ambayo hutusaidia kujua uwezo wa kila mmoja na namna ya
kumsaidia.’’
Anasema tangu mwaka 2008 wamekuwa
wakifanya vizuri katika matokeo hayo kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa na sasa
taifa. “Hayo ni matokeo ya kufanya kazi kama timu na kufuatilia malengo
tunayojiwekea,” anasema.
Akiwa amejaa furaha isiyo kifani,
mwalimu mkuu wa shule hiyo, Alphonce Magori kwanza anamshukuru Mungu kwa kuwa
ufaulu huo umetokana naye. Lakini anaongeza kusema kingine kilichosababisha
ufaulu mkubwa ni kila mdau wa shule kufanya kazi kwa kujituma.
“Kwanza ni mapenzi ya Mungu,
tunamweka yeye kwanza kabla ya kazi zingine, lakini pia uongozi wa shule
unatambua nafasi na umuhimu wa kila mtumishi, wajibu wake na tunapata muda wa
kujitathmini kama malengo yanafikiwa,” anasema.
Anasema ili kujua kama malengo
waliyojiwekea yanafikiwa, hufanya tathmini inayowashirikisha pia wanafunzi kwa
kupima uelewa wa wanayofundishwa.
“Nyinyi waandishi mnafanya vikao
asubuhi kabla ya kuanza kazi, ili kutathmini kazi ya jana na nini mfanye siku
hiyo. Nasi hapa kabla ya kufanya kazi yoyote, tunamshukuru Mungu na kujipanga
kwa kuangalia nini tumepanga na tufanye nini ili tufanikiwe,” anaeleza mwalimu
Magori.
“Wanafunzi wanamaliza silabasi na kurudia, pia wanapata muda wa kujisomea
vitabu vya kiada ili kupata maarifa zaidi. Kila wiki wanafanya majaribio ya
kupima uelewa, wasiofanya vizuri tunawasaidia.’’Tofauti na ilivyo kwa wamiliki wengi wa shule wanaoweka mbele maslahi badala ya maendeleo ya shule, meneja wa shule hiyo, Grace Godfrey anasema kwao kipaumbele ni kuhakikisha ada wanayotoza kwa watoto inafanana na matokeo.
Ni kwa sababu hiyo, anasema wazazi wengi wamekuwa wakivutika kusajili watoto wao katika shule yake.
Ilipotoka Twibhoki
Shule ya Msingi ya Twibhoki ilianza mwaka 2003. Katika mtihani iliyotoa wahitimu wa kwanza mwaka 2008, shule hiyo iliwashtua watu wengi kwa kushika nafasi ya kwanza kitaifa. Na mwaka mmoja baadaye ikateleza na kushika nafasi ya tatu.
Mwaka 2010, ikashika tena nafasi ya kwanza, kisha nafasi ya tatu mwaka 2011. Mwaka uliofuata shule ilifutiwa matokeo na ilipoibuka tena mwaka 2013 ikashika nafasi ya 29.
Wanafunzi waliofanya vizuri
Anna Bhoke(12) Wambura anasema siri ya kufanya vizuri somo la hisabati ni Mungu anayemwongoza, walimu na wazazi wake anaosema wamekuwa mstari wa mbele kufuatilia maendeleo yake kitaaluma.
“Matokeo haya yananipa hamasa kubwa sana, sasa nategemea kuanza safari ya kwenda hatua nyingine. Najua kuna changamoto, lakini kwa mapenzi ya Mungu nitazikabili. Misingi niliyojengewa shuleni na nyumbani itakuwa nguzo yangu,” anasema mwanafunzi huyo kwa kujiamini.
Anasema anatarajia kufanya vizuri zaidi ili afikie malengo yake ya kuwa daktari, kazi ambayo ameipenda tangu akiwa mdogo na anaamini atafikia malengo yake.
Kwa upande wake, Rolly Ged (16) anasema matokeo hayo anayachukulia kuwa ni chachu ya safari yake ya maisha ili kufikia malengo yake kimaisha.
Kama ilivyokuwa kwa mwenzake anasema kwake Mungu ni wa kwanza. Anaamini ndiye amekuwa kiongozi wake na hivyo mafanikio hayo anamrudishia shukrani.
Kuhusu fani anayoipenda, anasema: “Natarajia kuwa mhandisi. Mungu akinijaalia uhai nitafikia hatua hiyo maana nia ninayo na uwezo ninao, ingawa ni safari ndefu lakini yote yanawezekana.”
Newton Kamuzola ni mzazi wa mmoja wa wanafunzi bora shuleni hapo na kitaifa. Anasema mafanikio ya mtoto wake yanatokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya wazazi na walimu.
0 comments:
Post a Comment